Dodoma, Tarehe 21/04/2022:
Waziri wa Ujenzi na
Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) ametoa wito kwa wadau wanaotumia
huduma za hali ya hewa kibiashara kuhakikisha wanatimiza takwa la kisheria la
kuchangia huduma hizo. Alizungumza hayo alipokuwa akifungua rasmi mkutano wa
Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), uliofanyika
katika ukumbi wa Kilimani Land Mark – Dodoma, Tarehe 21/04/2022
“Kuchangia huduma za hali ya hewa ni suala la
kisheria hivyo kila mdau hana budi kulitekeleza. Wakati serikali inatekeleza
jukumu hilo, natoa wito pia kwa wadau wanaotumia huduma hizo kibiashara kuhakikisha
wanatimiza takwa hilo la kisheria la kuchangia huduma za hali ya hewa ili
ziweze kuboreshwa zaidi”. Alisisitiza Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine mheshimiwa Prof. Mbarawa aliwapongeza wadau wote walio onesha ushirikiano kwa
kujitokeza kusajili vituo vyao na kuchangia gharama za utoaji huduma mahususi
zinazotolewa katika sekta zao na hivyo kukidhi matakwa ya Sheria ya Mamlaka ya
Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 pamoja na kanuni zake. Aliwaelekeza TMA
kuongeza juhudi na kuhakikisha sekta zote ambazo hawajaanza kuchangia huduma za
hali ya hewa wanachangia kama sheria inavyoelekeza. Prof. Mbarawa aliwapongeza
TMA kwa kuiwakilisha vyema nchi katika shughuli za hali ya hewa kimataifa na
kuendelea kushikilia cheti cha ubora cha ISO 9001-2015.
Katika kutatua changamoto zinazoikabili TMA, Prof. Mbarawa aliahidi Wizara kuendelea kuiwezesha Mamlaka kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo ili kuhakikisha miundo mbinu ya hali ya hewa inaboreshwa. Aliongeza kusema maslahi ya watumishi pia yataboreshwa hivyo aliwataka wataalam wa hali ya hewa kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati serikali inashughulikia uboreshaji wa maslahi.
Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa TMA na kuwapatia mazingira bora ya kazi yanayowawezesha kutekeleza vyema jukumu lao la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Hali iliyopelekea kuendelea kuitambulisha Tanzania katika nyanja za hali ya hewa kimataifa na kumuwezesha Makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na wataalam wa hali ya hewa walioko katika vikosi kazi vya Shirika hilo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Kwa upande wake
Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alielezea dhumuni kuu la Baraza hilo la
Wafanyakazi kuwa ni kupitia bajeti ya Mamlaka ya mwaka 2022/2023 na kufanya
tathmini ya utendaji wa Mamlaka itakayosaidia kuongeza ubora na ufanisi katika
utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali
ya hewa na tabia nchi zinazoikabili Dunia. Aidha, aliishukuru serikali kwa
kuboresha miundo mbinu ya hali ya hewa nchini na kuwajengea uwezo wataalam hali
iliyoiwezesha TMA kukosa dosari yoyote wakati wa ukaguzi wa kimataifa
uliofanyika Desemba, 2021 na hivyo kuendelea kumiliki cheti cha ubora cha ISO.
No comments:
Post a Comment