Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akiwasilisha mapendekezo ya Kikosi kazi cha WMO cha kufanya mapitio ya muundo na utendaji kazi wa kanda za WMO (Executive Council Task Force on the Comprehensive Review of the WMO Regional Concept and Approaches) kuhusiana na maboresho ya kimuundo na utendaji kazi wa kanda za WMO, Dkt. Kijazi aliwasilisha mapendekezo hayo katika mkutano mkuu maalumu wa Kidunia wa hali ya hewa “Extra-ordinary session of the World Meteorological Congress (Cg-Ext (2021), tarehe 11 Oktoba, 2021. Kulia kwake ni Meneja wa Ushirikiano wa masuala ya hali ya hewa Kikanda na Kimataifa na Mshauri wa Makamu wa Tatu wa Rais, Bw. Wilbert Muruke akifuatilia mkutano na kumsaidia Dkt. Kijazi.
Washiriki wa TMA katika Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Utendaji la WMO “Seventy- Second Session of the WMO Executive Council (EC-74) wakifuatilia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 25 hadi 29 Oktoba, 2021, wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO, Dkt. Agnes Kijazi. Mkutano wa EC-74 ulifanyika kwa lengo la kujadili utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu maalumu wa Kidunia wa hali ya hewa “Extra-ordinary session of the World Meteorological Congress (Cg-Ext (2021). Aliyeko kwenye runinga ni Rais wa WMO, Prof. Gerhard Adrian akiongoza mkutano wa EC-74.
Dar es Salaam; Tarehe 22/10/2021
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano mkuu maalumu wa Kidunia wa hali ya hewa “Extra-ordinary session of the World Meteorological Congress (Cg-Ext (2021), uliofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 11 hadi 22 Oktoba, 2021.
Lengo la mkutano huo lilikuwa ni kujadili utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu wa 18 wa Kidunia wa hali ya hewa “Eighteenth Session of the World Meteorological Congress (Cg-18)” uliofanyika mwaka 2019, pamoja na mapendekezo mapya ya kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa ili ziweze kuleta tija zaidi kwa jamii. Mkutano mkuu huo maalumu ulijielekeza zaidi katika maeneo makuu matatu, ambayo ni:
· Tathmini ya utekelezaji wa mabadiliko ya muundo wa WMO “(WMO reform)”;
· Mchango wa WMO katika maendeleo ya sekta ya maji (WMO support to the global water agenda); na
· Maboresho ya sera ya WMO ya ubadilishanaji wa data za hali ya hewa (WMO Unified Policy on International Data Exchange).
Mkutano huo ulipokea na kujadili taarifa na mapendekezo ya kamati na vikosikazi mbalimbali vya WMO vinavyoshughulikia maeneo hayo.
Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya Kikosi kazi cha WMO kilichopewa jukumu la kufanya mapitio ya muundo na utendaji kazi wa kanda za WMO (Executive Council Task Force on the Comprehensive Review of the WMO Regional Concept and Approaches). Dkt. Kijazi ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kikosikazi, aliwasilisha maapendekezo ya Kikosikazi hicho kuhusiana na maboresho ya kimuundo na utendaji kazi wa kanda za WMO, ili ziweze kushiriki ipasavyo katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa WMO zilizomo katika kanda husika. Mkutano ulipitisha mapendekezo yaliyowasilishwa na kumwomba Katibu Mkuu wa WMO kusimamia utekelezaji wa maamuzi hayo.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano mkuu huo maalumu wa Kidunia wa hali ya hewa ulijumuisha washiriki kutoka TMA, Wizara ya Maji, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, na mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Geneva – Uswisi.
Mkutano mkuu huo maalumu ulifuatiwa na Mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Utendaji la WMO “Seventy- Second Session of the WMO Executive Council (EC-74) uliofanyika pia kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 25 hadi 29 Oktoba, 2021 kwa lengo la kujadili utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu maalumu wa Kidunia wa hali ya hewa.Mikutano yote miwili iliongozwa na Rais wa WMO, Prof. Gerhard Adrian, ambaye ni raia wa Ujerumani.
No comments:
Post a Comment