Wednesday, October 27, 2021

SEKTA MBALIMBALI ZASHAURIWA KUJIPANGA KUKABILIANA NA UPUNGUFU WA MVUA ZA MSIMU WA NOVEMBA 2021 HADI APRILI 2022 UNAOTARAJIWA KUJITOKEZA






Dar Es Salaam, Tarehe 27/10/2021.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka, ikijumuisha mikoa iliyopo magharibi mwa nchi ( Kigoma, Tabora na Katavi), yyanda za juu kusini magharibi (Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa), katikati mwa nchi (Dodoma na Singida), pwani ya kusini (Lindi na Mtwara), mkoa wa Ruvuma pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2021 hadi Aprili, 2022.

Akiwasilisha utabiri huo kwa waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi alisema kuwa, utabiri huo wa mvua za msimu unatarajiwa kuwa wa wastani hadi chini ya wastani hivyo kuwataka wadau kutoka sekta mbalimbali kuzitumia taarifa hizi za hali ya hewa kwa kujipanga ili kukabiliana na matarajio hayo.

“Natoa ushauri kwa wadau wa sekta mbalimbali wanaotumia taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile kilimo na usalama wa chakula, mifugo na uvuvi, maliasili, wanyamapori na utalii, nishati na maji, usafirishaji (nchi kavu, kwenye maji na angani), mamlaka za miji, afya, sekta binafsi pamoja na menejimenti za maafa kujipanga na kutumia njia ambazo zitaweza kukabiliana na upungufu wa mvua unaotarajiwa kujitokeza katika kipindi cha mwezi  Novemba, 2021 hadi Aprili, 2022” Alisema Dkt. Kijazi

Dkt. Kijazi aliongezea kusema, mvua hizo zinatarajiwa kuanza kwa maeneo mengi katika wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2021 na kuisha katikati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2022. Hata hivyo, ongezeko kidogo la mvua linatarajiwa mwezi Machi, 2022 katika nusu ya pili ya msimu huo. 

Aidha, Dkt. Kijazi alisisitiza kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa mirejesho ya mwelekeo wa mvua nchini kadri inavyohitajika na kuwashauri wadau kuendelea kuwasiliana na Mamlaka ili kupata taarifa mahsusi za utabiri wa msimu ili kukidhi mahitaji maalum katika sekta zao.

Kwa maelezo kamili kuhusu utabiri huu tembelea: https://www.meteo.go.tz/




No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...