Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeandaa mkutano
wa wadau mbalimbali kwa ajili ya msimu wa mvua za Vuli (Oktoba hadi
Desemba, 2018) ambao unalenga kupata maoni ya wadau jinsi utabiri wa
Msimu wa Mvua za Vuli utakavyoweza kutumika katika sekta mbalimbali za
kiuchumi na kijamii. Kauli mbiu ya mkutano huo ni “Ushirikishwaji wa
Wadau Katika Kuchochea Matumizi Ya Taarifa Za Hali Ya Hewa”.
Akizungumza
katika ufunguzi wa mkutano huo mgeni rasmi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Agnes Kijazi alisema kuwa lengo
kubwa la mkutano huo ni kuchochea matumizi ya taarifa za hali ya hewa
katika sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii hapa nchini.
‘lengo
kubwa la mkutano huu kama ilivyo katika kauli mbiu ni kuchochea
matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika sekta mbalimbali za kiuchumi
na kijamii, ambapo katika mkutano huu, mtapata fursa ya kuona utabiri wa
hali ya hewa wa msimu wa Oktoba hadi Disemba, 2018 na hivyo kuwa na
majadiliano yenye lengo la kuchangia juu ya athari zitakazopatikana
katika sekta zenu kutokana na utabiri huo na hatimaye kuandaa mbinu na
mipango ya kukabiliana na athari hizo’. Alisema Dkt.Kijazi.
Aidha
aliongezea kuwa mkutano huo ni sehemu ya kubadilishana uzoefu kati ya
wataalamu wa TMA, Sekta mbalimbali na Washirika wa Maendeleo hivyo basi
ni sehemu muhimu ya ushirikishwaji wa wadau katika kujenga na kuimarisha
utoaji na matumizi ya huduma za hali ya hewa katika jamii akisisitiza
kuwa kauli mbiu imechaguliwa ili kuakisi jitihada za Mamlaka katika
uandaaji na utoaji wa huduma shirikishi. Akifanunua umuhimu wa tarifa za
hali ya hewa katika kuchangia azma ya serikali ya kufikia uchumi wa
viwanda Dkt. Kijazi alisema huduma za hali ya hewa ni muhimu katika
uzalishaji wa mali ghafi za viwanda na utunzaji wa miundo mbinu ya
usafirishaji wa mali ghafi hizo pamoja na utunzaji wa miundo mbinu ya
viwanda vyenyewe. Aliwataka wadau kutumia huduma za hali ya hewa katika
sekta zao ili kumuunga mkono Mheshiwa Rais katika kufikia malengo hayo
ya uchumi wa viwanda.
Kwa
upande Wake mwakilishi wa mradi wa kilimo himilivu kutoka Shirika la
Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) Bw. Diomedes Kalisa alisema
kupitia mkutano huo wa wadau ni dhahiri malengo ya FAO ya kuboresha
mfumo wa utoaji taarifa za hali ya hewa yatafikiwa hususan katika kilimo
ili kubadilisha kilimo kutoka kilimo cha kujikimu kwenda kwenye kilimo
cha biashara katika kuboresha maisha ya wakulima na nchi yote katika
kufikia malengo ya uchumi wa viwanda.
Nao
wadau kutoka sekta mbali mbali wakijadili taarifa ya utabiri wa hali ya
hewa uliotolewa na TMA katika msimu wa Machi hadi Mei, 2018 ambao
usahihi wake ulifikia asilimia 96 waliipongeza Mamlaka kwa ongezeko hilo
la usahihi wa utabiri. Hata hivyo walizungumzia changamoto ya utabiri
kutowafikia wananchi wengi hasa wakulima na kuishauri TMA kuona
uwezekano wa kuwatumia maafisa ugani kuhakikisha wakulima wengi wanapata
taarifa za utabiri kwa wakati. Akijibu hoja hiyo Dkt. Agnes Kijazi
alisema TMA imejipanga kuihusisha Wizara husika ili kuona utaratibu
mzuri wa kutoa mafunzo kwa maafisa ugani na kuhakikisha wanapata utabiri
mara unapotolewa.
Mkutano
huo umefanyika tarehe 03 Septemba 2018 katika ukumbi wa mikutano wa
Taasis ya mafunzo ya uanasheri kwa vitendo Tanzania chini ya udhamini wa
TMA na FAO na kuwashirikisha wadau kutoka sekta mbalimbali zikiwemo
maji, Nishati, maafa, mazingira, kilimo,tawala za mikoa, afya, elimu,
Asasi zisizo za Kiserikali, wana habari na mashirika ya maendeleo ya
Kimataifa
IMETOLEWA NA KITENGO CHA UHUSIANO
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
|
Tupo pamoja
ReplyDelete