Tuesday, October 13, 2020

MWENENDO WA MVUA KWA UKANDA WA PWANI YA KASKAZINI

Dar es Salaam, 13 Oktoba 2020: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, inapenda kutoa ufafanuzi juu ya uwepo wa vipindi vya mvua zinazoendelea leo katika maeneo ya ukanda wa pwani ya Kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba). Mvua hizo zimetokana na uwepo wa mgandamizo mdogo wa hewa katika eneo la bahari ya Hindi uliosababisha kuvuma kwa upepo wenye unyevunyevu kutoka baharini kuelekea katika maeneo ya pwani ya nchi yetu. Hata hivyo, mvua hizi ni za muda mfupi na zinatarajiwa kupungua kwa siku ya kesho tarehe 14 Oktoba, 2020 na kuongezeka kidogo tarehe 15 Oktoba, 2020. Aidha, mvua za Vuli (Oktoba-Disemba, 2020) katika maeneo ya pwani ya kaskazini na nyanda za juu kaskazini mashariki zinatarajiwa kuanza kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 kama zilivyotabiriwa hapo awali (Septemba, 2020) na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kufuatilia hali hiyo katika bahari ya Hindi pamoja na mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa kwa ujumla na itatoa taarifa za mrejeo kila itakapobidi. USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania na kuzingatia tahadhari zinazotolewa na mirejeo yake pamoja na kupata na kuzingatia ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kupunguza athari zinazoweza kujitokeza.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...