Friday, March 24, 2023

TANZANIA YAADHIMIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 2023

Dodoma; Tarehe 23 Machi, 2023; Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeungana na nchi nyingine wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani yenye Kauli Mbiu “Mustakabali wa Hali ya Hewa, Tabianchi na Maji kwa Vizazi vyote”. Akizungumza na wanahabari, Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Uchukuzi), Mh Atupele Mwakibete (MB) alisema “Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani. Kila mwaka ifikapo tarehe 23 Machi, Jumuiya ya Hali ya Hewa Ulimwenguni kote husherehekea siku hii, kukumbuka kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani ambapo Mkataba wa Uanzishwaji wa WMO ulisainiwa rasmi tarehe 23 Machi mwaka 1950.” Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathamini mchango wa huduma za hali ya hewa katika maendeleo ya kijamii na uchumi wa nchi, hivyo serikali imefanya juhudi za dhati katika kuwekeza kwenye sekta ya hali ya hewa. “Katika kutatua changamoto kwenye sekta ya hali ya hewa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitunga sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ya mwaka 2019, ambayo ilihuisha utoaji wa huduma za hali ya hewa nchini Tanzania na kuiongezea Mamlaka jukumu la udhibiti na uratibu wa shughuli za hali ya hewa nchini. Lengo likiwa ni kuongeza uwezo wa kitaasisi ili kusaidia uboreshwaji wa huduma za hali ya hewa.” Alisema, Mhe. Mwakibete. Aidha, Mh. Mwakibete alieleza kuwa katika kuhakikisha taarifa za hali ya hewa zinatolewa kwa usahihi na uhakika, Serikali ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma za hali ya hewa. Miongoni mwa uwekezaji ni ununuzi wa Miundombinu ya kisasa ya uchunguzi wa hali ya hewa ikiwa pamoja na rada za hali ya hewa, Katika kuadhimisha siku hii muhimu duniani, TMA imewakumbusha watanzania na wadau wote wa hali ya hewa kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi duniani. Akifafanua Zaidi suala hilo kwa wanahabari, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema “Maadhimisho ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2023 yamekuja wakati muafaka ambapo mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi yanazidi kuongezeka na athari zake zinaonekana kila mahali na kuleta maafa ambayo yamesababishwa na ongezeko la idadi na ukubwa wa matukio ya hali mbaya ya hewa. Kwa mfano katika siku chache zilizopita, maeneo na nchi za kusini magharibi mwa Bahari ya Hindi yalikumbwa na kimbunga Freddy ambacho kilikuwa na nguvu kubwa na kilidumu kwa muda mrefu na kusababisha maafa makubwa na uharibifu wa mali, miundombinu na shughuli za kiuchumi katika nchi za Msumbiji, Malawi na Madagascar”. “Tanzania kama zilivyo nchi nyingine imeendelea kuathiriwa na kuongezeka kwa matukio ya hali mbaya ya hewa na maji yaliyosababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa wastani, joto la dunia limeongezeka kwa takribani nyuzi joto 1° na kwa upande wa Tanzania katika miaka michache iliyopita ongezeko la joto lilifikia takribani nyuzi joto 0.3 – 0.8 kwa kipimo cha sentigredi.” Alisisitiza Dkt. chang’a. Dkt. Chang’a aliwahakikishia watanzania na wadau wote wa hali ya hewa kwamba TMA itaendelea kutoa huduma bora za hali ya hewa zenye viwango vya kimataifa na watanzania watumie huduma hizi katika kufanya maamuzi ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kijamii na za kiuchumi. “Tunaposherehekea kumbukizi ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) na miaka 150 ya Shirika la Kimataifa la Hali ya Hewa (IMO), tungependa kuihakikishia jamii na wateja wetu kuwa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ni miongoni mwa Taasisi bora za hali ya hewa katika Bara la Afrika na katika nchi zinazoendelea na imedhamiria kutoa huduma bora za hali ya hewa zinazokidhi au kuzidi matarajio ya wateja wetu na zinazozingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa, kwa kuendelea kuboresha taratibu zetu za kazi. Hivyo, napenda kutoa wito kwa wadau wote kuzitumia ipasavyo taaarifa na huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA ili kuongeza tija na ufanisi katika kupanga, kufanya maamuzi na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.” Dkt. Chang’a.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...