Kibaha, Pwani 06 - 07/02/2023
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dkt. Ladislaus Chang’a amewataka watumishi wa TMA kutumia kauli mbiu ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo.
Dkt. Chang’a aliyasema hayo wakati akifungua rasmi mafunzo ya kuongeza uwezo kwa wataalam wa TMA katika utabiri wa mvua za msimu.
“Watumishi wote mnatakiwa kuangalia namna gani tunaweza kuishi kwa vitendo kauli mbiu ya Kazi Iendelee kwa kuzingatia weledi na umahiri mkubwa, kauli ambayo Mhe. Rais amekuwa akiisisitiza kila wakati”. Alisema Dkt. Chang’a.
“Sisi, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) jukumu letu la msingi ni kutoa utabiri wa hali ya hewa hivyo mafunzo haya yatasaidia kuendeleza kazi yetu ya msingi na kutoka viwango tulivyopo kwenda viwango vya juu zaidi ikiwa ni maana halisi ya kazi iendelee”. Alisisitiza Dkt. Chang’a.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, Dkt. Hamza Kabelwa alisema mafunzo hayo ni kwaajili ya kuwajengea uwezo wataalam wa TMA na kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwa wadau mbalimbali.
Warsha hiyo muhimu ya mafunzo juu ya utabiri wa mvua za msimu ilifanyika katika ukumbi wa mikutano wa TARI, Kibaha, Pwani, Tarehe 06 – 07 Februari, 2023 kwa ufadhili wa Taasisi ya Utafiti ya Norway ya Michelsen ambayo ni mtekelezaji wa mradi wa wa Huduma za Hali ya Hewa zinazozingatia jinsia kwa usalama wa chakula na lishe (COGENT). Lengo la mradi ni kuboresha huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA kwa sekta mbalimbali katika kulinda maisha na mali za watu.
No comments:
Post a Comment