Dar es salaam, 24 Januari
2020.
Dr. Hamza Kabelwa ambaye
ni Mkurugenzi wa huduma za utabiri wa hali ya hewa wa Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA), kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Makamu wa
Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi
amefungua mkutano wa wadau wa kitaifa wa maandalizi ya mkutano mkubwa wa wadau
wa huduma za setilaiti barani Afrika unaotarajiwa kufanyika Jijini Dar es
Salaam mwezi Septemba 2020 (14th
EUMETSAT User Forum in Africa).
Katika hotuba ya ufunguzi
aliyoiwasilisha kwa niaba ya Dkt. Kijazi aliwashukuru waandaaji wa mkutano huo
ambao ni taasisi ya utafiti ya Ulaya (European Organization for the Exploration
of Meteorological Satellite- EUMETSAT) kwa kuwezesha mkutano huo wa wadau wa
maandalizi na juhudi wanazofanya katika kujenga daraja kati ya watoa huduma (EUMETSAT
na TMA) pamoja na watumiaji wa huduma za Setilaiti zinazohusiana na hali ya
hewa kwa nchi wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Barani Afrika.
“Napenda kuishukuru
taasisi ya EUMETSAT ilivyoshirikiana na TMA, kuwakutanisha wataalamu kutoka
sekta mbalimbali pamoja na Wizara kuja kwenye mkutano huu wa wadau wa
maandalizi ya mkutano wa 14 wa EUMETSAT kwa wadau wa Bara la Afrika “(National
Preparatory Workshop for the 14th EUMETSAT User Forum in Africa)”,
pia nawashukuru EUMETSAT kwa mchango wenu mkubwa katika kutoa huduma za uangazi
ambazo zinatumika katika utabiri wa hali ya hewa wa kila siku na ufuatiliaji wa
hali ya mazingira; ikizingatiwa pia kuwa mimi ni Mwenyekiti wa Kamati ya WMO ya
kuongeza uwezo wa Nchi Wanachama wa WMO katika kuboresha huduma za hali ya hewa
“Capacity building”, alisema Dkt. Kabelwa kwa niaba ya Dkt. Kijazi.
Dkt. Kabelwa aliwakumbusha
wadau kuwa Bara la Afrika linakabiliana na changamoto za kutokuwa na taarifa za
kutosha za uangazi wa hali ya hewa na mazingira ambazo ni muhimu sana katika
kufanya maamuzi, hivyo akawahimiza wadau wa mkutano kushiriki kwa wingi katika
mkutano wa wadau wa Septemba 2020 ikiwa ni pamoja na kuwa mstari wa mbele
katika maandalizi yake ili ufanyike kwa ufanisi na kwa heshima ya Tanzania.
Aidha, wadau wa mkutano
huu wa maandalizi waliwasilisha mada zilizoonesha uzoefu wao katika matumizi ya
huduma zitolewazo na EUMETSAT hususan namna wanavyoshiriki katika miradi ya
kikanda ya ufuatiliaji wa hali ya hewa na mazingira ambayo inalenga kuboresha
huduma za hali ya hewa na mazingira katika nyanja kuu nne (4) ambazo ni ufuatiliaji
wa matukio ya ukame, matukio ya mafuriko, matukio ya moto na kilimo. Taarifa
hizi ni za muhimu sana katika maendeleo ya kijamii na uchumi wa nchi yetu.
No comments:
Post a Comment