Thursday, September 23, 2021

MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA) YAPATA VIFAA VIPYA VYA KUPIMA HALI YA HEWA YA ANGA LA JUU (UPPER AIR)

Wataalamu wa hali ya hewa kituo cha TMA-JNIA, wakifuatilia mafunzo ya uendeshaji wa mtambo mpya waupimaji wa hali ya hewa ya anga la juu. Mafunzo yalitolewa na mkufunzi kutoka kampuni ya MODEM ya Nchini Ufaransa, Bw. Benjamin Finot, tarehe 8 Septemba, 2021.



 Wataalamu wa hali ya hewa wakiwa katika mafunzo kwa vitendo ya urushaji puto linalobeba kifaa cha radiosonde kinachopima haliya hewa ya anga la juu, baada ya kukamilika zoezi la kufungwa vifaa hivyo JNIA, tarehe 8 Septemba, 2021



Dar es Salaam; Tarehe 13/09/2021

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) limeipatia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)vifaa vipya vya kupima hali ya hewa ya anga la juu (upper air).Vifaa hivyo vimetolewa kwa TMA ikiwa ni msaada chini ya utekelezaji wa program ya WMO ya kuboresha huduma za hali ya hewa kwa Nchi Wanachama wa Afrika Mashariki (EAC) zinazozunguka eneo la Ziwa Viktoria, iitwayo “HIGH impact Weather lAke SYstems (HIGHWAY)”.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na: mtambo wa kuzalisha gesi ya haidrojeni (Hydrogen gas Generator); radiosonde; Maputo maalumu ya kupima hali ya hewa ya anga za juu (weather balloons);program za kompyuta (computer softwares)na mavazi maalumu kwa ajili ya usalama. Vifaa hivyo vimefungwa tarehe 7 Septemba, 2021 katika kituo cha kupima hali ya hewa ya anga la juu (Upper Air Station) kilichopo katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa MwalimuJulius Nyerere, Dar es Salaam (JNIA). Aidha, zoezi la ufungaji wa vifaa hivyo lilienda sambamba na mafunzo kwa wataalamu.

Ufungwaji wa vifaa hivyo umewezesha kuhuisha kituo hichokuwa cha kisasa zaidi baada ya mitambo ya awali kuwa chakavu. Kituo hicho kwa sasa kitaendelea na shughuli zake za kupima hali ya hewa ya anga la juu kama kawaida.Uhuishaji wakituo hicho utawezesha kupima takwimu za hali ya hewa ya anga la juu, ambazo ni muhimu sana katikakutoa utabiri wa hali ya hewa kwa matumizi mbalimbali hususan usalama na usafiri wa anga nchini. 

Programu hiyo ya HIGHWAY ilitekelezwa nchini Tanzania kwa kipindi cha miaka mitano, kuanzia Septemba, 2017, ambapo miongoni mwa shughuli zake zilihusisha pia uhuishaji wa kituo hicho cha kupima hali ya hewa ya anga la juu katika uwanja wa JNIA. Msaada wa vifaa vilivyotolewa na WMO  ni sehemu ya utaratibu wa Shirika hilo ikiwa ni mrejesho kwa Nchi Wanachama kutokana na michango inayotolewa na Serikali za Nchi Wanachama kupitia ada ya uanachama kwa Shirika hilo.

Thursday, September 16, 2021

ZIARA YA MHE. NAIBU WAZIRI KATIKA OFISI ZA TMA -MWANZA


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Mhe. Mwita Waitara (MB) akipata maelezo kuhusiana na utoaji huduma Bora za hali ya hewa kwa usafiri wa anga katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza. Tarehe 16/09/2021.




 

Tuesday, September 14, 2021

DKT. KIJAZI AELEZA FAIDA KWA NCHI WANACHAMA WA WMO KANDA YA AFRIKA

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akiwasilisha mada kuhusiana na faida za mabadiliko ya kimuundo na majukumu ya kanda za WMO kwa Nchi za kanda ya Afrika. Aliwasilisha mada hiyo tarehe 23 Agost, 2021 katika mkutano wa 18 wa Nchi Wanacahma wa WMO kanda ya Afrika awamu ya pili “Eighteenth Session of WMO Regional Association 1-phase II (RA I – 18(II))”. Kulia kwake ni Meneja wa Mashirikiano ya Hali ya Hewa Kikanda na Kimataifa, Bw. Wilbert Muruke akimsaidia Mkurugenzi Mkuu Dr. Kijazi

 

Mkurugenzi wa Huduma za utabiri katika TMA, Dkt. Hamza Kabelwa aliwasilisha mwongozo wa WMO wa uchakataji wa data na utabiri “Manual on the Global Data Processing and Forecasting System (GDPFS)”katika mkutano wa 18 wa Nchi Wanacahma wa WMO kanda ya Afrika awamu ya pili “Eighteenth Session of WMO Regional Association 1-phase II (RA I – 18(II))”,terehe 24 Agosti, 2021


Mkurugenzi wa Huduma za utabiri katika TMA, Dkt. Hamza Kabelwa aliwasilisha mwongozo wa WMO wa uchakataji wa data na utabiri “Manual on the Global Data Processing and Forecasting System (GDPFS)” katika mkutano wa 18 wa Nchi Wanacahma wa WMO kanda ya Afrika awamu ya pili “Eighteenth Session of WMO Regional Association 1-phase II (RA I – 18(II))”,terehe 24 Agosti, 2021.

