Tuesday, August 30, 2022

WILAYA 86 NCHINI KUNUFAIKA NA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2022.











Dar es Salaam; Tarehe 30 Agosti, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema imeendelea kuongeza wigo wa utoaji taarifa za hali ya hewa kwa maeneo madogo madogo, ambapo msimu wa Vuli 2022 utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita zilizo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa ziwa Viktoria. Hayo yalizungumzwa na Mwenyekeiti wa Bodi ya TMA Dkt. Buruhani Nyenzi wakati akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Utabiri wa Mvua za Vuli 2022 katika Ukumbi wa Chuo cha Usafirishaji (NIT), Dar es Salaam, Tarehe 30/08/2022.

 

Utabiri huu wa msimu wa Vuli utaambatana na tabiri za wilaya zote themanini na sita (86) zilizomo kwenye kanda za nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya kaskazini na ukanda wa Ziwa Viktoria. Hivyo, mimi binafsi napenda kutoa pongezi nyingi sana kwa hatua hii kubwa ya kuongeza wigo wa utoaji wa utabiri wa hali ya hewa hususan kwa watumiaji wa taarifa za hali ya hewa wa sekta na maeneo mbalimbali ambao wamekuwa na uhitaji wa taarifa hizi kwenye maeneo yao”. Alisema Dkt. Nyenzi.

 

Aidha, Dkt Nyenzi alisisitiza ushirikiano katika kuhakikisha kwamba taarifa hizo zinawafikia watumiaji wa mwisho kwenye sekta mbalimbali ili kuweza kuchangia katika ukuaji wa uchumi na kuleta tija pamoja na kufuatilia kwa karibu, kuelewa, kupanga na kukabiliana na hali ya hewa inayotarajiwa katika sekta zao.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani, Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa kauli mbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Matumizi Sahihi ya Taarifa za Hali ya Hewa kwa Maendeleo Endelevu” hivyo, katika kuendana na kaulimbiu hiyo, TMA imeendelea kuboresha taarifa zake kwa kutoa utabiri mahususi kwa sekta mbalimbali na kuongeza thamani katika taarifa zake za utabiri wa msimu kwa kujumuisha taarifa za maeneo madogo madogo kwa ngazi ya wilaya.

“Wakati Serikali ya awamu ya sita ikiendelea na jitihada za kukuza uchumi wa nchi pamoja na kuboresha miundombinu na huduma mbalimbali za kijamii ikiwemo huduma za hali ya hewa, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kuweka msisitizo wa matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa kila sekta ili kuongeza tija katika uzalishaji”.Alizungumza Dkt. Kijazi.

Kwa upande wa mdau kutoka Wizara ya Kilimo, akizungumzia utabiri wa msimu uliopitaBw. Juma Makandi alisema mara baada ya kupata taarifa za utabiri wa msimu wa mvua za Masika za awali na zilizohuishwa, wizara iliaandaa tafsiri ya utabiri huo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na kuwasilisha kwa wadau mbalimbali kwa utekelezaji wake.

Katika Mkutano huo, wadau walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2022 na kuweza kutoa ushauri utaowezesha kuandaa mbinu na mipango ya kukabiliana na athari (hasi au chanya) za utabiri huo. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 1 Septemba 2022.


 

Tuesday, August 9, 2022

TMA YATAKIWA KUONGEZA WIGO WA KUTOA ELIMU KWA JAMII KUHUSU TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe.Suleiman Masoud Makame akizungumza alipotembelea banda la TMA, Tarehe 08 Agosti, 2022 kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Kizimbani, Mjini Unguja kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti, 2022.

  


Mwakilishi wa Jimbo la Mtambile Pemba Seif Salim Seif   alipotembelea banda la TMA, Tarehe 08 Agosti, 2022 kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Kizimbani, Mjini Unguja kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti, 2022. 
                            







Wageni mbalimbali wakiendelea kupata elimu ya hali ya hewa walipotembelea banda la TMA  kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Kizimbani, Mjini Unguja kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti, 2022.
                                        
Wafanyakazi wa TMA wakiwa katika picha ya pamoja na Kaimu Mkurugenzi wa TMA ofisi ya Zanzibar kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Kizimbani, Mjini Unguja kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti, 2022.
  

Zanzibar; Tarehe 08 Agosti, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imeombwa kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu taarifa za hali ya hewa kwa makundi mbali mbali hususani wadau ambao wanahusika moja kwa moja ili waweze kusikiliza na kutekezeleza taarifa  zinazotolewa na Mamlaka. Hayo yalizungumzwa na Waziri wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe.Suleiman Masoud Makame alipotembelea banda la TMA, Tarehe 08 Agosti, 2022 kwenye maonesho ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Kizimbani, Mjini Unguja kuanzia tarehe 6 hadi 15 Agosti, 2022. 

