Saturday, December 15, 2018

COP24: TANZANIA YATUMIA FURSA KUHAMASISHA ONGEZEKO LA WATAALAM KUTOKA AFRIKA KATIKA SEKRETARIET YA SHIRIKA LA HALI YA HEWA DUNIANI (WMO)


Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inashiriki Mkutano wa 24 wa Mabadiliko ya Hali ya Hewa (Climate Change Conference 24) unaoendelea huko Katowice, Poland kuanzia tarehe 3 hadi 14 Desemba 2018.

Mkutano huo umewakutanisha wadau mbalimbali kutoka duniani kote wakiwemo viongozi wa nchi, mashirika ya kimataifa, taasisi za kiserikali na zisizo za kiserikali n.k. Ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mussa Sima

Prof. Petteri Taalas (wa pili kutoka kulia) Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization) katika picha ya pamoja na Mhe. Mboni Mhita (MB) (wa pili kutoka kushoto) na mjumbe wa bunge la  Pan-Africa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  Dkt. Agnes Kijazi na  Bw. Marcellin Kokou Nakpon(wa kwanza kushoto),  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Benin 

Kupitia mkutano huo, Mbunge wa Handeni Vijijini Mhe. Mboni Mhita na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi walipata fursa ya kuongea na Katibu Mkuu wa WMO na kujadili masuala mbali mbali yanayohusu ushiriki wa Taasisi za Hali ya Hewa za Afrika katika kutekeleza programu za WMO na misaada WMO inayoweza kutoa kuziwezesha taasisi hizo ikiwa pamoja na kuongeza wataalam kutoka Afrika katika Secretariat ya WMO.

Aidha mhe. Mboni aliiomba WMO kuendelea kuzisaidia nchi za Afrika kupata vifaa vya kisasa kulingana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa ili kufanikisha utoaji wa taarifa sahihi za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu.

Aliongezea kwa kutoa mfano wa umuhimu wa taarifa za hali ya hewa kwa jimbo lake, ambapo alielezea namna walivyo nufaika na kilimo cha mhogo (mazao yanayostahimili ukame) baada ya kupata utabiri wa msimu mvua kutoka TMA.

Kwa upande wa Dkt. Kijazi aliwashukuru WMO kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa TMA ikiwemo kufadhili baadhi ya miradi ya huduma za hali ya hewa nchini.

Thursday, December 13, 2018

TANZANIA YASHIRIKI MAJADILIANO YA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KWA USAFIRI WA ANGA KWA KUANGALIA FURSA NA CHANGAMOTO ZILIZOPO KATIKA AFRIKA.

Washiriki wa Mkutano wa Afrika wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Usafiri wa Anga (World Meteorological Organization African Conference on Meteorology for Aviation – ACMA-2018), tarehe 28 Novemba 2018, Saly, Senegal.

Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) kwa kushirikiana na Wadau limeandaaa mkutano wa Afrika kuhusu Utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Usalama wa Usafiri wa Anga (2018 African Conference on Meteorology for Aviation (ACMA-2018), uliofanyika Saly- Senegal.

Mkutano huo ulifanya majadiliano na kupeana uzoefu wa huduma za hali ya hewa kwa usafiri wa anga ili kuwa na uelewa wa pamoja wa fursa na changamoto zilizopo katika Afrika. Aidha, ulilenga kujua vipaumbele na vihatarishi vya utoaji wa huduma za hali ya hewa kuhusiana na mpango wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani ICAO Global Air Navigation Plan (GANP) and aviation System Block Upgrades (ASBU) methodology.

Vile vile, Tanzania ilipata nafasi ya kujadili kwa pamoja na wanachama wengine athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa upande wa usafiri wa anga hususan katika Afrika na kujua mahitaji ya wadau. Aidha,kufanyika kwa mkutano huo ni utekelezaji wa Azimio la Pili la Mkutano wa Nchi Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani(WMO) kanda ya Afrika (Resolution 2 of the sixteenth session of WMO Regional Association I - Africa) uliofanyika Praia, Cabo Verde Februari, 2015.

Makubaliano ya mkutano huo yatawasilishwa kwenye mkutano wa 17 ujulikanao kama seventeenth session of WMO Regional Association I unaotarajiwa kufanyika Cairo, Misri mwezi Februari, 2019.

