Wednesday, March 27, 2019

MATUKIO MBALI MBALI KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA HEWA DUNIA (WMD) 2019

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi  na Mawasiliano akizungumza na vyombo vya habari kuhusu WMD 2019
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Mhandisi Japhet Loisimaye akifafanua namna taasis yake inavyozingatia matumizi sahihi ya huduma  za hali ya hewa
Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TAA Bw. Elius Mwashiuya alifafanua jinsi huduma za hali ya hewa zinavyosaidia katika ujenzi na uendeshaji wa viwanja vya ndege nchini
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Bw. Hamza Johari akielezea umuhimu wa huduma za hali ya hewa kwenye sekta usafiri wa anga
Baadhi ya washiriki wakifuatilia jambo wakati wa maadhimisho hayo
Mkurugenzi Mkuu wa TMA akimkaribisha mhe. waziri kuzungumza
Wafanyakazi wa TMA wakishiriki igizo fupi la kuonesha umuhimu wa huduma za hili ya hewa katika shughuli za uchumi na kijamii kwa ujumla

Saturday, March 23, 2019

BARAZA: WAZIRI KAMWELWE AIPONGEZA TMA KWA KUFANIKIWA KUPATA SHERIA MPYA ILIYOSAINIWA NA MHE RAIS.

Mhe. Isack Kamwelwe katika picha ya pamoja na menejiment ya TMA
Mhe. Isack Kamwelwe katika picha ya pamoja na wajumbe wa baraza la wafanyakazi wa TMA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Isack Kamwelwe ameipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) kwa kufanikiwa kupata sheria mpya ya huduma za hali ya hewa nchini. Waziri Kamwelwe alizungumza hayo wakati akilifungua rasmi Baraza la Wafanyakazi wa TMA, tarehe 22 Machi 2019.

‘Napenda kutumia nafasi hii kipekee kabisa kuipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania chini ya uongozi wa Wizara yangu kwa sheria iliyopitishwa na Bunge la jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Januari, 2019 na kusainiwa na Mhe. Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuri’.  Alizungumza mhe. Kamwelwe

Mhe Kamwele aliongezea kwa kusema sheria hii inaipa TMA mamlaka kamili ya kutoa huduma na kuhakiki shughuli zote zinazohusiana na hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru mhe waziri kwa kukubali kufungua baraza la wafanyakazi wa TMA na kuelezea madhumuni ya baraza hilo.

‘Madhumuni makuu ya Baraza hili ni kupokea, kujadili na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Mamlaka kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020’. Alizungumza Dkt. Kijazi

‘Aidha, mapendekezo hayo ya bajeti yanazingatia vipaumbele vitakavyo iwezesha Mamlaka kufikia malengo yake na kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa  huduma za hali ya hewa kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za hali mbaya ya hewa na hivyo kuchangia katika kukuza pato la Taifa’. Aliongezea Dkt. Kijazi


TAARIFA YA WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO NA MKURUGENZI MKUU WA TMA KATIKAKUADHIMISHA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 23 MACHI 2019

Mhehimiwa Mhandisi Isack Kamwelwe

Muhtasari wa Taarifa ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Mhandisi  Isack Kamwelwe kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day (WMD)”, Ukumbi wa Wizara, Dar es Salaam, 23 Machi 2019.

