Mamlaka ha Hali ya Hewa
Tanzania kwa kushirikiana na kituo cha kimataifa cha utafiti kilichoko Marekani
“International Research Institute (IRI) imezindua mfumo utakao wawezesha
watumiaji wa huduma za hali ya hewa kupata huduma hizo kwa urahisi kupitia tovuti ya Mamlaka (www.meteo.go.tz).
Akizindua mfumo huo
Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Mamlaka Dkt. Buruhani Nyenzi aliitaka Mamlaka
ya Hali ya Hewa kuongeza ufanisi
katika utoaji wa huduma za hali ya hewa.
Aidha, Dkt Nyenzi aliipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa jitihada
zake za kushirikiana na wataalam kutoka nchi mbalimbali ambazo ni wanachama wa
Shirika la Hali ya Hewa Duniani katika kuboresha huduma za hali ya hewa hapa
nchini. Mwenyekiti huyo wa Bodi ya
Ushauri ya TMA alikishukuru kituo cha kimataifa cha utafiti kilichoko Marekani
(IRI) kwa msaada waliotoa hata kuiwezesha TMA kukamilisha mfumo huo na kufikia
hatua ya kuzinduliwa rasmi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa
TMA, Dkt. Agnes Kijazi alitoa msisitizo kwa wadau kuzingatia matumizi sahihi ya taarifa za hali
ya hewa ili kuongeza tija na ufanisi katika shughuli za kiuchumi na kijamii na
pia kuweza kukabiliana na majanga yatokanayo na hali mbaya ya hewa. Dkt. Kijazi
aliwashukuru kituo cha kimataifa cha utafiti (IRI) kutoka Marekani kwa
kushirikiana na TMA kwa kipindi cha miaka mitatu katika kuandaa mfumo huo.
Vilevile aliwashukuru wadhamini wa uzinduzi wa mfumo huo ambao ni DFID kupitia
chuo kikuu cha Columbia kilichoko Marekani.
Uzinduzi huo ulifanyika katika Ukumbi wa
Blue pearl tarehe 18 Desemba 2015 nakushirikisha wadau mbalimbali kutoka Wizara
na Taasisi za Serikali pamoja na asasi za kiraia.
IMETOLEWA NA: MONICA MUTONI, AFISA UHUSIANO,
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA.
No comments:
Post a Comment