Dar es Salaam
Tarehe 12/04/2022.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na waandishi wa habari
kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa ikiwa
ni maandalizi ya kurejea utabiri wa MASIKA uliotolewa Februari 2022. Akizungumza
na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, amesema mifumo ya hali ya hali
ya hewa imebadilika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea kubadilika
kwa mwenendo mzima wa mvua za msimu wa MASIKA 2022. Aliyazungumza hayo alipokuwa akifungua warsha ya wanahabari
iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya TMA, Ghorofa ya tatu,
Ubungo Plaza, tarehe 12/04/2022.
“Tanzania tumeanza kuziona athari za
mabadiliko ya tabia nchi, katika mifumo ya hali ya hewa hasa kubadilika kwa joto
la bahari ambalo kwa kawaida halibadiliki kwa haraka kutokana na tabia ya maji
kutunza joto lake kwa muda mrefu.” Alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi alisema kuongezeka kwa joto
duniani (global warming) kunasababisha kuyeyuka kwa barafu zilizoko katika ncha
za dunia na hivyo kuongeza vina vya bahari katika maeneo mbalimbali duniani
ikiwa Pamoja na kubadilika kwa hali ya joto la bahari na hivyo kuathiri mifumo
ya hali ya hewa.
Aidha Dkt. Zewdu Segele ambaye ni mtaalam wa
masuala ya hali hewa kutoka kituo cha utabiri na matumizi ya hali hewa (ICPAC)
alisema, ICPAC imetoa mrejeo wa utabiri wake wa Machi – Mei ambao iliutoa mwezi
Februari. Dkt. Zewdu alisema mifumo ya awali ilionyesha uwepo wa mvua za juu ya
wastani katika nchi za pembe ya Afrika ikiwemo Tanzania, lakini baada ya mifumo
kubadilika nchi hizo sasa zitapata mvua za chini ya wastani.
Dkt. Zewdu aliongeza kusema utabiri unaotolewa
na ICPAC ni wa maeneo makubwa hivyo nchi wanachama wana jukumu la kuandaa
utabiri wa maeneo madogo madogo katika nchi zao.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia
kutoa rasmi mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa Masika (MAM) 2022 Tarehe 13/04/2022.
No comments:
Post a Comment