Ni heshima kubwa kwangu kuwepo nanyi kwenye kilele cha maadhimisho haya ya siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day (WMD)” kwa mwaka 2019. Naipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kuandaa maadhimisho haya. Haya ni maadhimisho ya 69 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) mwaka 1950. Kauli mbiu ya mwaka  huu ni  “Jua, Dunia, na Hali ya Hewa (The Sun, The Earth, and the Weather)”,  ambayo imelenga kutoa elimu kwa jamii na kuongeza uelewa wa sayansi ya hali ya hewa, hususan maandalizi, usambazaji na matumizi ya taarifa za hali ya hewa.
Siku ya Hali ya Hewa Duniani ni muhimu sana kwani inatupa nafasi ya kutafakari mchango wa Tanzania, kama mwanachama wa WMO katika utoaji wa huduma za hali ya hewa hapa Tanzania na ulimwenguni kote.
Kwa upande wa Tanzania, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kusimamia na kutoa huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa minajili hii Serikali yetu inaendelea kuwekeza katika kuimarisha huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya uangazi, kwa mfano ununuzi wa RADAR na vifaa vingine vya hali ya hewa ambavyo ni kipaumbele kama ilivyolekezwa katika Mpando wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Taifa  (2016/2017-2020/2021) chini ya Serikali ya awamu ya Tano.  Mpaka sasa Serikali tayari imenunua RADAR mbili za hali ya hewa ambazo zimewekwa Dar es Salaam na Mwanza. RADAR nyingine tatu zinatarajiwa kuwekwa Mtwara, Mbeya na Kigoma na ziko katika hatua za ununuzi.
Ni dhahiri kwamba huduma zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania zimeendelea kuongezeka viwango vya ubora ikiwa ni pamoja na usahihi wa utabiri na hivyo zinafaa kutumika katika sekta mbali mbali za maendeleo hapa nchini. Ninatoa wito kwa wadau wote wa hali ya hewa kutoka sekta zote za kiuchumi na kijamii na wananchi kwa ujumla kuendelea kufuatilia na kutumia huduma za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa ajili ya kupanga na kufanya maamuzi katika shughuli za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya ustawi wa Taifa letu.
Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha huduma za hali ya hewa kwa matumizi ya sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya usafiri wa anga, ambapo katika mwaka 2019 Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi tatu barani Afrika zilizopata cheti cha ubora wa huduma za hali ya hewa katika usafiri na usalama wa anga (ISO 9001:2015) kwa mujibu wa Shirika la Viwango Duniani (ISO). Katika kuboresha usambazaji wa huduma za hali ya hewa, TMA imebuni mfumo wa kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi uitwao FarmSMS ambao umerahisisha upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa kwa wadau.
Haya ni mafanikio makubwa katika kutekeleza mkataba wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani na kauli mbiu ya siku ya hali ya hewa Duniani ya mwaka huu. Pamoja na mafanikio haya, bado kuna changamoto nyingi zikiwemo gharama kubwa za vifaa vya hali ya hewa, kuendana na mabadiliko ya kukua kwa teknolojia katika tasnia ya hali ya hewa na mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi (Climate Change). Utatuzi wa changamoto hizi unahitaji jitihada za pamoja za wadau mbalimbali.
Hivyo napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa wadau mbalimbali wa huduma za hali ya hewa kushirikiana na Serikali katika kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate Servives), ambayo ni mwongozo muhimu katika utoaji na utumiaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini.
Mwisho, napenda kuwashukuru tena na kuwapongeza TMA na WMO kwa maadhimisho haya ya siku ya hali ya hewa Duniani. Natoa wito kwa jamii yote, ambao kimsingi ndio watumiaji wa taarifa za hali ya hewa tusherehekee siku hii kwa kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kwa usalama wetu na mali zetu.
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2019
“Jua, Dunia, na Hali ya Hewa
 
Dkt. Agnes Kijazi
UJUMBE WA MKURUGENZI MKUU WA MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA), DKT. AGNES KIJAZI KWENYE KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI “WORLD METEOROLOGICAL DAY (WMD)”, 23 MACHI, 2019.
Leo ni siku ya Hali ya Hewa Duniani “the World Meteorological Day (WMD)”, siku ambayo dunia inaadhimisha kuanzishwa kwa Shirika la Hali Duniani (WMO) ambapo Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika hilo ulisainiwa mnamo tarehe 23 Machi 1950. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikiwa moja wapo ya Taasisi za Hali ya Hewa za nchi 192 wanachama wa WMO inaungana na Jumuiya ya Hali ya Hewa Ulimwenguni  kote kusheherekea  siku hii. Taasisi za Hali ya Hewa, hutumia siku hii kueleza huduma za hali ya hewa na umuhimu wa kuzingatia na kujumuisha taarifa za hali ya hewa, ikiwemo utabiri na tahadhari katika kupanga na kutekeleza shughuli mbalimbali za kiuchumi, kijamii na kimaendeleo kwa ujumla.

