Sunday, August 31, 2025

DKT. LADISLAUS CHANG’A ASHIRIKI KATIKA MKUTANO WA 6 WA MAWAZIRI NA MAMLAKA ZA MAZINGIRA WA ASIA NA PASIFIKI

 




Nadi, Fiji – 29 Agosti 2025

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Sayansi ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (IPCC), Dkt. Ladislaus Chang’a, kwa mwaliko wa Programu ya Umoja wa Mataifa uratibu wa Mazingira (UNEP) ameshiriki kikamilifu katika Mkutano wa 6 wa Mawaziri na Mamlaka za Mazingira wa Asia na Pasifiki (6th AP Forum) uliofanyika kuanzia tarehe 26–29 Agosti 2025 Jijini Nadi, Fiji. Mkutano huo uliandaliwa kwa pamoja na Serikali ya Fiji na UNEP ukiwa na kaulimbiu “Kutafuta Suluhisho Endelevu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi Duniani”.

Sambamba na mkutano huo, Dkt. Chang’a alikuwa na vikao mbalimbali na waheshimiwa na taasisi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kikao na Mhe. Rupa B. K., Waziri wa Serikali ya Nepal, Wizara ya Misitu na Mazingira, ambapo alimpatia taarifa kuhusu mpango kazi wa IPCC unaotekelezwa hadi mwaka 2029. Mazungumzo hayo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuboresha sera za mazingira. Mhe. Rupa alishukuru na kupongeza sana kazi kubwa inayofanywa na IPCC.

Aidha, Dkt. Chang’a alishiriki na kuratibu kikao cha ngazi ya Mawaziri kuhusu Mfumo wa tahadhari za majanga ikiwa ni pamoja na yale yanayosababishwa na hali ya hewa. Kikao hiki cha Waheshimiwa Mawaziri wa Asia na Pasifiki kilikuwa na wazungumzaji (panelists) wakiwemo: Mhe. Thoriq Ibrahim, Waziri wa Utalii na Mazingira wa Maldives; Mhe. Bi. Mona Ainu’u, Waziri wa Rasilimali Asili wa Niue; Mhe. Dkt. Maina Vakafua Talia, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira wa Tuvalu; Bi. Fleur Downard, Mkurugenzi wa Masuala ya Mazingira ya Kimataifa na Kitengo cha Umoja wa Mataifa, Wizara ya Mabadiliko ya Tabianchi, Nishati, Mazingira na Maji, wa Australia; na Bw. Sefanaia Nawadra, Mkurugenzi Mkuu, Sekretarieti ya Programu ya Mazingira kanda ya Pasifiki (Pacific Regional Environment Programme-SPREP).

Kikao hicho kiliangazia umuhimu wa mifumo ya tahadhari za majanga (multi-hazard early warning systems-MHEWS) kama mojawapo ya hatua bora zinazotekelezeka katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi, kwa lengo la kulinda maisha na mazingira”.

Mkutano huu wa 6 wa Waheshimiwa Mawaziri wa Asia na Pasifiki wenye dhamana ya sekta ya mazingira ulikuwa pia jukwaa muhimu kwa makundi mbalimbali katika ukanda huo wawakilisha serikali zao, mashirika ya kikanda, vijana, sekta binafsi na wadau ambapo mchango na maoni yao vitasaidia katika maandalizi ya Mkutano wa 7 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (Seventh Session of the United Nations Environment Assembly (UNEA-7) unaotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2025 jijini Nairobi, Kenya.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...