Katibu tawala wa Wilaya ya Nyamagana Bibi Mayala amewataka
wanahabari kutumia fursa ya mafunzo ya El Nino na athari zake katika msimu wa
VULI katika kuboresha elimu kwa jamii kuhusu athari za El Nino nchini. Bibi
Mayala aliyasema hayo wakati akifungua warsha ya wanahabari iliyofanyika Jijini
Mwanza, tarehe 02 Februari 2016. Aidha, aliwapongeza TMA kwa jitihada zao kubwa
za kuelimisha wanahabari kwa kuwa vyombo vya habari ni sekta muhimu katika
kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa wananchi.
Katika warsha hiyo Dkt. Kijazi ambaye ni
Mkurugenzi Mkuu wa TMA alisema warsha
hiyo ni muhimu kwani itawawezesha wana habari kuwa na uelewa mkubwa wa taarifa
za hali ya hewa na hivyo kuzisamabaza kwa usahihi zaidi. Aidha aliwashukuru
wana habari kwa kuhuduria warsha hiyo na ushirikiano wanaoutoa katika kuhakikisha
kwamba taarifa zinazotolewa na TMA zinawafikia wadau kwa wakati. Dkt. Kijazi aliwashukuru wafadhili wa warsha
hiyo ambao ni Serikali ya Norway kupitia Shirika la Hali ya Hewa ulimwenguni.
Kwa upande wa wanahabari, Bi. Theopista Nsanzugwanko kutoka gazeti la
Habari Leo alisema semina hii itasaidia waandishi wa habari kuweza kujifunza
masuala mbalimbali kuhusu mifumo ya hali ya hewa na kuwezesha kuandika habari kwa usahihi na kusaidia jamii kutumia
vema taarifa za hali ya hewa. Pia itawezesha jamii kupata elimu ya kukabiliana
na madhara ya mvua za El Nino ili kupunguza madhara kwa jamii ikiwa ni pamoja
na kutoa taarifa za tahadhari kwa usahihi zaidi.
TMA imekuwa ikiandaa warsha mbalimbali kwa wadau
mbalimbali wakiwemo wanahabari katika mwendelezo wa utoaji elimu ya sayansi ya
hali ya hewa pamoja na kudumisha ushirikiano baina ya Mamlaka na watumiaji wa
taarifa za hali ya hewa ambao ni wadau kutoka sekta mbalimbali. Warsha hiyo
imejumuisha wanahabari kutoka vyombo mbali mbali vya habari hapa nchini ambao
wako Dar es Salaam na Mwanza.
IMETOLEWA NA MONICA MUTONI;
AFISA UHUSIANO, MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment