Tuesday, September 18, 2018

TANZANIA YAZINDUA PROGRAMU YA KIDUNIA YA HUDUMA ZA HALI YA HEWA (GFCS) AWAMU YA PILI.


Dar es Salaam 18/09/ 2018

Tanzania imezindua rasmi programu ya kidunia ya huduma za hali ya hewa kwa awamu ya pili, tarehe 18 Septemba 2018, katika ukumbi wa  Golden Jubilee Tower, Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization) kupitia ufadhili wa Serikali ya Norway imekuwa ikitekeleza Mfumo wa Kidunia wa Huduma za Hali ya Hewa “Global Framework for Climate Service-GFCS (2014-2016)”. Washirika wengine katika mradi huu hapa nchini ni Wizara ya Kilimo, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani – WFP, Shirika la Afya Duniani – WHO, Shirika la Msalaba Mwekundu Tanzania.

Utekelezaji wa programu ya GFCS hapa Tanzania ulianza mwezi Februari 2014 kwa warsha ya uzinduzi iliyojumuisha wadau wa masuala ya hali ya hewa wa ndani na nje ya nchi. Lengo kuu la warsha lilikuwa ni kukubaliana namna bora ya utekelezaji na usimamizi wa programu ambapo  mfumo wa utekelezaji na usimamizi uliundwa rasmi ikiwa ni pamoja na mapendekezo ya TANDREC kwasasa TADMAC kuwa msimamizi mkuu wa GFCS, na kuchagua rasmi wilaya za Kiteto na Longido kuwa maeneo ya majaribio ya utekelezaji wa programu sambamba na Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali ya Hewa “National Framework for Climate Services (NFCS)” uanze kutekelezwa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Akizindua rasmi programu hiyo, Katibu Mkuu Ofisi ya waziri Mkuu (Sera na Uratibu) Prof. faustin Kamuzora alisisitiza kuwa programu hii imekuja wakati muafaka kwa vile serikali imekuwa na jitihada za kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa, aidha alisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa program hiyo huhakikishe taarifa za hali ya hewa zinawafikia wananchi hususani wa maeneo ya vijinini kwa wakati na usahihi huku akiipongeza TMA kwa ongezeko la usahihi wa utabiri unaotolewa kwa kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Naye, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alimshukuru mgeni rasmi na wafadhili wa programu hiyo kwa ushirikiano wao huku akifafanua lengo la uzinduzi wa awamu ya pili ni kuanzishwa rasmi utekelezaji wa shughuli za program kwa awamu nyingine. Ikiwa na lengo la kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa watumiaji walio katika hatari ya kuathirika na hali ya hewa hasa hasa katika kukabiliana na maafa yatokanayo na hali mbaya ya hewa, usalama wa chakula na afya

Kwa upande wa wafadhili wa programu hiyo kupitia serikali ya Norway, mwakilishi kutoka WMO Bi. Erica Allis alisema kuwa WMO imeamua kuzindua awamu ya pili ya utekelezaji wa programu hiyo kutokana na mafanikio yaliyopatikana katika utekeleza wa awamu ya kwanza na uhitaji wa utekelezaji wa kina zaidi kama vile kufanyiwa kazi mahitaji ya mfumo wa taifa wa hali ya hewa, utoaji wa taarifa za hali ya hewa zenye ubora zaidi kwa maeneo madogo madogo na mafunzo kwa wataalamu ndani na nje sambamba na usambazaji kupitia mfumo wa simu za mkononi FARMSMS

Mwakilishi kutoka Norway aliongezea kwa kusema kuwa wanatambua uhitaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii  kwahiyo ni wakati muafaka kwa wadau wanaoshiriki katika utekelezaji wa programu hii kujifunza kutoka katika awamu ya kwanza na kufanya maboresho ya utekelezaji wake ili jamii ikanufaike zaidi na programu hii.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa na wadau mbali mbali kutoka wizara za serikali, mashirikia ya kimataifa, mashirika ya elimu, mashirika ya siyo ya kiserikali, taasisi za utafiti, wanahabari na wengine wengi.
Imetolewa:
Monica Mutoni,
Ofisi ya Uhusiano,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...