 

Dar es Salaam; Tarehe 23/08/2021

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, ameeleza faida zitakazopatikana kwa  Nchi Wanachama wa WMO kanda ya Afrika“WMO Regional Association I – Africa (RA I)”kutokana na uboreshaji wa muundo na majukumu ya kanda za WMO unaotekelezwa na Shirika hilo. 

Dkt. Kijazi alieleza hayo tarehe 23 Agosti, 2021 katika mkutano wa 18 wa Nchi Wanachama wa WMO kanda ya Afrika awamu ya pili “Eighteenth Session of WMO Regional Association 1-phase II (RA I – 18(II))”,uliofanyika kwa njia ya mtandao kuanzia tarehe 23 hadi 26 Agosti, 2021. Dkt. Kijazi ambaye ni Mwenyekiti wa Kikosi kazi cha WMO cha kufanya mapitio ya muundo na majukumu ya kanda za WMO “(Executive Council Task Force to lead the Comprehensive Review of the WMO Regional Concept and Approaches)”, alieleza faida hizo alipowasilisha mada kuhusiana na namna Nchi Wanachama wa WMO kanda ya Afrika zitakavyofaidika na maboreho hayo, ambapo mada hiyo ililenga kutoa uelewa kuhusiana na manufaa ya maboresho hayo kwa kanda ya Afrika. 

Akiwasilisha mada hiyo, Dkt. Kijazi, alisema miongoni mwa faida zitakapatikana kwa Nchi za kanda ya Afrika ni pamoja na kuimarishwa kwa njia za kuibua na kushughulikia  vipaumbele vya kanda ya Afrika, ambapo vipaumbele hivyo vitaibuliwa kupitia mfumo maalumu wa WMO (WMO Community Platform). Aidha, maboresho hayo yanatoa fursa kwa viongozi na wataalamu katika kandakujielekeza zaidi katika kujadili na kutoa mapendekezo stahiki ya kutatua changamoto za Nchi Wanachama katika kanda husika. Maboresho hayo pia yataweka mfumo bora wa kuratibu utekelezaji wa maamuzi ya WMO, kwa kuweka utaratibu wa kupima utendaji kazi na utekelezaji wa maamuzi hayo.

Faida zingine ni kuimarika zaidi  kwa ushirikiano baina ya Taasisi za Hali ya Hewa, taasisi za maji, sekta binafsi,  taasisi za elimu ya juu na mashirika ya Umoja wa Mataifa; Kuimarika na kuongezeka kwa fursa za mashirikiano baina ya Nchi au maeneo yanayohusiana katika kanda; na uboreshwaji wa vituo vya huduma za hali ya hewa vya kikanda (Regional Specialized Meteorological Centres-RSMC) katika kuzijengea uwezo zaidi Nchi Wanachama katika Kanda. 

Faida hizo alizoeleza ni sehemu ya mapendekezo ya jopo analoliongoza yatakayowasilishwa na kutolewa maamuzi katika Mkutano Mkuu wa WMO “Extra-Ordinary Meteorological Congress (2021)”unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Mapendekezo hayo yanajumuisha pia majukumu ya Nchi Wanachama katika kanda husika, pamoja na majukumu ya viongozi waandamizi katika kanda. Maboresho hayo ya muundo na majukumu ya kanda za WMO ni mwendelezo wa mabadiliko ya kimfumo yanayotekelezwa na WMO ili kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa kwa Nchi Wanachama.

Sambamba na faida zilizoainishwa, mkutano huo pia ulijadili mada mbalimbali, ikiwa ni pamoja na masuala ya uboreshaji wa miundombinu ya hali ya hewa, utafiti na huduma za hali ya hewa barani Afrika. Katika eneo la miundombinu, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri wa TMA, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya WMO inayoshughulikia uchakataji wa data na utabiri wa hali ya hewa “Standing Committee on Data Processing for Applied Earth System Modeling and Prediction (SC-ESMP)”,Dkt. Hamza Kabelwa aliwasilisha mada kuhusu mwongozo wa WMO wa uchakataji wa data na utabiri “Manual on the Global Data Processing and Forecasting System (GDPFS)”. Aidha,Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi wa TMA, Dkt. Pascal Waniha alichangia katika mkutabno huo na kushauri Nchi za kanda ya Afrika kuuhuisha mpango wa kuwa na satelaiti ya hali ya hewa ya Afrika itakayosaidia kuboresha upatikanaji wa data za hali ya hewa na hatimaye kuboresha zaidi huduma za hali ya hewa barani Afrika.