“Mamlaka inatakiwa kuongeza wigo wa kutoa elimu kwa jamii kuhusu taarifa za hali ya hewa kwani tunawatu wasiopungua elfu 37000 wanaokwenda baharini kwa shughuli mbalimbali kila siku hivyo inatupasa tubadilike kidogo kwenye kutoa elimu tutumie wataalamu,wasanii,mikutano mbalimbali,kuwajuza watu kuhusu taarifa za hali ya hewa”. Alisema Mhe. Makame

Wakati akielezea hayo Waziri Makame aliongezea kuwa wananchi pia wanapaswa kuwa tayari kusikiliza taarifa za hali ya hewa na kuzifanyia kazi kwa usalama wao na mali zao kwani majanga mbali mbali yanatokea mara kwa mara, hivyo bila kufuatilia taarifa hizi majanga yanaweza kuongezeka na Serikali pia ipo tayari kuwahimiza wananchi na wadau husika  kutumia taarifa za hali ya hewa ili kupunguza majanga hayo. 

Nao wageni waliotembelea katika Banda la Mamlaka waliiomba TMA kuongeza njia za kuwafikia wakulima wa hali ya chini kabisa ambao hawana uwezo wa kupata taarifa hizi kwa njia zinazotumika ambazo ni televisheni, radio na mitandao ya kijamii, hivyo njia ya kupatata taarifa kupitia meseji za kawaida za simu za mkononi iboreshwe kwaajili ya  kurahisisha upatikanaji wa taarifa hizo.

“Hapo mwanzo tulikuwa tukipata taarifa za hali ya hewa kilimo mara nyingi kupitia meseji kwenye simu bure kabisa sasa hivi hatupati taarifa zile na zile tunazozipata baada ya taarifa ya habari hazilingani na zile za meseji hivyo tunaomba mturahisishie taarifa hizi ilitupate taarifa kwa urahisi”. Alisema Bwana Abdu Abdalla ambae ni mkulima kutoka Zanzibar.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Ofisi ya Mamalaka ya hali ya hewa Zanzibar Bw. Masoud M. Faki alieleza kuwa pamoja na kuwepo njia mbali mbali zinazotumiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania katika kusambaza taarifa za hali ya hewa inawapasa wananchi pia kufatilia taarifa za hali ya hewa ili waweze kuepukana na majanga na usumbufu unaoweza kujitokeza hasa kipindi hiki tunapoelekea siku ya SENSA ya watu na makazi.

 

 

Friday, August 5, 2022

TMA YAHIMIZWA KUONGEZA JITIHADA ZA KUIFIKISHIA JAMII TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA WAKATI

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema akizungumza mara baada ya kupata elimu ya hali ya hewa alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.

 


Ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo akitoa elimu ya hali ya hewa kwa Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema akisaini katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.

Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo akisaini katika kitabu cha wageni alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.



Wageni mbalimbali wakipokea zawadi kutoka kwa ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo, walipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.

Ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo akizungumza na wananchi wa Mbeya kupitia vyombo mbalimbali vya habari katika banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.




Wageni mbalimbali wakiendelea kupata elimu ya hali ya hewa walipotembelea banda la TMA kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.


Mbeya; Tarehe 05 Agosti, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imehimizwa kuongeza jitihada za kuifikishia jamii  taarifa za hali ya hewa kwa wakati, hayo yalizungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Pololet Kamando Mgema akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Mhe. Kanali Laban Elias Thomas alipotembelea banda la TMA, tarehe 5 Agosti 2022 kupitia maonesho ya NaneNane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya John Mwakangale, Uyole - Mbeya kuanzia tarehe 1 hadi 8 Agosti, 2022.

“Kazi yenu inajitangaza kwa kuwa mmekuwa mnafanya vizuri katika utabiri wenu wa msimu hivyo nawapongeza sana, lakini niwahimize kuongeza jitihada za kuwafikishia jamii taarifa hizo za hali ya hewa kwa wakati ziweze kutumika na kuwasaidia kwa wakati. Alisisitiza Mhe. Pololet Mgema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Aziza Mangosongo akiongozana na Mhe. Pololet Mgema aliongezea kwa kuipongeza TMA kwa utabiri mzuri wanaoutoa na kufanya wananchi kuwa na imani na taarifa za hali ya hewa kwa kuzitumia katika shughuli zao za kiuchumi na kijamii.

Aidha, akielezea namna TMA ilivyoboresha utabiri wa hali ya hewa katika ngazi ya wilaya kupitia vyombo vya habari, Ndg. Isack Yonah, Meneja wa Huduma za Hali ya Hewa Kilimo alisema, Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Namba 2 ya mwaka 2019 imeipa Mamlaka jukumu la kutoa huduma, kudhibiti na kuratibu shughuli za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na tayari imeshaboresha vifaa na mitambo ya hali ya hewa inayotumia teknolojia ya kisasa inayosaidia upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi zinazokusanywa katika vituo vya hali ya hewa ikiwemo kituo cha hali ya hewa kinachojiendesha chenyewe (Automatic Weather Station-AWS) ambacho kimeletwa kwenye maonesho hayo.

Ndg. Isack Yonah aliongezea kuwa katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa, TMA inatoa utabiri wa hali ya hewa hadi ngazi ya wilaya na hata kama ikitokea mkulima au mdau yeyote atahitaji kujua hali ya hewa ya eneo lake anaweza kuandaliwa taarifa mahususi kulingana na mahitaji yake kwa kuchangia huduma hiyo ili kufanya huduma hizo ziendelee kuwa endelevu. 


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...