Tanzania iliwakilishwa katika mkutano huo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) – Dkt. Agnes Kijazi pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri – Dkt. Hamza Kabelwa na Meneja wa kitengo cha kusimamia Viwango wa Ubora na Vihatarishi – Dkt Geofrid Chikojo. Mkutano huo pia ulihudhuriwa na wajumbe wengine wakiwemo kutoka Shirika la KImataifa la Usafiri wa Usalama wa Anga (ICAO), Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Taasisi ya Hali ya Hewa Uingereza (UK Met Office), Taasisi ya Hali ya Hewa Finland (FMI), Wakala wanaosimamia kutoa na Kudhibiti Usafiri wa Anga Nchi za Mangharibi (ASECNA)
Dkt. Agnes Kijazi mmoja wa washiriki akichangia mada kwenye Mkutano wa Afrika wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Usafiri wa Anga (World Meteorological Organization African Conference on Meteorology for Aviation – ACMA-2018), tarehe 28 Novemba 2018, Saly, Senegal.
Washiriki kutoka TMA wakipongeza jambo wakati wa Mkutano wa Afrika wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Usafiri wa Anga (World Meteorological Organization African Conference on Meteorology for Aviation – ACMA-2018), tarehe 28 Novemba 2018, Saly, Senegal.


Tuesday, December 11, 2018

NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA MAKAMU WA RAIS MUUNGANO NA MAZINGIRA MHE. MUSSA SIMA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA MABADILIKO YA TABIANCHI – POLAND

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima akisalimiana na Prof. Petteri Taalas Katibu Mkuu wa Shrika la Hali ya Hewa Duniani.  Naibu Waziri Sima anaongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 24 wa Nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Katowice Poland. Kushoto ni Dkt. Freddy Manyika Kaimu Mkurugenzi Msaidizi anayesshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima  (wa kwanza kutoka kushoto) wakijadiliana jambo na Prof. Petteri Taalas Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  Dkt. Agnes Kijazi ,Katowice Poland.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mussa Sima  (wa pili kutoka kushoto) katika picha ya pamoja na Prof. Petteri Taalas Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization), Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  Dkt. Agnes Kijazi na  Dkt. Freddy Manyika Kaimu Mkurugenzi Msaidizi anayesshughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais. mara baada ya kushuhudia WMO ikisaini Mkataba na Global Climate Fund wenye lengo la kuzisaidia taasis za hali ya hewa Duniani kushiriki katika utekelezaji wa makubaliano ya mabadiliko ya tabianchi.
Prof. Petteri Taalas Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (World Meteorological Organization) katika picha ya pamoja na Mhe. Mboni Mhita (MB) na mjumbe wa bunge la  Pan-Africa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania  Dkt. Agnes Kijazi na  Bw. Marcellin Kokou Nakpon,  Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Hali ya Hewa ya Benin akimwakilisha Rais wa RA1- Afrika baada ya kikao cha pamoja ( kati ya RA1-Afrika, Tanzania na WMO ) kilichojadili masuala mbali mbali yanayohusu Ushiriki wa Taasisi za hali ya hewa za Afrika katika kutekeleza programu za WMO na misaada WMO inayoweza kutoa kuziwezesha taasisi hizo ikiwa pamoja na kuongeza wataalam kutoka Afrika katika Secretariat ya WMO.

Monday, December 3, 2018

TAARIFA YA VIPINDI VYA HALI YA JOTO KALI

Meneja Kituo Kikuu cha Utabiri, Bw. Samuel Mbuya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuelezea ongezeko la joto,pembeni ni Bi. Monica Mutoni kutoka ofisi ya Uhusiano-TMA 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inatoa taarifa na ufafanuzi kwa jamii juu ya hali ya ongezekeo la joto katika baadhi ya maeneo hapa nchini.

Kwa kawaida kipindi cha miezi ya Oktoba hadi Machi kila mwaka jua la utosi linakuwa katika maeneo ya kizio cha kusini mwa dunia. Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zilizopo katika kizio cha kusini, huwa na hali ya joto kali katika maeneo mengi ikilinganishwa na miezi mingine. Hapa nchini, vipindi vya jua la utosi vinafikia kilele  kati ya mwishoni mwa mwezi Novemba na mwezi Disemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea kusini (Tropiki ya Kaprikoni) na  hali hiyo hujirudia tena mwezi Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea kaskazini (Tropiki ya Kansa). Jua la utosi huambatana na hali ya Joto kali kwa sababu kipindi hicho ndipo uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine. Hali hii hushuhudiwa zaidi kunapokuwepo na upungufu wa mvua ambazo zingesaidia katika kupunguza hali ya joto  katika kipindi husika.