 

Thursday, September 2, 2021

MVUA ZA VULI 2021 ZINATARAJIWA KUANZA KWA KUSUASUA.

Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri - TMA, Dkt. Hamza Kabelwa mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu wa Vuli Oktoba - Desemba 2021


Bw. Ramadhan Omary akitoa tathmini ya mvua za msimu wa Masika 2021, kabla ya kutolewa rasmi mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli kwa kipindi cha mwezi Oktoba hadi Desemba 2021.


Washiriki mbalimbali wakiwa kwenye mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Vuli Oktoba - Desemba 2021.

 

Dar es Salaam, 02/09/2021;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2021 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi wa Huduma za utabiri Dkn. Hamza Kabelwa alisema Utabiri huu ni mahsusi kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka (Nyanda za juu kaskazini mashariki, Pwani ya kaskazini, Ukanda wa Ziwa Viktoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma).

Dkt Kabelwa alisema, Msimu wa mvua za Vuli unatarajiwa kuanza kwa kusuasua katika wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Oktoba 2021 ukiwa na mtawanyiko na muendelezo usioridhisha katika maeneo mengi. Aidha, Mvua za Vuli zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zinatarajiwa kuambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi yanayopata mvua za Vuli.

Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kabelwa  alisema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hali ambayo inaweza kuleta uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, hivyo mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo kutokana na maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kabelwa

Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2021 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram. 

Kwa taarifa zaidi tembele: https://www.meteo.go.tz/news/mvua-za-vuli-2021-zinatarajiwa-kuanza-kwa-kusuasua

WANAHABARI WAHIMIZWA KUENDELEA KUWA MABALOZI WAZURI WA TMA.

Washiriki wa warsha ya wanahabari kuhusu msimu wa mvua za Vuli, mwezi Oktoba hadi Disemba 2021 katika picha ya pamoja


Kaimu Mkurugenzi Mkuu - TMA, Dkt. Ladislaus Chang'a, akifungua warsha ya wanahabari kujadili utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba - Disemba 2021)  unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 02 Septemba 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania  

Dkt. Hamza Kabelwa, Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri - TMA, akifafanua jambo katika warsha ya wanahabari kujadili utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba - Disemba 2021)  unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 02 Septemba 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania      

Mtaalam wa Hali ya Hewa kutoka TMA, Bi. Rose Senyagwa akitoa tathmini ya mvua za msimu wa Masika 2021, katika warsha ya wanahabari kujadili utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba - Disemba 2021) unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 02 Septemba 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania  









Wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakichangia mada katika warsha ya wanahabari kujadili utabiri wa msimu wa mvua za vuli (Oktoba - Disemba 2021) unaotarajiwa kutolewa rasmi Tarehe 02 Septemba 2021 katika ukumbi wa mikutano wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, Tanzania  


 Kibaha, 1/09/2021.

Ikiwaa ni muendelezo wa ushirikishwaji wa wanahabari katika kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinawafikia wananchi kwa wakati na kwa lugha inayoeleweka. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili muelekeo wa msimu wa mvua za VULI kwa mwaka 2021, kabla ya kutolewa rasmi kwa umma Tarehe 02 Septemba 2021.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Agnes Kijazi, wakati wa ufunguzi wa mkutano huo katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Uuguzi, Kibaha – Pwani, Dkt. Ladislaus Chang’a ambaye pia ni Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya taarifa za hali ya hewa wa TMA aliwahimiza waandishi wa habari kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa TMA kwa umma.

‘Nizidi kuwakumbusha kuwa mabalozi wazuri wa TMA kuelezea na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zote za kiuchumi na kimaendeleo. Aliyasema hayo Dr Ladislaus Chang'a. 

Dkt. Chang’a alisema kuwa upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa ni muhimu kwa sababu zina mchango mkubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, nishati, maji n.k. kwani miongoni mwa maeneo yanayopata mvua za vuli, kuna mikoa inayotegemewa katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa nchi na vyanzo vya maji na mabwawa kwa kuzalisha umeme.

Waandishi wa habari wakiwasilisha mada mbalimbali kupitia mkutano huo wameipongeza TMA kwa kuwaongezea uelewa juu ya maswala ya hali ya hewa na kuleta muhitikio kwa vijana kufuatilia taarifa za hali ya hewa.

Aidha, waandishi hao wameahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kwa TMA ikiwemo kufuatilia sekta mbali mbali ambazo zinatumia taarifa za hali ya hewa ili kujua namna walivyojipanga kutumia taarifa hizo zinazotarajiwa kutolewa rasmi na TMA ili kuepukana na athari zinazoweza kujitokeza kutokana na hali mbaya ya hewa.

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...