Dar es Salaam, Tarehe 22/02/2023;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2023 kwa maeneo yanayopata mvua
mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika
Ofisi za TMA-Dar es Salaam, Ubungo Plaza, tarehe 22/02/2023, Kaimu Mkurugenzi
Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata
misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya
wastani.
“Mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa
katika maeneo mengi ya nchi yayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka isipokuwa
maeneo machache ya mikoa ya Dar es Salaam, pwani (ikijumuisha mafia),kaskazini
mwa Morogoro pamoja na Kisiwa cha Unguja ambapo mvua za wastani hadi juu ya wastani
zinatarajiwa”. Alisema Dkt. Chang’a.
Aidha, aliongezea kuwa “Ongezeko la
mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Mei 2023, hususan katika maeneo ya
pwani ya kaskazini”.Alisema Dkt. Chang’a.
Mvua za Masika zinatarajiwa kuanza mwezi
Machi 2023 katika maeneo mengi na zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya
Mwezi Mei 2023, katika maeneo mengi ingawa mwendelezo wa mvua za nje ya msimu
unatarajiwa mwezi Juni 2023 katika maeneo machache ya mikoa ya Tanga, Dar es
Salaam, Morogoro kaskazini, Pwani, Kisiwa cha Mafia, kisiwa cha unguja na Pemba.
Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza,
Dkt. Chang’a alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza
kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha,
milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.
Kwa taarifa zaidi tembelea; www.meteo.go.tz https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast
No comments:
Post a Comment