Wednesday, April 27, 2022

TMA YAJIPANGA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU MBALIMBALI WA HALI YA HEWA ZANZIBAR

Mkurugenzi wa TMA - Zanzibar, Ndg. Mohammed Ngwali, akizungumza na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwenye maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.










Matukio mbalimbali kwa picha wakati wataalam wa TMA wakitoa elimu ya hali ya hewa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali waliotembelea banda la TMA, kupitia maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.  


Mkurugenzi wa TMA - Zanzibar, Ndg. Mohammed Ngwali, akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam wa hali ya hewa kupitia maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.

 

Zanzibar, Tarehe 26/04/2022

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni Taasisi ya Muungano ambayo inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria Tanzania Bara na Zanzibar ambapo huduma tunazotoa zina umuhimu mkubwa kwa jamii kwa sababu zimelenga katika kuokoa maisha ya watu na mali zao pamoja na kukuza uchumi wa nchi. Mamlaka imejipanga kudumisha ushirikiano na wadau mbali mbali wa hali ya hewa hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuimarisha usalama kwa jamii na kuinua uchumi kupitia huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi”. Aliyasema hayo Mkurugenzi wa TMA – Zanzibar, Ndugu Mohamed Ngwali wakati wa maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22/04 – 06/05/2022

Aidha, Ndugu Ngwali alisisitiza kuwa zipo njia mbali mbali ambazo wadau na wananchi wanaweza kutumia kupata taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na tovuti ya TMA, luninga, redio, magazeti, mitandao ya kijamii na pia wanaweza kufika katika Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa zilizopo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume, Zanzibar na Uwanja wa ndege wa Pemba.

Sambamba na hilo wataalam wa hali ya hewa wa TMA wameendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, usafiri wa anga na maji ili kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na kuongeza uzalishaji kupitia sekta zao. Vilevile elimu hii husaidia katika kuepusha majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa sambamba na kutambua njia zitumikazo na Mamlaka katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa wadau na wananchi kwa ujumla.

Katika manesho haya, wageni mbalimbali wameweza kutembelea banda la TMA na wameonesha kufurahishwa na huduma zinazotolewa na Mamlaka. Aidha, TMA inaendelea kutekeleza jukumu hili kwa umakini wa hali ya juu na kuongeza ushirikiano zaidi na jamii ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata na anatambua umuhimu wa huduma hizi muhimu za hali ya hewa na kuzitumia kwa usahihi na kwa wakati ili kuepuka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa yanayoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...