Thursday, February 28, 2019

KAMWELE APONGEZA UTENDAJI KAZI MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA (TMA)

Matukio mbalimbali kwa picha wakati Mhe. Kamwele akitembelea vitengo mbalimbali vya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi. Isack Kamwele amepongeza utendaji kazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA). Mhe. Kamwele alitoa pongezi hizo wakati alipotembelea Ofisi za TMA, Ubungo Plaza, Dar es Salaam, tarehe 27 Februari  2019 na alipata taarifa ya utendaji kazi wa mamlaka na kutembelea baadhi ya sehemu za kazi kabla ya kuzungumza na wafanyakazi. Mhe. Kamwele alipokelewa na uongozi na menejiment ya TMA, ikiongonzwa na mwenyekiti wa bodi ya ushauri Dkt. Buruhani Nyenzi na kaimu mkurugenzi mkuu Dkt. Ladislaus Chang’a.

“Nawapongeza TMA kwa umakini na utekelezaji wa majukumu yenu, nakiri kusema ni moja ya taasisi makini kati ya taasisi zilizo chini ya wizara yangu nilizo tembelea”. Alizungumza mhe. Kamwele

Aidha, mhe. Kamwele alisisitiza kuboresha mfumo wa ushirikishwaji wa wadau na usambazaji wa taarifa za hali ya hewa, akitolea mfano mafuriko yaliyo bomoa barabara eneo la Dumila, kuwa baada ya kufuatilia taarifa za hali ya hewa waligundua TMA ilitoa taarifa hizo siku mbili kabla ya tukio na kuonesha rangi nyekundu yenye kumaanisha tahadhari kwa maeneo ya Kilindi lakini taarifa hiyo haikuwafikia walengwa.

Mhe. Kamwele alimalizia kwa kuahidi kutatua changamoto zinazoikabili TMA zikiwemo uhitaji wa ongezeko la vituo vya hali ya hewa, mitambo ya hali ya hewa, kupatikana kwa jengo la kituo kikuu cha utabiri n.k

Akitoa salamu za shukrani kwa upande wa TMA, mkurugenzi wa ofisi ya TMA Zanzibar, Bw. Mohamed Ngwali alimshukuru mhe. Waziri kwa pongezi sambamba na kutembelea na kuona shughuli zinazofanywa na TMA, na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa .

Imetolewa:
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)

Monday, February 25, 2019

NDITIYE AZITAKA WIZARA ZINAZOSIMAMIA SEKTA YA HALI YA HEWA AFRIKA KUENDELEA KUSAIDIA TAASISI ZA HALI YA HEWA KATIKA KUFANIKISHA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAKE.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye akihutubia Mkutano wa Nne wa Mawaziri wa Nchi za Afrika wenye Dhamana ya Sekta ya Hali ya Hewa (Fourth Session of the African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET-4), Cairo, Misri, 21 Februari 2019
Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasilino Mhe. Atashasta Nditiye akiwasilisha mada ya umuhimu wa nchi kuwa na mpango mkakati wa Kitaifa (National Strategic Plan) katika Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Hali ya Hewa Afrika (African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET), Cairo, Misri 21 Februari 2019.
Dkt. Kijazi akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Vikosi Kazi vya Wataalamu wa RA1 katika Mkutano wa WMO RA1, Cairo, 23 Februari 2019 akiwa mwenyekiti wa kamati


Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Nditiye  akifurahi jambo na Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas pamoja Dkt. Agnes Kijazi baada ya mazungumzo ya mafupi
Mtaalamu wa hali ya hewa mwandamizi wa TMA Bw. Wilberforce Kikwasi akiwasilisha mada ya mfumo aliotengeneza (invention) wa "Digital  Meteorological Observatory (DMO) ambao unasaidia na kurahisisha katika ukusanyaji, ufungashaji, mawasiliano na usambazaji wa data za hali ya hewa kwa ndani ya nchi na kidunia katika Mkutano wa Mawaziri wenye Dhamana ya Hali ya Hewa Afrika (African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET), Cairo, Misri 21 Februari 2019


Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye amezitaka wizara zinazosimamia sekta ya hali ya hewa katika nchi za Afrika kuhakikisha zinatoa ushirikiano wa hali ya juu kwa taasisi za hali ya hewa ili kufanikisha uboreshaji na utekelezaji wa majukumu yao. Nditiye alizungumza hayo wakati akihutubia mkutano wa Mawaziri wenye dhamana ya kusimamia sekta ya hali ya hewa barani Afrika, Jijini Cairo, Misri tarehe 21 Febrauari 2019 ulipofanyika mkutano wa AMCOMET-4.

“Napenda kuweka msisitizo kuwa ni muhimu sana kwa Serikali zetu kupitia Wizara zinazosimamia sekta ya hali ya hewa katika nchi za Afrika kuhakikisha tunakuwa karibu na kuzisaidia taasisi za hali ya hewa zilizopo chini ya wizara zetu. Hii itasaidia katika kuboresha huduma za hali ya hewa na kurahisisha utekezaji wa majukumu yao kwa manufaa ya nchi zetu”. Alisema Mhe. Nditiye

Aidha, Mhe. Nditiye alielezea namna ambavyo Serikali ya Tanzania imekuwa karibu na inasaidia Mamlaka ya hali ya hewa katika utendaji wake wa kila siku. Mhe. Nditiye alitoa mfano wa namna ambavyo Serikali ya Tanzania kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyosimamia na kufanikisha kupitishwa kwa sheria ya huduma za hali ya hewa mwezi Januari 2019 ambayo itaiwezesha TMA kuwa Mamlaka kutoka kuwa Wakala wa Serikali, kwa lengo hilo hilo la kuboresha huduma za hali ya hewa nchini Tanzania.

