Friday, March 24, 2023

KAMATI YA KUCHAKATA DATA ZA HALI YA HEWA DUNIANI YAKUTANA TANZANIA

Arusha, Tanzania; Tarehe 20/03/2023 Tanzania imekuwa mwenyeji wa mkutano wa Kamati ya Kuchakata Data za Hali ya Hewa Duniani, lengo ikiwa ni kuhakikisha data za hali ya hewa zinatumika ipasavyo na taasisi za hali ya hewa katika nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na kwa manufaa ya sekta mbalimbali. Mkutano huo unaojumuisha wajumbe kutoka nchi kumi na mbili (12). Akizungumzia umuhimu wa mkutano huo kwa nchi, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Hamza Kabelwa, alisema “ kwanza ni kutangaza utalii wa nchi yetu ambapo wageni hawa watakuwa mabalozi wa vivutio vya Tanzania katika nchi zao, aidha, kutokana na changamoto kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, upatikanaji data sahihi za hali ya hewa ni muhmu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania katika kusaidia kukabiliana na mabadiliko hayo ili kutoa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”. Naye, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. David Richardson, alisema Kamati anayoisimamia itajikita katika kusaidia kujenga uwezo na kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji wote ili kulinda maisha ya watu na mali zao. Kwa upande wake, Dkt. Anthony Rea, Mkurugenzi wa Idara ya Miundombinu WMO alisema, majukumu ya kamati hiyo yanaenda sambamba na jitihada mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na WMO za kusaidia nchi katika kufanikisha upatikanaji wa data za uangazi za hali ya hewa ambazo zinazaa taarifa za hali ya hewa kwa matumizi ya nchi wanachama wa WMO. Nchi zinazoshiriki mkutano huo unaofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) kuanzia tarehe 20 hadi 24 Machi, 2023 ni Australia, Brazil, Canada, Finland, Ufaransa, Ujerumani, Korea ya Kusini, Japan, Afrika Kusini, Hispania, Uingereza na Marekani.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...