Kwa upande wa hapa nchini Tanzania, huduma za hali ya hewa hutolewa na kusimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA).  TMA ni taasisi ya serikali chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Mamlaka imepewa dhamana ya kutoa na kusimamia huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ili kusisitiza na kuhamasisha umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika mipango na maamuzi ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika sekta mbalimbali, Uadhimishaji wa sherehe za siku ya Hali ya Hewa Duniani unaambatana na kauli mbiu maalumu kwa kila mwaka. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Jua, Dunia na Hali ya hewa (The Sun, The Earth, and the Weather)”. Kauli mbiu hii imechaguliwa kwa kuzingatia ukweli kwamba jua ndicho chanzo kikuu cha nishati ambayo huwezesha maisha ya viumbe vyote hapa duniani na huendesha mifumo ya hali ya hewa, mikondo ya bahari na mzunguko wa maji (hydrological cycle) na kuchangia katika shughuli zetu za kila siku za kiuchumi na kijamii katika uso wa Dunia.

Jua ndio nyota iliyo karibu zaidi na Dunia, umbali upatao Kilometa milioni 150 kutoka uso wa Dunia. Jua ndicho kitovu cha Unajimu na chanzo kikuu cha joto lililopo katika uso wa dunia ambalo linahitajika na viumbe hai mbalimbali ili viweze kuishi. Bila mwanga na joto litolewalo na jua kusingekuwa na maisha yoyote katika uso wa Dunia. Hivyo, joto litokanalo na jua ndilo husababisha mzunguko wa maji (hydrological cycle), mvukizo wa maji angani (evaporation) ambayo huganda na kufanyika mawingu na kisha kurudi tena kwenye uso wa Dunia kwa njia ya mvua. Mbali na kuwa chanzo kikuu cha mifumo ya hali ya hewa tunayoipata na kuwezesha maisha ya viumbe hai, mwanga wa jua una mchango wa pekee katika afya na ustawi wa viumbe hai na masuala ya Nishati. Inatazamiwa kuwa mchango wa Nishati mbadala katika mahitaji ya nishati ya dunia utafikia asilimia 40% ifikapo mwaka 2040. Uimarishaji wa upatikanaji na matumizi ya Nishati mbadala, ikiwemo nishati ya Jua na nishati ya upepo unahitaji jitihada kubwa za kuimarisha shughuli za uangazi wa hali ya hewa, ambapo mchango na wajibu wa Taasisi za Hali ya Hewa ikiwemo TMA ni mkubwa. Utoaji wa taarifa za hali ya hewa mahsusi kwa ajili ya masuala ya nishati ni wa muhimu sana, ukizingatia mikakati ya jumuiya ya kimataifa ya kuimarisha matumizi ya nishati mbadala ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa (climate change). Uelewa kuhusu hali ya klimatolojia ya eneo husika ikiwemo mwenendo wa jua na nguvu yake, pamoja na nishati ya upepo ni muhimu sana katika kutoa mwongozo na kuongeza ufanisi na tija kwa uwekezaji  unaolenga kuimarisha nishati mbadala.
Katika kuimarisha upatikanaji na utumiaji wa taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii na kufikia maendeleo endelevu jitihada mbalimbali za kuboresha huduma za hali ya hewa katika ngazi ya kidunia na kitaifa zinafanyika. Katika ngazi ya kidunia, Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa “The Global Framework for Climate Services (GFCS)” ndiyo programu inayotoa mwongoza wa namna ya kuboresha utoaji na utumiaji wa  taarifa za hali ya hewa katika mipango na maamuzi kwenye sekta mbali mbali za kiuchumi na kijamii duniani. Katika kuendeleza jitihada za kidunia, Tanzania inatekeleza Programu ya Kitaifa ya Huduma za Hali ya Hewa “the National Framework for Climate Services (NFCS)”, ambayo ilizunduliwa rasmi mwezi julai, 2018 ikiwa na malengo ya kuboresha huduma za hali ya hewa hususan kwa sekta zilizo katika hatari ya kuathirika zaidi na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya tabia nchi zikiwemo Kilimo na Usalama wa chakula, Maji, Afya, Nishati na Maafa. Utekelezaji wa mpango wa NFCS umejikita katika kuimairisha shughuli za uangazi, utabiri, utafiti, ushirikishwaji wa Wadau na kujenga uwezo wa wataalamu na watumiaji wa taarifa za hali ya hewa.

