Dar es Salaam, 06 Januari
2020:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa
juu ya hali ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini.
Kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila
mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia.
Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali
ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. Hapa nchini,
vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele kati ya
mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini
(Tropiki ya Kaprikoni) na hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati
jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi
huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia
katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Hali hii
hujitokeza zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mawingu na mvua ambazo husaidia
katika kupunguza hali ya joto katika kipindi husika.
Nyakati za usiku pia kunaonekana kuwa na hali ya joto
kutokana na kuwepo na kiwango kikubwa cha unyevunyevu angani kinachofika
asilimia themanini na zaidi kwa baadhi ya maeneo. Unyevunyevu huo hutunza hali
ya joto litokanalo mionzi ya jua na hivyo kuleta hali ya fukuto.
Kwa sasa msimu wa mvua za Vuli umeisha katika maeneo
mengi hususan yale yaliyoko ukanda wa
Pwani, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na baadhi ya maeneo ya mikoa ya
Simiyu, Shinyanga hivyo kuwa na joto kali. Pamoja na maeneo hayo mkoa wa Tabora
nao unatarajiwa kuendelea kupata vipindi
vya joto kali. Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kuongezeka katika
mwezi Februari 2020 ambapo jua litakuwa la utosi hapa nchini. Baada ya kipindi
hicho hali ya joto inatarajiwa kuanza
kupungua hasa kuelekea mwezi Machi ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa
kuongezeka katika maeneo yanayopata mvua za msimu na kuanza kwa msimu wa mvua
za masika na hivyo kupunguza hali ya
joto kali.
Hata hivyo, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea
kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, hivyo
tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua
stahiki kila inapobidi.
No comments:
Post a Comment