Siku ya Ijumaa usiku wa tarehe 27 Julai, 2018, tukio la
kupatwa kwa mwezi linatarajiwa ambapo nuru ya mwezi mkamilifu (full moon) itazuiwa
na Dunia hivyo mwezi kuonekana kuwa na rangi nyekundu katika kipindi cha saa
kadhaa kuanzia saa 4:30 usiku hadi saa 6:14 usiku. Tukio la kupatwa kwa mwezi linatarajiwa
kuonekana vizuri katika maeneo mengi ya bara la Afrika, Asia na Ulaya. Hapa nchini Tanzania tukio hilo linatarajiwa kuonekana katika maeneo mengi na linatarajiwa
kudumu kwa takribani masaa mawili.
Kupatwa kwa Mwezi hutokea wakati Dunia, Mwezi na Jua vinapokuwa
kwenye mstari mmoja. Hali
hiyo inapotokea mwanga wa jua unaofika katika uso wa mwezi huzuiwa na duara la
Dunia. Katika mpangilio huo nuru ya Mwezi huonekana kuwa na giza (Total Lunar
Eclipse). Hiyo ndio hali inayotarajiwa kujitokeza katika maeneo ya bara la Afrika,
Asia na Ulaya usiku wa tarehe 27 Julai 2018.
Kupatwa kwa Mwezi husababisha mabadiliko katika nuru ya
mwezi na hivyo kufanya nuru ya mwezi kuwa hafifu(Partial Lunar Eclipse) au kuwa
giza (Total Lunar Eclipse). Kwa kuwa kupatwa kwa mwezi kutatokea kipindi Mwezi ukiwa
mbali zaidi na Dunia, inatarajiwa kuwa tukio hili litaonekana kwa muda mrefu
zaidi ukilinganisha na matukio mengine katika karne ya 21.
Mabadiliko
katika hali ya hewa;
Kwa vile katika tukio hili mabadiliko katika nguvu za
uvutano kati ya Dunia na Mwezi yatakuwa ni madogo kutokana na umbali mkubwa kati ya Mwezi na
Dunia hali ya Bahari Kujaa (High tide) na Bahari Kupwa (Low Tide) haitarajiwi
kuwa na mabadiliko makubwa, na pia hakuna mabadiliko makubwa
yanayotarajiwa katika mifumo ya hali ya
hewa.
Mamlaka ya Hali
ya Hewa inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa na itatoa taarifa za ziada
za hali ya hewa kila itakapobidi.
No comments:
Post a Comment