Utabiri utolewao na TMA ni pamoja na utabiri wa kila siku (masaa 24), siku tano, siku kumi, mwezi, msimu na taarifa za hali mbaya ya hewa (severe weather warnings and alerts). Tabiri hizi za hali ya hewa ni kwa jamii yote kwa ujumla, na kwa sekta maalumu kama vile sekta ya usafiri wa anga, usafiri wa kwenye maji na nchi kavu, kilimo (kilimo mazao, mifugo na uvuvi), nishati, maji, utalii, afya, na usimamizi wa majanga kwa kutaja maeneo machache.

Taarifa hizi husambazwa kwa njia mbalimbali zikiwemo tovuti ya TMA (www.meteo.go.tz), radio, runinga, mitandao ya kijamii (facebook, twitter and Youtube), magazeti na Mfumo wa Kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa njia ya simu za mkononi (FarmSMS).

Katika kuadhimisha siku ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2019, napenda kutoa wito kwa wadau wote kuzifuatilia na kuzitumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii kwa ajili ya maendeleo endelevu ya  nchi yetu na hasa kuchangia katika azma ya nchi yetu kwenda katika uchumi wa kati na uchumi wa viwanda
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani “World Meteorological Day” (WMD).

“Jua, Dunia na Hali ya Hewa”.

Siku ya Hali ya Hewa Duniani 2019


Thursday, March 21, 2019

TMA YATOA MREJEO WA MUELEKEO WA MVUA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2019


Taarifa hiyo imeelezea uwepo wa migandamizo midogo ya hewa kuanzia tarehe 5 Machi, umepelekea kutokea kwa kimbunga (Idai) kuanzia tarehe 10 hadi 15 Machi, 2019 katika rasi ya Msumbiji na kusababisha upepo wenye unyevunyevu kusukumwa kusini mwa Afrika na hivyo kupelekea upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi hususan ukanda wa kaskazini. Migandamizo midogo ya hewa inaendelea kujitokeza katika maeneo ya kaskazini mwa Madagascar, ambapo kwa sasa moja ya migandamizo hiyo imeimarika na kuwa kimbunga Savannah. Migandamizo na vimbunga hivi vinatarajiwa kusababisha mvua kuelekea zaidi katika maeneo ya bahari ya Hindi na upungufu katika maeneo mengi ya nchi, kutokana na mahali mwelekeo unaotarajiwa.

Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na jinsi inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi cha Machi – Mei 2019 (kama ilivyoelezwa katika kipengele II cha taarifa hii);

Uwezekano mkubwa wa upungufu wa mvua katika mikoa ya Dar es salaam, Pwani, Tanga, maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na vipindi vichache vya upungufu wa mvua katika maeneo machache ya mikoa ya Kilimanjaro na Manyara.
Mwelekeo wa mvua za Masika uliotolewa ulionesha kuwa mvua zinatarajiwa kuwa za muda mfupi na kuisha mapema kati ya wiki ya nne ya mwezi Aprili na wiki ya kwanza ya mwezi Mei, 2019. Hata hivyo, hali iliyopo sasa inaonesha uwezekano wa mvua za Masika kuisha mapema zaidi katika baadhi ya maeneo wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019.
Mvua za msimu (Novemba-Aprili) zinatarajiwa kuendelea kama zilivyotabiriwa. “Mvua za Msimu ambazo zilianza mwezi Novemba, 2018 zinatarajiwa kuendelea hadi mwishoni mwa mwezi April 2019. Katika kipindi hicho mvua hizo za Msimu zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo machache ya kanda ya Kusini (Ruvuma), pamoja na mikoa ya Dodoma na Singida”.
I. MREJEO WA MWELEKEO WA MSIMU WA MVUA KIPINDI CHA MACHI - MEI 2019