Wastani wa joto katika mwezi Novemba na Disemba ni  nyuzi joto 31.5  kwa mikoa ya Dar es Salaam,  Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba. Hata hivyo, mpaka  kufika mwishoni mwa Novemba 2018 joto limeshafika nyuzi joto 34. Katika baadhi ya maeneo hapa nchini ikiwemo mikoa ya Kilimanjaro, Arusha,  Manyara, Morogoro, Dar es salaam, Pwani pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba ambapo msimu wa mvua za Vuli unaendelea  kukumbwa na mtawanyiko hafifu wa mvua hali ya fukuto inachangia  katika  hali ya joto japo vipimo vya nyuzi joto katika baadhi ya maeneo hayo ni vya wastani.


Vipindi hivi vya joto kali vinatarajiwa kupungua  kadiri mtawanyiko wa mvua za vuli utakavyoimarika  katika  mwezi Disemba 2018. Hata hivyo ikizingatiwa kuwa  hali ya joto inatarajiwa  kujirudia tena mnamo mwezi Februari 2019, wakati wa kipindi cha pili cha jua la utosi.  Aidha, taarifa za mwenendo wa joto, zinaendelea kutolewa katika utabiri wa kila siku na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hivyo  tunatoa wito kwa wananchi kuendelea kufuatilia taarifa hizo na kuchukua hatua stahiki  kila inapobidi.


Thursday, November 29, 2018

TMS YAWAPONGEZA DKT.BURUHANI NYENZI KWA KUCHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA JUKWAA LA KIMATAIFA LA WATAALAMU WA HALI YA HEWA (IFMS) NA DKT. AGNES KIJAZI KWA KUTEULIWA NA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA (UN) KUWA MJUMBE WA JOPO LA WATAALAM KUMI (10-MEMBER GROUP).




Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzania Meteorological Society-TMS) kimewapongeza Dkt. Buruhani Nyenzi ambaye pia ni rais wa chama hicho kwa kuchaguliwa kuwa makamu rais wa Jukwaa la Kimataifa la Wataalamu wa hali ya hewa ( International Forum of Meteorological Societies- IFMS) na Dk. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mjumbe wa Jopo la wataalam kumi (10-member Group) lenye jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu namna ambavyo sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) zinavyoweza kutumika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya umoja huo (Sustainable Development Goals(SDGs).

Pongezi hizo zilitolewa katika mkutano wa TMS uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa kujumuisha wanachama wa TMS kutoka maeneo mbali mbali nchini. Makamu wa rais wa TMS Dkt. Clavery Tungaraza kutoka chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na Katibu wa TMS Dkt.Ladislaus Chang'a kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa pamoja walisema mafanikio hayo ni mafanikio ya TMS kwani Dkt. Nyenzi na Dkt.Kijazi ni wanachama wa TMS.

Tunampongeza sana rais wa Umoja wetu Dkt. Nyenzi kwa kuchaguliwa kuwa makamu wa rais wa IFMS na Dkt. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo la wataalam kumi (10) kuunda kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja huo, tunatambua nafasi hizi ni fahari kwa wana TMS wote kwani ni fursa kwa TMS  kuitangaza nchi yetu kimataifa ‘alisema Dkt. Tungaraza’

Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwashukuru sana wanachama wote kwa pongezi na kusisitiza ushirikiano ili aweze kuipeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa. Jukwaa lile ni la kimataifa hivyo mtanzania kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa jukwaa (forum) hilo ni jambo la kujivunia sisi kama wana TMS na nchi yetu kwa ujumla. Akipokea pongezi hizo Dkt. Kijazi aliwashukuru wanachama na kufafanua kwamba wao kama wana sayansi mawazo yao ni muhimu katika kumuwezesha kutekeleza jukumu hilo kubwa la kimataifa. Uteuzi huu ni fahari kwa TMS na nchi yetu kwa ujumla hasa ikizingatiwa kwamba katika kundi la watu kumi tu kwa dunia nzima Tanzania nayo inatajwa ‘alisema Dkt. Kijazi.’

