Friday, February 18, 2022

WAZIRI JAFO AAGIZA TATHMINI ZA ATHARI KWA MAZINGIRA KUZINGATIA SHERIA NA TAKWIMU ZA HALI YA HEWA.

 







Dar es Salaam; Tarehe 18 Februari, 2022;

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo  amewaagiza wadau wa mazingira kuzingatia takwimu za hali ya hewa katika kuandaa tathmini za athari kwa mazingira nchini ili kutekeleza matakwa ya sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mhe. Jafo alitoa maelekezo hayo wakati akifungua rasmi warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa, iliyofanyika katika Ukumbi wa Maktaba, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tarehe 18/02/2022.

“Nikiwa waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) nitahakikisha kabla ya kutoa vyeti tathmini za athari kwa mazingira (EIA), jambo kubwa nitakaloliangalia ni chanzo cha takwimu zilizoambatishwa, hivyo hakuna namna ya kukwepa, tutumie takwimu sahihi za hali ya hewa kwa mustakhabali wa nchi yetu”. Alisema Mhe.Jafo.

“Kila mradi unaotaka kuwekezwa unatakiwa kufanyiwa tathimini za athari za mazingira (EIA), na mchakato wa EIA ni lazima unahitaji takwimu za hali ya hewa, na ikitokea umekosea takwimu utaleta shida”. Alieleza Mhe. Jafo.

Aidha, Mhe. Jafo alieleza kuwa sheria Na.2 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaipa Mamlaka ya Hali ya Hewa jukumu la kutoa takwimu za hali ya hewa na kuzitaka wizara,taasisi na wataalam elekezi wa mazingira (consultants) kuzingatia umuhimu wa matumizi ya takwimu za hali ya hewa na endapo takwimu hizo zitakosekana inatakiwa kupata ushauri wa kitaalamu kutoka TMA na kutokufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi.

Awali, Mhe Jafo alisema warsha hiyo imetokana na mchakato wa kisheria ambapo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania mwaka 2019 na kanuni zake kusainiwa mwaka 2021, hivyo kupelekea taasisi tatu ambazo ni Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Chama cha Wataalam wa Mazingira Tanzania (TEEA) kuona umuhimu wa kubadilishana mawazo ya namna ya kutekeleza sheria hiyo. Vilevile, Mhe Jafo aliwataka TMA kuandaa semina kwa maafisa mazingira waliopo katika halmashauri na mikoa yote nchini ili wafahamu vyema masuala muhimu ya hali ya hewa kama ilivyoainishwa katika sheria. Pia aliwataka (TMA) na kutoa mada kwenye vikao vya wakurugenzi wa jiji na halmashauri, ili kuwajengea uelewa wa sheria hiyo Na. 2 ya mwaka 2019.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kuwa warsha hii ni fursa  muhimu ya kuboresha huduma katika sekta ya mazingira kwa kuzingatia matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA na matakwa ya kisheria pamoja na kuimarisha uelewa kuhusiana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi.Aidha,Dkt. Kijazi aliwajulisha washiriki wa warsha hiyo kwamba huduma za hali ya hewa zinazotolewa nchini zimeongezeka viwango vya usahihi hivyo zinafaa kutumika katika sekta zote za maendeleo.

Aidha, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Bi Lilian Lukambuzi alisema NEMC na TMA wameingia makubaliano yenye lengo la kufanya tafiti za pamoja kuhusu masuala ya ya hali ya hewa na mazingira  na kufuatilia miradi ya kimkakati ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu.

Naye, mwakilishi wa TEEA Bi. Rukia Ismail alifafanua kuwa warsha hiyo itawasaidia  katika kuimarisha ufanisi wa kuandaa thathmini za athari kwa mazingira na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wadau wa mazingira katika utekelezaji wa majukumu yao ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa takwimu za muda mrefu za hali ya hewa.

Warsha ya wadau wa mazingira kuhusu umuhimu wa huduma za hali ya hewa imeandaliwa kwa ushirikiano wa TMA, NEMC na TEEA ikiwa na lengo la kujenga uelewa kuhusu taarifa za hali ya hewa na umuhimu wa kuzingatia mipango ya utekelezaji wa mipango hiyo.

Thursday, February 17, 2022

TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2022 KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.