Msimu wa mvua za Masika ni mahususi katika maeneo ya Nyanda za Juu Kaskazini-mashariki, pwani ya Kaskazini na visiwa vya Unguja na Pemba, ukanda wa Ziwa Victoria pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Ufuatao ni mwelekeo wa mvua za Masika kwa kipindi kilichosalia;

a) Kanda ya Ziwa Victoria (Mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara na Simiyu): Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani kwa ujumla katika maeneo ya mikoa ya Mwanza, Geita, Shinyanga, Simiyu na Mara. Hata hivyo, maeneo machache ya mkoa wa Kagera na wilaya ya Kibondo yanatarajiwa kuwa na upungufu wa mvua. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019.

b) Ukanda wa Pwani ya Kaskazini: (Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro):

Katika kipindi cha msimu kilichosalia, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika maeneo ya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga pamoja na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. Aidha, mvua za wastani kwa ujumla zinatarajiwa katika maeneo mengi ya visiwa vya Unguja na Pemba. Pamoja na mvua za juu ya wastani kujitokeza katika maeneo machache ya visiwa vya Unguja na Pemba, mvua zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili, 2019. Mvua katika maeneo ya mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro zinatarajiwa kuisha katika wiki ya pili ya mwezi Aprili, 2019.

c) Nyanda za juu Kaskazini Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara):

Kwa ujumla, mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi. Hata hivyo, mvua za juu ya wastani zinatarajiwa kujitokeza katika maeneo machache ya mkoa wa Arusha. Mvua zinatarajiwa kuisha mapema katika wiki ya tatu ya mwezi Aprili, 2019.

II. MIFUMO YA HALI YA HEWA

Hali ya joto la bahari pamoja na mifumo ya hali ya hewa inaonesha upungufu wa mvua katika maeneo mengi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka. Katika kipindi cha msimu kilichosalia, joto la bahari la juu ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya kati na kusini magharibi mwa bahari ya Hindi, hali ambayo inatarajiwa kupelekea kuvuma kwa upepo hafifu kutoka mashariki na kusababisha upungufu wa mvua katika maeneo mengi nchini. Halikadhalika, joto la bahari la wastani hadi juu kidogo ya wastani linatarajiwa katika eneo la kusini mashariki mwa bahari ya Atlantic karibu na pwani ya Angola. Hali hii inatarajiwa kupunguza msukumo wa upepo kutoka magharibi na hivyo kupunguza uwepo wa unyevunyevu kutoka misitu ya Kongo.

III. USHAURI

Mamlaka ya Hali ya Hewa inawashauri watumiaji wa taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na wakulima, wafugaji, Mamlaka za Wanyamapori, Mamlaka za Maji na Afya waendelee kutafuta, kupata na kufuata ushauri wa wataalamu katika sekta husika.

Mwelekeo wa mvua uliotolewa hapa umezingatia zaidi kipindi cha msimu (miezi mitatu) na hali ya mvua katika maeneo makubwa. Hivyo, viashiria vinavyochangia mwenendo wa mifumo ya mvua na mabadiliko ya muda mfupi katika maeneo madogo utazingatiwa katika uchambuzi wa utabiri wa muda wa kati na mfupi. Watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa pia kufuatilia utabiri wa saa 24, siku 10 pamoja na mwezi kama unavyotolewa na Mamlaka ya hali ya Hewa Tanzania.

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania itaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na kutoa taarifa za mwelekeo wa mvua nchini.

Wednesday, March 13, 2019

TUKIO: MAADHIMISHO YA SIKU YA HALI YA HEWA DUNIANI 23MACHI, 2019


Katika kuadhimisha siku hii kwa mwaka 2019, TMA itatoa elimu kwa jamii hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, na wananchi kwa ujumla kupitia vyombo vya habari na kufundisha mashuleni na pia kuelimisha watakaotembelea vituo vya hali ya hewa.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka huu wa 2019 ni "Jua Dunia, na Hali ya Hewa ( The sun, The Earth, and the Weather)". Kauli mbiu hii inalenga kutoa elimu kwa jamii na kuongeza uelewa wa taarifa za hali ya hewa.

