Dar es Salaam, Tarehe 13/04/2022:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa MASIKA 2022, uliotolewa rasmi Februari 2022 kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara mbili kwa mwaka, ikijumuisha maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za juu Kaskazini Mashariki pamoja na Pwani ya Kaskazini. Katika mrejeo huo TMA imetoa uchambuzi wa mwenendo mzima wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo uliohuishwa wa msimu wa nvua katika kipindi cha Machi hadi Mei 2022 pamoja na ushauri kwa wadau kutoka sekta mbalimbali.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi ameelezea sababu zilizosababisha kuwepo kwa vipindi virefu vya ukavu hususan kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki kuwa ni pamoja na kujitokeza kwa vimbunga katika Bahari ya Hindi pamoja na mabadiliko ya muda mfupi ya joto la bahari.
“Kumekuwa na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha mwezi Machi, 2022 hususan kwa maneo ya pwani ya Kaskazini na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki ambapo maeneo hayo yalipata vipindi virefu vya ukavu, hali iliyosababishwa na matukio ya vimbunga katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji, pamoja na kujitokeza kwa mabadliko ya muda mfupi ya joto la bahari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”, Alisema Dkt. Kijazi.
Dkt. Kijazi alisisitiza kuwa pamoja na maeneo mengi yanayopata mvua za msimu mara mbili kwa mwaka kutarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani katika msimu huu wa mvua za MASIKA 2022, watumiaji wa utabiri wanatakiwa kuzingatia kuwa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza katika maeneo hayo sambamba na kuwataka kupata ushauri wa kitaalam kutoka kwa maafisa wa sekta zao.
Aidha katika hotuba yake mapema asubuhi alipokuwa akifungua warsha ya wadau iliyotangulia kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Dkt. Kijazi aliwataka wadau kutumia mrejeo mpya wa utabiri wa msimu wa mvua za Masika katika mipango yao ya maendeleo hapa nchini.
Kwa taarifa zaidi tembelea: https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast
No comments:
Post a Comment