 Dar es Salaam 17 Februari, 2022.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2022 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza, tarehe 17/02/2022, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

 

Mvua za Masika kwa kipindi cha Machi hadi Mei, 2022 zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani, aidha mvua hizo zinatarajiwa kuanza mapema kati ya wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Februari2022 na kuisha mwezi Mei 20202 katika maeneo mapema”. Alisema Dkt. Kijazi

 

“Mikoa inayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma”. Aliendelea Dkt. Kijazi.

 

Vilevile, taarifa hiyo imeeleza pia ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2022 katika maeneo ya pwani ya kaskazini na mwezi  Aprili katika maeneo ya tya nyanda za juu kaskazini mashariki.

 

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa miundombinu, upotevu wa mali na maisha, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.

 

Ilikupata taarifa zaidi za utabiri tembelea https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

Tuesday, February 15, 2022

TMA YAWATAKA WANAHABARI KUENDELEA KUWA MABALOZI WA KUSISITIZA UMUHIMU WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.

Mgeni rasmi, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa wakati akifungua rasmi Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika (Machi hadi Mei, 2022)  kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022.

                              Matukio kwa picha wakati waandishi wakisikiliza mada mbalimbali zilizowasilishwa katika Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika 2022 katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022.
 

Waandishi kutoka vyombo mbalimbali katika picha ya pamoja na mgeni rasmi katika katika Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika 2022 katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022. Utabiri huo unatarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 17 Februari 2022 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza - Dar es Salaam, Tanzania.

 

Tanga; Tarehe 14 Februari, 2022;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imewataka wanahabari wote nchini kuendelea kuwa mabalozi wa kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa nchini. Hayo yalizungumzwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri Dkt. Hamza Kabelwa wakati akifungua rasmi Warsha ya Wanahabari kuhusu Utabiri wa Mvua za Masika 2022 kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi katika Ukumbi wa Bandari, Tanga, Tarehe 14/02/2022.

“Mamlaka inamchango mkubwa katika ukuaji wa kiuchumi kwa vile huduma za hali ya hewa ni mtambuka na zinahitajika katika kila sekta.Napenda kuwakumbusha kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa TMA na daraja kati ya TMA na jamii katika kuelezea na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zetu za kila siku”. Alisema Dkt. Kabelwa.

Aidha, Dkt. Kabelwa alivipongeza vyombo vya habari nchini kwa ushirikiano wake katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na wakati, na kukiri kuwa faida ya kuendelea kufanyika kwa warsha za wanahabari kabla ya kutoa utabiri wa msimu zimeendelea kuonekana.

“Kama mnavyofahamu, warsha hii ni muendelezo wa warsha nyingine nyingi ambazo zimekuwa zikifanyika ikiwa ni juhudi za Mamlaka kutaka kuhakikisha taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinawafikia walengwa kwa uhakika, usahihi na kwa wakati. Napenda kukiri kuwa faida za warsha hizi kwa sisi TMA tumeziona kwani mwamko wa jamii sasa hivi umekuwa mkubwa na hata taarifa zinazorushwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari  zimekuwa katika lugha rahisi na inayoeleweka kwa jamii, hivyo kwa hatua hii napenda kuwapongeza na muendelee kuongeza bidii ili kufikia malengo ya juu na kuwafikia watanzania wote kwa wakati”. Alieleza Dkt. Kabelwa.

Kwa upande wake mwandishi wa habari kutoka gazeti la Majira, Bi. Penina Malundo alisema kuwa warsha za mafunzo kutoka TMA zimeendelea kuwajengea uwezo hivyo kuwasaidia katika uandishi wa taarifa sahihi bila kupotosha umma na kuwezesha jamii na wadau kujipanga na kuandaa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo yao.

Katika warsha hiyo, wanahabari walipata fursa ya kuona rasimu ya utabiri wa hali ya hewa katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei 2022, ambao ni mahsusi kwa maeneo ya Nyanda za juu kaskazini mashariki (Mikoa ya Arusha,Kilimanjaro, Manyara), Pwani ya Kaskazini (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani ikijumuisha visiwa vya Mafia), Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Pemba na Unguja, Ukanda wa Ziwa Viktoria (Mikoa ya Kagera, Mwanza, Geita,Mara, Simiyu  na Shinyanga) pamoja na Kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za MASIKA 2022 kupitia vyombo vya habari, tarehe 17 Februari 2022.


 

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...