Monday, March 11, 2019

TMA YAKUTANA NA WADAU WA HUDUMA ZA BAHARINI KUJADILI NAMNA YA KUBORESHA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KWA USALAMA WA MAISHA YA WATU NA MALI ZAO.
















Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika jitihada zake za kutambua umuhimu wa ushirikishwaji wa wadau wa huduma za hali ya hewa ili kuhakikisha huduma zitolewazo zinakidhi matwaka ya watumiaji, imekutana na wadau wa huduma za hali ya hewa baharini ili kupata mrejesho wa huduma zinazotolewa na kuweza kuzifanyia maboresho kulingana vigezo vya kitaifa na kimataifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho cha wadau wanaotumia huduma za hali ya hewa kwa shughuli baharini kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Baharia (DMI), tarehe 08 Machi 2019, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi aliwaeleza washiriki wa mkutano lengo ni kutoa uelewa wa huduma zitolewazo na kupokea mrejesho pamoja na kuibua fursa za ushirikiano kati ya TMA na wadau hao na kusaidia katika kuboresha huduma.

lengo la mkutano huu ni kuwapa uelewa wa huduma za hali ya hewa zinazotolewa kwaajili ya watumiaji wa bahari na pia kupata mrejesho kutoka kwenu kuhusu huduma hizo sambamba na kuibua fursa za ushirikiano kati ya TMA na ninyi watumiaji wa huduma za hali ya hewa ili kuboresha huduma zinazotolewa katika sekta hii ya bahari ‘Alizungamza Dkt. Kijazi’.

Aidha, aliongezea kwa kueleza kuwa mkutano huo unasaidia kuibua fursa na changamoto zilizopo ili kwa pamoja tuweze kufanikiwa katika utoaji na utumiaji wa huduma za hali ya hewa kwa shughuli za bahari na maziwa makuu kwa kuzingatia miongozo ya ndani na miongozo inayotolewa na Mashirika ya kimataifa ikiwemo  Shirika la Hali ya Hewa Duniani - (WMO);  Shirika la Kimataifa la Bahari – (IMO) na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa kupitia kamisheni inayohusu masuala ya bahari ya Hindi - (UNESCO-IOC).

Vile vile, wadau walipata fursa ya kupitia mfumo mpya wa mawasiliano unaoitwa Mfumo wa Mawasiliano wa Taarifa za za Hali ya Hewa Baharini – Marine Meteorological Information System (MMIS) unaoundwa na kuweza kutoa michango yao ya maboresho kabla ya kuzinduliwa rasmi.

Kwa upande wa wadau waliipongeza TMA kwa kuandaa warsha/mkutano kama huo wenye lengo la kukidhi mahitaji ya wadau na kushauri kuwa endelevu ili kufika malengo ikiwa ni pamoja na mafunzo ya mfumo, kufanikisha huduma za baharini zinapata cheti cha ubora kama zilivyo huduma za usafiri wa anga.

Mkutano huo wa wadau uliwakutanisha wadau kutoka Mamlaka ya Bandari za Tanzania Bara na Visiwani (TPA na ZPC), Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC),   Chuo cha Bahari (DMI), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Chama cha Maafisa wa Meli Tanzania (MNOAT), Shirika la Maendeleo ya Mafuta (TPDC),  wakala wa makampuni ya meli kama vile PIL, MESSINA, Chama cha Mabaharia (TSC), Flyinghorse na wengine wengi

IMETOLEWA NA
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Tuesday, March 5, 2019

UFUNGUZI WA MAFUNZO YA HALI YA HEWA KWA AJILI YA MATUMIZI YA KILIMO

Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya taarifa za hali ya hewa wa TMA dkt. Ladislaus Chang'a (aliyesimama) akitoa neno kwenye ufunguzi huo.
Washiriki wa mafunzo kwenye picha ya pamoja na mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania dkt. Agnes Kijazi  (wa nne kutoka kushoto)

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...