Dar es Salaam; Tarehe 24
Oktoba, 2022;
Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania (TMA) imekutana na wadau kutoka sekta mbalimbali ili kujadili utabiri
wa mvua za msimu unaotarajiwa kuanza mwezi Novemba 2022 hadi Aprili 2023 kwa
maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka ambayo ni Tabora, KigomaKusini,Katavi,Mbeya,Rukwa,Songwe,Njombe,Iringa,Ruvuma,Mtwara,Lindi,Dodoma,
singida na Morogoro Kusini . Katika ufunguzi wa kikao hicho kilichofanyika
katika ukumbi wa Tiffany Diamond Hotels uliopo jijini Dar es Salam, Tarehe 24
Oktoba 2022, mgeni rasmi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani
Nyenzi amehimiza wadau kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa ambazo ni
chachu katika kujenga uchumi wa viwanda hapa nchini.
“Taarifa za hali ya hewa
zinalenga katika kusaidia nchi kufikia malengo ya mpango wa Taifa katika
kujenga uchumi wa viwanda kwa kusaidia kupunguza athari zitokanazo na majanga
yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa ili kusaidia kulinda mafanikio ya
uwekezaji katika miundo mbinu ya uchukuzi ikiwemo barabara, reli na vyombo vya
usafiri majini”. Alisema Dkt.Nyenzi
Dkt. Nyenzi aliongezea kwa
kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.
Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea
kuijengea uwezo TMA, hatua ambayo imeisaidia kuboresha utabiri wa hali ya hewa
na kusaidia Taifa katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya
hewa ikiwemo upungufu wa mvua, mafuriko, joto na baridi kali pale zitakapojitokeza.
Kwa upande wa Mkurugenzi
Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
Dkt. Agnes Kijazi ameelezea namna serikali ilivyoendelea kuijengea uwezo
Mamlaka kwa kuboresha miundo mbinu yake ambayo kwa njia moja au nyingine
inasaidia kukuza uchumi wa nchi.
Dkt. Kijazi amesema mtandao
wa rada upo katika hatua za mwisho ili kukamilika, huku vituo vya hali ya hewa
vinavyojiendesha vyenyewe vikizidi kuongezwa na mbiundombinu ya uchambuzi wa
taarifa za hali ya hewa ikiendelea kuboreshwa, Aidha mitambo ya mawasiliano
imeendelea kuboreshwa ili taarifa hizi ziweze kuwafikia wadau kwa wakati, na
pia wataalam wameendelea kujengewa uwezo kupitia mafunzo mbalimbali na hivyo
kuwapa uwezo wa kufungasha taarifa zilizoboreshwa.
Aidha, Dkt. Kijazi
aliwashukuru ILRI kutoka Nairobi ambao
wamefadhili kwa sehemu kikao hicho cha wadau.
Aidha, wadau mbalimbali wa hali ya hewa walielezea namna wanavyozitumia taarifa za hali ya hewa katika kujiandaa na kukabiliana na hali ya hewa tarajiwa katika sekta zao, ambapo mdau kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ndugu Emmanuel Kato (Afisa Malisho), alielezea namna sekta hiyo inavyojiandaa katika kukabiliana na hali ya hewa tarajiwa na maandalizi hayo ni pamoja na kuchimba visima virefu vya maji na ujenzi wa mabwawa katika kupunguza au kuepusha migogoro ya wafugaji katika kutafuta maji kwaajili ya mifugo pale upungufu wa mvua unapojitokeza.
Kwa upande wa mdau wa kilimo Juma Makandi, alisema kupitia taarifa za TMA timu ya wataalam imeweza kutembelea maeneo yenye dalili za upungufu wa chakula na kwa sasa inaendelea na tathmini na ripoti itatolewa baada ya kazi kukamilika, naye, mdau wa kutoka TANESCO James Kirahuka alisema umuhimu wa taarifa za hali ya hewa katika uzalishaji wa nishati ya umeme nchini ni pamoja na kusaidia katika kutoa tahadhari za hali mbaya ya hewa ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme kama vile kuanguka kwa nguzo za umeme.
No comments:
Post a Comment