Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mheshimiwa Dkt. Charles Tizeba, amewapongeza wataalamu wa hali ya hewa kutoka Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuboresha taarifa za hali ya hewa. Mhe. Dkt. Tizeba alisema hayo wakati akifungua rasmi mkutano wa Arobaini na Moja wa Jukwaa la Wataalam wa Hali ya Hewa kutoka nchi za Pembe ya Afrika (Greater Horn of Africa Climate Outlook Forum – GHACOF-41) uliofanyika Dar es Salaam, Tanzania katika hoteli ya Kunduchi tarehe 24 - 25 Agosti 2015.
“Tunathamini na kutambua mchango unaotolewa na Jukwaa
la Kikanda la Hali ya Hewa katika
kuboresha na kujengea uwezo wa taasisi za hali ya hewa, wadau na watumiaji
wa taaarifa za hali ya hewa ili kuongeza ubora na matumizi sahihi ya taaarifa
hizo katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii” alisema
Dkt.Tizeba.
Aidha,
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) Dkt. Agnes Kijazi alitoa
shukrani zake za dhati kwa Tanzania kupewa jukumu la kuwa mwenyeji wa mkutano
huo. “Napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Kituo cha kutoa
taarifa za Hali ya Hewa katika Ukanda wa Pembe ya Afrika pamoja na Afrika
Mashariki (IGAD Climate prediction and Application Center (ICPAC)) kwa
kushirikiana na Taasisi zinazosimamia huduma za Hali ya Hewa katika ukanda huu,
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na wadau wengine wa maendeleo kwa kuandaa
Mkutano huu muhimu katika hoteli ya Kunduchi Beach, Dar es Salaam, ni heshima
kubwa sana kwetu”. alisema Dkt. Kijazi.
Mkutano huu
wa majadiliano uliwaleta pamoja watumiaji na wataalamu wa huduma za hali ya
hewa katika sekta muhimu za kiuchumi na kijamii kutoka kwenye taasisi za
serikali na zisizo za kiserikali, watoa maamuzi, wanasayansi na wadau kutoka Asasi
za Kiraia. Mkutano ulifanya mapitio ya viashiria vinavyotarajiwa kuathiri
mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa katika kipindi cha msimu wa mvua kwa mwezi
Septemba hadi Disemba, 2015. Aidha, ilibainishwa kuwa kuwepo kwa El Nino ni
miongoni mwa viashiria vinavyotarajiwa kuchangia kwa kiasi kikubwa hali ya mvua
katika msimu huu. Maeneo mengi ya ukanda wa Pembe ya Afrika na Afrika Mashariki
yanatarajiwa kuwa na mvua nyingi isipokuwa kwa baadhi ya maeneo machache.
Watumiaji
na wadau waliohudhuria mkutano huo kutoka katika sekta za Kilimo na Usalama wa Chakula,
Afya, Habari, Taasisi za Uratibu wa Maafa, Maji pamoja na wadau wa maendeleo
walijadli na kuweka mikakati mbalimbali ya kutumia taarifa ya utabiri wa hali ya hewa iliyotolewa na
kupunguza athari mbaya zinazoweza kujitokeza katika sekta zao.
Mkutano huu umedhaminiwa na kuandaliwa
na Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP), Taasisi ya matumizi ya huduma za hali
ya hewa (ICPAC) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) akiwa mwenyeji wa
mkutano huo.
IMETOLEWA NA: MONICA
MUTONI
AFISA
UHUSIANO,
MAMLKA YA HALI
YA HEWA TANZANIA
No comments:
Post a Comment