Wakati huo huo katika mkutano huo Mhe. Nditiye alizungumzia juu ya umuhimu wa nchi kuwa na mpango mkakati wa Kitaifa (National Strategic Plan) unaohusu utoaji wa huduma za hali ya hewa ambao unaendana na mipango ya maendeleo ya nchi husika, huku akifafanunua faida za utekelezaji wake katika uboreshaji wa huduma za hali ya hewa kijamii na kiuchumi.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya hewa Tanzania (TMA), Dkt. Agnes Kijazi alikuwa miongoni wa ujumbe wa Tanzania ulioshiriki katika mkutano huo wa AMCOMET-4 pamoja na Mkutano wa kumi na saba (17) wa wakuu wa Taasisi za hali ya hewa barani Afrika (RAI-17) uliofanyika pia Jijini Cairo, Misri kuanzia tarehe 22 hadi 23 Februari 2019, ambapo alipata kuungwa mkono kwa wingi na kwa hali ya juu sana na wakuu wenzake wa Taasisi za hali ya hewa barani Afrika kufuatia nia yake aliyoonesha ya kugombea nafasi ya makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambayo iko wazi na uchaguzi na uchaguzi wa viongozi wa WMO utakaofanyika katika Mkutano Mkuu wa WMO (WMO Congress), Juni 2019.

Mkutano wa AMCOMET-4 ulikutanisha washiriki mbalimbali kutoka nchi za bara la Afrika wakiongozwa na Mawaziri wenye dhamana ya sekta ya hali ya hewa au wawakilishi wao, Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kupitia Katibu Mkuu, Prof Petteri Taalas na Sekretariati ya WMO kanda ya Afrika, Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za nchi za Afrika, wataalamu mbalimbali wa hali ya hewa na washirika wa maendeleo kama vile Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Barani Afrika (AfDB).

IMETOLEWA NA MONICA MUTONI
OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Thursday, February 14, 2019

TMA YATOA MWELEKEO WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA MACHI - MEI 2019

Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) dkt. Agnes Kijazi, mbele ya waandishi wa habari  akichambua  mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika Machi - Mei 2019
Picha mbalimbali za waandishi wa habari walioshiriki mkutano wa wanahabari wa kutoa mwelekeo wa mvua za Msimu wa Masika Machi - Mei 2019.


Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu kuanzia mwezi Machi, 2019 hadi Mei, 2019 katika mkutano wa waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za TMA. 
 
Taarifa inatoa uchambuzi wa mwenendo wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo wa msimu wa mvua katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2019. Pia ushauri na tahadhari kwa wadau wa sekta mbali mbali wanaohitaji taarifa za hali ya hewa katika utekelezaji wa majukumu yao kama vile Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Uchukuzi na Mawasiliano, Nishati na Maji, Mamlaka za Miji, Afya pamoja na Menejimenti za Maafa. Muhtasari wa mwelekeo wa mvua hizo na athari zake ni kama ifuatavyo: Kusoma zaidi ingia humu http://www.meteo.go.tz/news/177 

TMA YAENDELEA KUWASHIRIKISHA WADAU WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA NCHINI KATIKA MAANDALIZI YA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA 2019

Washiriki wa warsha ya wadau wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwenye picha ya pamoja, walipokutana katika maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika,  mwezi Machi hadi Mei 2019




Lengo kuu la warsha hii ilikuwa ni  kuwashirikisha Wadau katika mchakato wa maandalizi ya utabiri wa mvua za msimu wa masika na kupata maoni na michango kuhusiana na tafsiri na matumizi sahihi ya  utabiri katika sekta husika. Aidha warsha hii pia ilikuwa ni fursa kwa Mamlaka ya Hali ya Hewa kuendelea kuwajengea uelewa kuhusiana na mifumo ya hali ya hewa, utabiri na umuhimu wa kuzingatia tarifa za hali ya hewa katika kupanga mipango ya kiuchumi na kijamii.

“Ni muhimu sana kuongeza uelewa na kuimarisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli zetu za kiuchumi na kijamii hasa katika kipindi ambapo dunia inakabiliwa na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa” alisema Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, kupitia hotuba yake ya ufunguzi iliyosomwa na Dkt. Ladislaus Chang’a, Mkurugenzi wa Utafiti na Matumizi ya huduma za hali ya hewa wakati akifungua warsha ya wadau wa huduma za hali ya hewa nchini uliofanyika tarehe 12 Februari 2019 katika ukumbi wa “Law School”.

Warsha hii ni mwendelezo wa jitihada za TMA za kuimarisha ushirikishwaji wa WADAU katika mchakato wa uandaaji wa utabiri na usambazaji wa tarifa za hali ya hewa kwa msimu wa mvua za MASIKA na VULI. Warsha hizi zinajumuisha wadau kutoka sekta mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, afya, maji, nishati, maafa, mipango, wanahabari, usafirishaji, ujenzi n.k

Aidha, katika hotuba yake, Dkt. Kijazi, aliwashukuru wafadhili wa warsha ambao ni Shirika la Hali ya Hewa Duniani-World Meteorological Organization (WMO) kwa kudhamini warsha hiyo kupitia programu ya Mfumo wa Kidunia wa Huduma za Hali ya Hewa - Global Framework for Climate Services (GFCS) ambao umewezesha kushirikisha wadau wengi zaidi pamoja Shirika la kimataifa la Chakula na Kilimo-Food and Agriculture Organization (FAO) kwa kuwezesha ushiriki wa wadau kutoka katika wilaya za Mvomero, Kilosa na Uyui.

Utabiri wa mvua za msimu wa masika unatarajiwa kutolewa rasmi tarehe 14 Machi 2019.

IMETOLEWA NA OFISI YA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...