Sunday, December 28, 2025

HALI YA MVUA KUBWA NCHINI

 HALI YA MVUA KUBWA NCHINI


Dar es Salaam, 28 Desemba, 2025:
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inapenda kutoa taarifa ya mwenendo wa Mvua Kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali hapa nchini. 

Mnamo tarehe 26 hadi 27 Desemba, 2025 Mamlaka iliendelea kutoa Tahadhari ya vipindi vya Mvua Kubwa katika maeneo mengi nchini kuanzia tarehe 26 hadi 29 Desemba, 2025. Kwa mujibu wa Tahadhari hiyo maeneo yaliyotarajiwa kuathirika na vipindi hivi vya mvua kubwa ni pamoja na Mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Mbeya, Songwe, Iringa, Njombe, Dodoma, Singida, Songea, Morogoro, Lindi, Mtwara, Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, Pwani (ikijumisha Kisiwa cha Mafia) pamoja na Visiwa vya Unguja na Pemba. 

Kuanzia usiku wa kuamkia leo hadi hivi sasa maeneo mengi nchini yameendelea kupata vipindi vya Mvua Kubwa zikiambatana na upepo mkali na hivyo kusababisha uharibifu wa mali na miundombinu katika baadhi ya maeneo hapa nchini. Hadi kufikia saa 3:00 kamili asubuhi ya leo viwango vya mvua kubwa vinavyozidi milimita 50 ndani ya saa 24 vilipimwa katika vituo vya Same (milimita 94.5), Morogoro (milimita 58.6) na Tabora (milimita 55.4). Aidha, viwango vya mvua vilivyopimwa katika vituo vingine ni pamoja na Hombolo (milimita 49.5), Kibaha (milimita 43.6), Dodoma (milimita 36.6) na Iringa (milimita 35.6). 

Hadi muda huu tumepokea taarifa kuwa mvua hizo zimesababisha athari katika miundombinu ya reli ya zamani ya MGR kwa kuathiri madajara katika eneo la Kidete, Wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro na Gulwe Wilaya   Dodoma; kusababisha hitilafu za umeme wa TANESCO pamoja na umeme wa SGR; na pia Barabara kuu ya Morogoro - Iringa eneo la Mama Marashi - Mikumi kumetokea maporomoko ya mawe na tope kurundikana barabarani.

Mvua hizo zimesababisha miundombinu na shughuli za usafiri wa abiria na shehena kwa ujumla kuathirika, hususan kupitia Reli ya SGR.

Kwa ujumla Serikali inaendelea na juhudi za kurejesha hali hiyo katika hali yake ya kawaida. 

Mifumo ya hali ya hewa iliyopo kwa sasa inaonesha kuendelea kuimarika kwa Ukanda Mvua na hivyo kuendelea kusababisha vipindi vya Mvua Kubwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Mara, Simiyu, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa, Njombe, Morogoro, Ruvuma, Lindi na Mtwara kwa siku ya kesho tarehe 29 Desemba, 2025. 

USHAURI: Wananchi wanashauriwa kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam katika sekta husika ili kujikinga na athari zinazoweza kujitokeza.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) inaendelea kufuatilia mwenendo wa mifumo ya mifumo ya hali ya hewa hapa nchini na itaendelea kutoa taarifa mara kwa mara kila inapobidi.
 


No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...