Thursday, August 13, 2020

HALI YA BAHARI KUFUATIA TETEMEKO LA ARDHI CHINI YA BAHARI YA HINDI.

 

Dar es Salaam, 12 Agosti 2020:

 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa kuhusu hali ya bahari

kufuatia tetemeko la ardhi chini ya bahari ya Hindi. Leo tarehe 12/08/2020 majira ya saa mbili (2) usiku, tumepokea taarifa zilizothibitishwa na “Geological Survey of Tanzania” (GST) kuhusu tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 5.9 katika eneo la kusini mashariki mwa Mkoa wa Pwani katika bahari ya Hindi.

 Kutokana na Tetemeko hilo kutokea katika eneo la chini ya bahari, Mamlaka ya Hali yaHewa Tanzania imefanya uchambuzi wa taarifa za tetemeko hilo katika kituo chake cha Tahadhari ya Tsunami ili kuona iwapo kuna uwezekano wowote wa tetemeko hilo kusababisha mawimbi ya Tsunami baharini. Matokeo ya uchambuzi huo yanaonesha kuwa hakuna tishio la Tsunami kutokana na tetemeko hilo. Tetemeko hilo halikuwa nguvu kubwa na hakuna maporomoko ya ardhi yaliyojitokeza baharini ambayo yangeweza kuzalisha tsunami.

 TMA inaendelea kufuatilia mifumo ya hali ya hewa baharini na kutoa taarifa endapo kutajitokeza mwendelezo wa matetemeko katika eneo la Bahari.

 ATHARI: Hakuna adhari zilizojitokeza au zinazotarajiwa katika mifumo ya hali ya hewa ya bahari kutokana na tetemeko hilo.

 USHAURI: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inawashauri watumiaji wa eneo la bahari ikiwa ni pamoja wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyokaribu na bahari ya Hindi kutokuwa na hofu na kuendelea na shughuli kwa kuzingatia taarifa ya hali ya hewa Baharini kama ilivyotolewa awali na Mamlaka.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...