Tuesday, January 14, 2020
DKT. KIJAZI AWATAKA WATENDAJI WA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO) KUTOA MWONGOZO KWA NCHI WANACHAMA KUHUSU NJIA BORA ZA KUFUNGASHA NA KUWASILISHA TAARIFA ZA HALI YA HEWA KWA JAMII ZILIZO KATIKA MAZINGIRA HATARISHI
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirikia la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Lawrence Kijazi, amewataka watendaji wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kuandaa mwongozo kwa nchi wanachama kuhusu njia sahihi za kuboresha ufungashaji (packaging) na uwasilishwaji (communication) wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa.
Alizungumza hayo katika mkutano ulioandaliwa na WMO kwa kushirikiana na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Marekani “National Oceanic and Atmospheric Administration (NOAA)- National Weather Service”, uliofanyika sambamba na mkutano wa American Meteorological Society unaoendelea Boston, nchini Marekani, kuanzia tarehe 10 hadi 16 Januari, 2020.
“Tunatakiwa kuandaa mpango katika ngazi ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani utakaotoa mwongozo ambao utawezesha nchi wanachama kuboresha njia za ufungashaji na uwasilishaji wa taarifa za hali ya hewa ili kuhakikisha taarifa hizo zinawafikia walengwa katika mfumo (format) unaoeleweka na kwa wakati kwa lengo la kuziwezesha jamii zinazoishi katika mazigira hatarishi kuchukua hatua stahiki zitakazosaidia kupunguza maafa”. Alisema Dkt. Kijazi wakati akichangia mada.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa WMO, ikiwa ni pamoja na Rais wa WMO (Prof. Gerhard Adrian- Ujerumani), Makamu wa kwanza wa Rais wa WMO (Prof. Celeste Saulo - Urgentina), Makamu wa Pili wa Rais wa WMO (Bwana Albert Martis - Curacao), Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO (Dkt. Agnes Kijazi -Tanzania) na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas - Finland, wakuu wa taasisi za hali ya hewa kutoka baadhi ya nchi wanachama wa WMO na wadau wa huduma za hali ya hewa, miongoni mwao wakiwemo sekta binafsi na watafiti kutoka vyuo vikuu.
Lengo la mkutano huo lilikuwa kujadili uboreshaji wa uandaaji, ufungashaji na uwasilishwaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi, hususan visiwa vilivyopo katika ukanda wa tropiki na ‘arctic’ (Improving Communication and Preparedness in Vulnerable Regions and Underserved Communities of the tropical and Arctic region islands), ambavyo viko katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na vimbunga na mawimbi ya Tsunami.
Aidha, majadiliano ya mkutano huo yalijielekeza zaidi katika matokeo ya tafiti zilizofanyika katika nchi za Guyana, Finland, Indonesia, Marekani (Jimbo la Alaska), visiwa vya Caribbean na Bahamas, pamoja na eneo la Pasifiki. Tafiti hizo ziliainisha changamoto katika uandaaji, ufungashaji na uwasilishwaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii zinazoishi katika mazingira hatarishi ya kukumbwa na majanga yanayotokana na hali mbaya ya hewa. Vile vile, tafiti hizo ziliainisha njia za asili zinazotumiwa na jamii hizo katika kuchukua tahadhari na kutoa mapendekezo ya kuboresha ili kupunguza maafa yanayotokana na majanga hayo.
Kwa upande mwingine, akichangia mada hiyo, Dkt. Kijazi alifafanua kwamba kwa kuwa changamoto zilizowasilishwa zinaweza kuwepo katika maeneo mengine duniani, yakiwemo maeneo yanayofanana na hayo yaliyopo katika Bara la Afrika, ni vyema kuandaa mpango wa pamoja utakaoratibiwa na WMO wa kushughulikia changamoto hizo kwa maeneo yaliyoainishwa katika mkutano huo pamoja na maeneo mengine yote duniani yanayokabiliwa na changamoto hizo ikiwemo bara la Afrika.
Ili kuharakisha utatuzi wa changamoto zilizowasilishwa pamoja na kujadiliana njia bora ya kuzitatua kupitia programu mbali mbali za Shirika la Hali ya Hewa Duniani, viongozi waandamizi wa WMO (Rais na makamu wote watatu wa Rais) wameazimia kufanya vikao kwa njia ya mtandao (teleconference) kila mwisho wa mwezi, kuanzia mwezi Januari 2020. “ Tutafanya mikutano ya mtandao kila mwisho wa mwezi ili kuwa katika nafasi nzuri ya kufuatilia utekelezaji wa makubaliano yanayofikiwa ikiwa ni pamoja na maelekezo yaliyotolewa katika Congress”. Alisema Prof. Gerhard Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Featured Post
DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.
Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...
-
10 Septemba 2024, Arusha: Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa elimu kwa wadau mbalilmbali wa Ununuzi kuhusu matumizi sahihi ya h...
-
06 Septemba 2024, Dar es Salaam: Wahandisi nchini wamekumbushwa umuhimu wa huduma za hali ya hewa sambamba na kuchangia gharama za upatik...
-
DODOMA; Tarehe 19 Agosti, 2024; Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali nchini ili kujipanga na...
No comments:
Post a Comment