Wakati huo huo wanachuo waliomaliza na kufanya vizuri kwa masomo ya elimu ya shahada ya sayansi ya hali ya hewa (Bsc. Meteorology) kwa mwaka 2017 Bi. Aisha Nassor (mwanafunzi bora wa jumla), Bi. Leila Muhoma na Bw. Kekazuri Elly walipongezwa kwa jitihada zao na kupatiwa zawadi ya cheti na fedha taslim. Akikabidhi zawadi hizo Dkt. Kijazi alisema anafurahishwa kuona wanawake wanaongoza katika mafunzo hayo ya BSc Meteorology yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwajulisha wanachama kwamba TMS itaendelea kuwapongeza wanafunzi wanaofanya vizuri kwa lengo la kuchangia katika kuendeleza taaluma ya hali ya hewa hapa nchini.

Imeandaliwa na;
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA)

Monday, November 26, 2018

TMA YAZINDUA PROGRAMU MPYA YA KISASA YA KUSAMBAZA UTABIRI WA KILA SIKU WA HALI YAHEWA KWENYE TELEVISHENI (LUNINGA)



26/11/2018; DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imezindua rasmi programu mpya ya usambazaji wa utabiri wa kila siku wa hali ya hewa kwa njia ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya kidigitali ya kisasa “Full HD” katika mkutano na vyombo vya habari, Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza Dar es Salaam. 

Akizindua rasmi programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alivishukuru vyombo vya habari hapa nchini kwa kushirikiana na Mamlaka katika kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa jamii pia alisisitiza lengo la Mamlaka kuboresha ubora wa huduma zake kwa jamii kwa kufuata maoni yao.

‘Napenda kuvishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano mnaotupatia katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na maoni yenu kuhusu uboreshaji wa huduma zetu, Mamlaka imekuwa sikivu na kufanyia kazi maoni ambayo mmekuwa mkiyatoa’.

Mamlaka imekuwa ikiboresha huduma zake kwa jamii ili kukidhi matakwa ya watumiaji  na miongoni mwa matakwa hayo ni pamoja na kuwa na muonekano wa ‘graphics’ zenye mvuto katika utabiri wa kila siku unaotolewa na televisheni mbalimbali za habari hapa nchini. 

‘TMA inatambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuboresha utangazaji wa njia ya televisheni ambapo kwa sasa imeshaingia katika urushaji kwa njia ya kidigitali. Aidha TMA ikiwa ni mmoja wa wadau wanaotumia vyombo vya habari hususan televisheni  katika kufikisha taarifa zake kwa jamii imeona pia ni muhimu kuboresha miundombinu yake ili kuendana na mabadiliko hayo’ alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza ambayo kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) waliisaidia TMA kupata ‘software’ hiyo ya kisasa (High Definition) na pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa TMA.
Kutokana na huduma hizo za usambazaji zilizoboreshwa Dkt. Kijazi aliviomba vyombo vyote vya habari vinavyotoa taarifa kwa jamii kupitia Televisheni kushirikiana na TMA ili kusambaza utabiri wa kila siku wa hali ya hewa. Alisema utabiri wa kila siku ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao pia kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo wote tushirikiane kulijenga Taifa letu.


Thursday, November 22, 2018

VIONGOZI TUGHE WATAKIWA KUWA VIELELEZO VYA UADILIFU KWENYE MAENEO YA KAZI


Halmashauri ya TUGHE ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na menejiment ya TMA wamejumuika katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TMA makao makuu,Ubungo Plaza tarehe 22 Novemba 2018.

Katika kikao hicho, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt.Agnes Kijazi aliwataka viongozi wa TUGHE kuwa vielelezo vya uadilifu kwenye maeneo yao ya kazi.

Aliongezea kuwa ni vyema viongozi  wa TUGHE na menejiment ya TMA kuweka vipaumbele vya ufanisi wa kazi ili kufanikisha maendeleo ya nchi kupitia huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA

Wakati huo huo alisisitiza haki iende sambamba na wajibu kwa kuzingatia utendaji kazi wa pamoja (team work)

Kwa upande wa TUGHE katibu wake,bw.Benjamin Bikulamchi alishukuru Menejiment ya TMA kwa ushirikiano uliopo baina yao pamoja na kutoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi

Kikao hicho cha siku moja kilijadili masuala mbalimbali kwa manufaa ya Mamlaka kwa ujumla
Halmashauri ya TUGHE katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi na baadhi ya viongozi wa TMA
Halmashauri ya TUGHE katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa halmashauri hiyo wanaotarajiwa kustaafu
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao hicho


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...