Friday, February 28, 2020

TANZANIA YAISHUKURU JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI KWA USHIRIKIANO WALIOTOA KUMUUNGA MKONO MKURUGENZI MKUU WA TMA KATIKA KINYANG’ANYIRO CHA NAFASI YA MAKAMU WA TATU WA RAIS WA WMO.



Kigali, Rwanda; Tarehe 08 Februari, 2020;
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi amewashukuru wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa katika Jumuia ya Afrika Mashariki kwa ushirikiano mkubwa waliompatia katika kuwania nafasi ya Makamu Watatu wa Rais wa WMO
 
“Naomba ushirikiano huu (teamwork) tulio uonyesha katika kipindi cha uchaguzi uendelee pia katika utekelezaji wa majukumu ya Kikanda kwenye uboreshaji na utoaji huduma za hali ya hewa”. Alizungumza Dkt. Kijazi wakati akitoa shukrani hizo kwa niaba ya nchi katika Mkutano wa Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika Mashariki (Heads of EAC Meteorological Service Meeting), uliofanyika tarehe 7 hadi 8 Februari, 2020, Kigali, Rwanda.
 
Dkt. Kijazi  alisisitiza umuhimu wa kufanya vikao  kazi vya pamoja ili kuhakikisha masuala muhimu yanayohusiana na utoaji huduma ikiwa ni pamoja na kubadilishana taarifa za hali ya hewa yanapewa kipaombele.
 
“Kwa kutambua kuwa hali ya hewa haina mipaka ya nchi, hivyo ni wakati muafaka kwa Taasisi zetu kuwa na vikao vya kujadili masuala mbalimbali ya kuboresha huduma, tukichukua mfano wa hali ya hatari iliyopo kwa sasa ya uvamizi wa nzige na mlipuko wa virusi vya corona ambapo kwa kiasi kikubwa hali hizo zinauhusiano na hali ya hewa”. Alisisitiza Dkt. Kijazi.
 
Masuala muhimu yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na nchi wanachama wa EAC kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za hali ya hewa kwa viwango vya kimataifa ikiwa pamoja na kupata cheti cha ubora cha utoaji wa huduma za hali ya hewa yaani ISO 9001:2015 (Tanzania kupitia TMA imeshapata cheti hicho cha ubora cha utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga). Vile vile nchi wanachama wa EAC kuongeza kasi katika upanuaji wa mtandao wa vituo vya upimaji wa hali ya hewa na mawasiliano ya data hizo na ubadilishanaji wa ujuzi kuhusu matumizi ya teknolojia mpya za upimaji wa hali ya hewa katika eneo la Jumuia ya Afrika Mashariki.

Aidha, suala la uchangiaji wa huduma za hali ya hewa kwa sekta zinazotumia huduma za hali ya hewa kibiashara (cost recovery) lilipewa kipaombele pamoja na taasisi za hali ya hewa kuendelea kuhifadhi data za hali ya hewa kwa kutumia kanzi data ambazo ni imara kutokana na uhitaji wa matumizi ya data hizi katika maendeleo endelevu ya nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki.

Kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababisha mabadiliko makubwa katika mifumo ya hali ya hewa mkutano huo umefikia makubaliano kwamba nchi wanachama waendelee kufanya tafiti na kushiriki katika mijadala ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya nchi hizo.  Tanzania imeng’ara katika mkutano huo kwa kuonekana kwamba imetekeleza makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano wa awali kwa kiwango cha kuridhisha na hiyo imepelekea TMA kupewa jukumu la kuzisaidia taasis zingine za Hali ya Hewa katika Jumuia ya Afrika Mashariki zenye changamoto katika utoaji wa huduma ikiwemo Burundi na Sudan ya kusini.

Thursday, February 13, 2020

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi, mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za msimu wa Masika (Machi – Mei 2020) katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza – Dar es Salaam, Tanzania.

Mtaalamu wa hali ya hewa kutoka TMA, Bi. Rosemary Senyagwa akitoa tathmini ya mvua za msimu wa Vuli (Novemba 2019 hadi Aprili 2020), kabla ya kutolewa rasmi mwelekeo wa msimu wa mvua za MASIKA kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2020

Mwandishi wa Habari kutoka Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle (DW) Bi. Hawa Bihoga akiuliza swali katika mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika (Machi – Mei 2020) katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza – Dar es Salaam, Tanzania.



Vyombo mbalimbali vya habari vikichukua taarifa wakati wa mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika (Machi – Mei 2020) katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza – Dar es Salaam, Tanzania.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Masika kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni  Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara  pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. 
 
Mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2020 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani katika maeneo ya mkoa wa Tanga, visiwa vya Unguja na Pemba, maeneo mengi ya mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, mashariki mwa mkoa wa Geita pamoja na mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara”. Alisema Dkt. Kijazi

Aliendelea kwa kuyataja maeneo ya mkoa wa Kagera, magharibi mwa mkoa wa Geita, kaskazini mwa mkoa wa Kigoma, Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro kuwa yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani. Aidha, Dkt. Kijazi alifafanua kuhusu mvua za nje ya msimu zinazoendelea katika maeneo yanayopata mvua za Masika hususan maeneo yaliyopo katika pwani ya kaskazini, mvua hizo zinatarajiwa kuendelea na kuungana na msimu wa mvua wa Masika 2020.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hata katika maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani, hivyo jamii inashauriwa kuchukua hatua stahiki kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...