Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa Tanzania Dkt. Agnes Kijazi anasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa
Mkurugenzi Mkuu mstaafu Dkt. Mohamed Mhita aliyezaliwa tarehe 17 Februari 1946 na
kufariki siku ya Jumatatu tarehe 06 Aprili
2015 katika hospitali ya Agakhan jijini Dar
es Salaam.
Dkt. Mhita alikuwa Mkurugenzi Mkuu
wa iliyokuwa Idara Kuu ya Hali ya Hewa kwa kipindi cha miaka 8 kuanzia 1992
hadi 1999 na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kipindi
cha miaka 9 kuanzia 1999 hadi 2008. Dr. Mhita kwa kushirikiana na uongozi wa
iliyokuwa idara Kuu ya Hali ya Hewa alishiriki katika kuishauri Serikali kuhusu
kuanzishwa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kutoka iliyokuwa Idara Kuu ya
Hali ya Hewa.
Pamoja na nafasi ya Mkurugenzi
Mkuu pia alikuwa Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya
Hewa Duniani kuanzia mwaka 1992 hadi 2008. Alichaguliwa kuwa Mjumbe katika Baraza
Kuu la Shirika la Hali ya Hewa Dunia kuanzia mwaka 1995 hadi 2007. Alichaguliwa
kushika nafasi ya Rais wa Jumuiya ya
Hali ya Hewa katika Bara la Afrika (RA 1) kuanzia mwaka 1998 hadi 2007. Dkt Mhita
alikuwa Rais wa ‘Tanzania Meteorological Society’ sambamba na nafasi nyingine
nyingi mbalimbali alizoshika ndani na nje ya nchi.
Akielezea baadhi ya mambo makubwa
yatakayomfanya Dkt. Mhita aendelee kukumbukwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa nchini Dkt. Agnes Kijazi alisema ‘Dkt. Mhita atakumbukwa kwa
mchango wake mkubwa katika kuendeleza sayansi ya hali ya hewa hapa nchini, katika
Bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hususani katika ushiriki wake wa
kuianzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini kwa kuandaa dira (vision) na dhamira (mission)
ya Mamlaka kwa kipindi cha miaka kumi na tano (15) kuanzia mwaka 2000 hadi 2015’.
Dkt. Mohamed Mhita ni mmoja kati ya
wanasayansi waliokuwa zao la chuo kikuu cha Stolkholm, Sweden ambako alitunukiwa
shahada ya hali ya hewa (BSc. Met) mwaka 1977.
Kuanzia mwaka 1981 hadi 1984 alikuwa mafunzoni katika chuo Kikuu cha Reading, Uingereza ambako
alitunikiwa shahada ya uzamivu (PhD). Hapa nchini alipata mafunzo ya Sekondari
katika shule za Tanga na Kamrimjee zote zikiwa mkoani Tanga.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania
inajumuika na familia, ndugu, jamaa na marafiki katika kuomboleza msiba huu.
Bwana Alitoa na Bwana Ametwaa Jina lake lihimidiwe.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI AFISA MAHUSIANO MAMLAKA
YA HALI YA HEWA TANZANIA.
Hakika sisi sote ni wa Mwenyezi Mungu, na Hakika kwake ndio marejeo yetu. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi..Amin
ReplyDelete