Tuesday, October 25, 2022

WASHINDI WA TUZO YA MWAHABARI BORA WA HABARI ZA HALI YA HEWA 2022 WAPONGEZWA

 





















Dar es Salaam; Tarehe 25 Oktoba, 2022;

"Natoa pongezi zangu za kipekee kwa washindi wa Tuzo ya mwanahabari bora wa mwaka wa habari za hali ya hewa Tanzania 2022 pamoja na kuwapa hamasa wanahabari wengine kuendelea kufanya kazi bora zaidi na kuziwasilisha taarifa hizo ili ziweze kutambuliwa na Mamlaka na kuwa sehemu ya  mchakato wa Tuzo hii katika wakati ujao”. Alizungumza hayo Dkt. Nyenzi wakati akifungua hafla ya utoaji tuzo ya mwanahabari bora wa mwaka wa habari za Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania (TMA), 2022 iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano katika hoteli ya Tiffany Diamonds, Dar es Salaam, Tarehe 25 Oktoba 2022.

Dkt. Nyenzi alianza kwa kukabidhi Tuzo hizo za Mwanahabari bora, ambapo mshindi aliyepewa tuzo ya jumla alikuwa ni Irene Mark kutoka gazeti la Jamvi la habari na blog ya habari mseto, mshindi wa upande wa magazetini alikuwa Irene Mark kutoka gazeti la Jamvi la habari, mshindi wa upande wa Luninga na redio alikuwa Mussa Kharid kutoka Kiss FM, na mshindi wa upande wa mitandao ya kijamii alikuwa Noel Lukanuga kutoka Uhondo TV.

Aidha, Dkt. Nyenzi aliongezea kwa kuwapongeza wanahabari na vyombo vyote vya habari kwa kuendelea kushirikiana na TMA katika usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa jamii pamoja na kuipongeza TMA kwa kuendeleza ushirikiano huo uliosababisha jamii kupata taarifa kwa wakati na kujilinda au kupunguza athari mbaya za hali ya hewa sambamba na kuijengea jamii uwezo wa kutumia taarifa hizo kwa maendeleo yao ya kiuchumi na kijamii.

Ndugu Mbaraka Islam nguli wa habari hapa nchini ambaye ni mhariri gazeti la Raia Mwema  aliwakumbusha wanahabari kufuata vigezo vilivyoainishwa na Mamlaka na kuwa wabunifu pale wanapopata taarifa kutoka TMA kwa kuhusisha taarifa hizo na shughuli za kijamii kutoka sekta mbalimbali ili taarifa zao ziwe na tija kwa jamii.

Kabla ya hafla hiyo ya Tuzo kwa wanahabari bora, Mamlaka ilipata muda wa kujadiliana na wanahabari kupitia warsha ya wanahabari iliyofanyika hotelini hapo kwa lengo la kutoa uelewa wa pamoja kuhusu mwelekeo wa mvua za msimu kwa kipindi cha mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 unaotarajiwa kutolewa rasmi katika ukumbi wa TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo plaza tarehe 26 Oktoba 2022.

Kupitia warsha hiyo yenye kauli mbiu “Matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa kwa maendeleo endelevu”, wanahabari wametakiwa kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na kutafuta, kupata na kuwasilisha ufafanuzi na maelezo ya ziada ya kisekta kutoka kwa wataalam ili taarifa sahihi ziweze kufikia jamii kwa ukamilifu

Aidha, wanahabari wamekumbushwa kuendelea kuwa mabalozi wazuri wa TMA kuelezea na kusisitiza umuhimu wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa jamii katika shughuli zao za kila siku

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...