Sunday, January 19, 2020

DKT. BURUHANI NYENZI AMBAE NI RAIS WA TANZANIA METEOROLOGICAL SOCIETY (TMS) NA MAKAMU WA RAIS WA JUKWAA LA KIMATAIFA LA VYAMA VYA WATAALAM WA HALI YA HEWA DUNIANI (IFMS) ANAYESHUGHULIKIA UTAWALA, AYATANGAZA MAFANIKIO YA TMS KATIKA MKUTANO WA SITA WA JUKWAA HILO.



Rais wa Chama cha wataalam wa sayansi ya hali ya hewa Tanzania (TMS) na makamu wa Rais wa IFMS anayeshughulikia masuala ya utawala, Dkt. Buruhani Nyenzi akiwasilisha mada kuhusu shughuli zilizofanywa na TMS kwa mwaka 2019.
Washiriki wa mkutano wa 6 wa IFMS wakiwa katika picha ya pamoja na makamu wa tatu wa Rais wa WMO Dkt. Agnes Kijazi na Katibu mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas wakati wa ufunguzi wa mkutano huo.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) akifuatilia mawasilisho mbalimbali yaliyowasilishwa katika  ufunguzi wa mkutano wa sita wa IFMS.
Washiriki wa mkutano wa IFMS wakifuatilia mada iliyowasilishwa na katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani. Katika meza ya mbele, kulia ni Rais wa IFMS, Dkt. Harinder Ahluwalia na kushoto ni Rais wa TMS na makamu wa Rais wa IFMS, Dkt. Buruhani Nyenzi.

Rais wa Chama cha Wataalamu wa Sayansi ya Hali ya Hewa Tanzania “Tanzania Meteorological Meteorological Society (TMS)”, Dkt. Buruhani Nyenzi amesema kwamba, licha ya changamoto zilizokuwepo katika mwaka 2019, chama hicho kimeweza kupiga hatua katika kutekeleza majukumu yake.  Dkt Nyenzi alisema hayo tarehe 16 Januari 2016 wakati akiwasilisha mada inayohusu shughuli zilizofanywa na TMS kwa mwaka 2019 katika Mkutano wa 6 wa Jukwaa la Kimataifa la Vyama vya Wataalamu wa Hali ya Hewa Duniani “International Forum of Meteorolocal Societies (IFMS) uliofanyika kuanzia tarehe 14 hadi 16 Januari, 2020 Boston nchini Marekani.

Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana kwa mwaka 2019 ni pamoja na kuanza kwa mchakato wa kuandaa mpango mkakati wa TMS; kuongezeka kwa idadi ya wanachama; na kushiriki katika kutoa elimu kwa wadau wa huduma za hali ya hewa, jambo ambalo limechangia kuboresha zaidi matumizi ya utabiri wa hali ya hewa utolewao na TMA. Alisema Dkt. Nyenzi. Rais huyo wa TMS ambaye pia ni Makamu wa Rais wa IFMS anayeshughulikia masuala ya utawala alisema ushirikiano uliopo kati ya TMA na TMS unafaa kuigwa na vyama vingine hasa katika nchi za Afrika ambapo vyama vingi vinashindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na ushirikiano hafifu na Taasis za hali ya hewa katika nchi hizo. Pamoja na mafanikio hayo changamoto kubwa inayoikabili TMS ni ufinyu wa bajeti, ambapo chanzo kikuu cha mapato ni michango ya wanachama pekee ambayo hata hivyo haitolewi kwa wakati. Aliongeza Dkt. Nyenzi.

Awali akifungua mkutano huo Rais wa IFMS Dkt. Harinder Ahluwalia aliwasisitiza viongozi wa vyama vya wataalamu wa hali ya hewa  na wadau wengine wa sekta binafsi kuunganisha nguvu ili kusaidia kukuza sekta ya hali ya hewa. Alifafanua ushirikiano uliopo kati ya IFMS na WMO na akamshukuru Dkt. Agnes Kijazi ambaye ni makamu wa tatu wa Rais wa WMO kwa kuhudhuria ufunguzi wa mkutano huo. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Prof. Petteri Taalas alisema sekta binafsi, vikiwemo vyama vya wataalamu wa hali ya hewa vinatarajiwa kutoa mchango chanya katika utekelezaji wa mpango mkakati wa WMO, ambao unaenda sambamba na mabadiliko ya kimuundo katika Shirika hilo. Alisema mabadiliko hayo yamelenga kupunguza changamoto za sekta ya hali ya hewa  ili kukidhi mahitaji ya wadau, ambayo yameendelea kuongezeka, hususan katika kipindi hiki ambacho dunia inakabiliwa na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.

Mkutano wa IFMS umefanyika kwa mujibu wa kalenda ya shughuli zake za mwaka 2019, kwa lengo la kujadili utekelezaji wa shughuli za vyama vya wataalamu wa sayansi ya hali ya hewa vya Nchi wanachama wa WMO. Mkutano huo umefanyika sambamba na mkutano mkuu wa 100 wa Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa  cha Marekani “100th Annual Meeting of American Meteorological Societies (AMS100).

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...