Mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa wakati akifungua rasmi Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika (Machi hadi Mei, 2022) kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022.
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali katika picha ya pamoja na mgeni rasmi katika katika Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika 2022 katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022. Utabiri huo unatarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 17 Februari 2022 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania.
Tanga; Tarehe 14 Februari, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wanahabari wote nchini kuendelea kuwa mabalozi wa kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa nchini. Hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa wakati akifungua rasmi Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika 2022 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022.
“Mamlaka inamchango mkubwa katika ukuaji wa kiuchumi kwa vile huduma za hali ya hewa ni mtambuka na zinahitajika katika kila sekta.Napenda kuwakumbusha kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa TMA na daraja kati ya TMA na jamii katika kuelezea na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zetu za kila siku”. Alisema Dkt. Kabelwa.
Aidha, Dkt. Kabelwa alivipongeza vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wake katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na wakati, na kukiri kuwa faida ya kuendelea kufanyika kwa warsha za wanahabari kabla ya kutoa utabiri wa msimu zimeendelea kuonekana.
“Kama mnavyofahamu, warsha hii ni muendelezo wa warsha nyingine nyingi ambazo zimekuwa zikifanyika ikiwa ni juhudi za Mamlaka kutaka kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati. Napenda kukiri kuwa faida za warsha hizi kwa sisi TMA tumeziona kwani mwamko wa jamii sasa hivi umekuwa mkubwa na hata taarifa zinazorushwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari zimekuwa katika lugha rahisi na inayoeleweka kwa jamii, hivyo kwa hatua hii napenda kuwapongeza na muendelee kuongeza bidii ili kufikia malengo ya juu na kuwafikia watanzania wote kwa wakati”. Alieleza Dkt. Kabelwa.
Kwa upande wake mwandishi wa habari kutoka gazeti la Majira, Bi. Penina Malundo alisema kuwa warsha za mafunzo kutoka TMA zimeendelea kuwajengea uwezo hivyo kuwasaidia katika uandishi wa taarifa sahihi bila kupotosha umma na kuwezesha jamii na wadau kujipanga na kuandaa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.
Katika warsha hiyo, wanahabari walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2022, ambao ni mahsusi kwa maeneo ya Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha,Kilimanjaro, Manyara), Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia), Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja, Ukanda wa Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita,Mara, Simiyu na Shinyanga) pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za MASIKA 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 17 Februari 2022.
No comments:
Post a Comment