Wednesday, October 21, 2020

TMA IMETOA RASMI MWELEKEO WA HALI YA HEWA KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA ZA MSIMU MARA MOJA KWA MWAKA.

Dar es Salaam,Tarehe 21/10/2020: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka ikijumuisha mikoa iliyopo magharibi mwa nchi ( Kigoma, Tabora na Katavi), nyanda za juu kusini magharibi (Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa), katikati mwa nchi (Dodoma na Singida), pwani ya kusini (Lindi na Mtwara), mkoa wa Ruvuma pamoja na maeneo yaliyoko kusini mwa mkoa wa Morogoro na pia kuelezea athari zinazoweza kujitokeza. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi aliwataka wananchi wa maeneo hayo kuzitumia vizuri mvua hizo na kufuata ushauri kutoka kwa wataalamu wa sekta husika. ‘Naendelea kuwahimiza wananchi waishio katika mikoa husika kuhifadhi mazao baada ya kuvuna kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam ili kuepuka uharibifu unaoweza kujitokeza kutokana na hali ya mvua na unyevunyevu inayotarajiwa kwani maeneo mengi yanatarajiwa kuwa na mvua za wastani hadi juu ya wastani’ alisema Dkt. Kijazi. Kuhusu mvua za msimu wa Vuli kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ilielezwa kuwa zinatarajiwa kuendelea kama ilivyotabiriwa hapo awali ambapo maeneo mengi yalitarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani, japo alisisitiza kuwa mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari 2020. Aidha, kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara moja kwa mwaka utabiri ulionesha katika maeneo mengi ya mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Songwe, Ruvuma, Njombe, Iringa, Lindi, Mtwara, Kusini mwa mkoa wa Morogoro na mashariki mwa mikoa ya Tabora na Katavi inatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani huku mikoa ya Kigoma, Rukwa pamoja na Magharibi mwa mikoa ya Tabora na Katavi mvua zikitarajiwa kuwa za wastani hadi chini ya wastani. Dkt. Kijazi aliendelea kuelezea kuwa mvua hizo kwa maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka zinatarajiwa kuanzia mkoa wa Tabora katika wiki ya kwanza na ya pili ya mwezi Novemba, 2020 na baadae kutawanyika katika mikoa mingine ifikapo wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 na ikitarajiwa kuisha katika maeneo mengi ya nchi katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2021, japo kwa mkoa wa Ruvuma zikitarajiwa kuisha katikati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Aprili, 2021. Kwa taarifa zaidi tembelea:

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...