Dar es Salaam, Tarehe 26/10/2022
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa mvua za msimu kwa maeneo yanayopata mvua mara moja kwa mwaka. Maeneo hayo yakijumuisha mikoa ya (Tabora, Kigoma Kusini, Katavi, Mbeya, Rukwa, Soingwe,Njombe, Iringa, Ruvuma na Morogoro Kusini) katika kipindi cha miezi ya Novemba, 2022 hadi Aprili, 2023.
Wakati akitoa utabiri huo kwa niaba ya Mkurugenzi Wakati wa akitoa utabiri huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Hamza Kabelwa ambaye pia ni Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri, TMA alisema katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza, hivyo sekta mbalimbali zinatakiwa kujipanga na kukabiliana na hali hiyo.
“Upungufu mkubwa wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi yanayopata mvua za Msimu na kuathiri ukuaji wa mazao na upatikanaji wa malisho kwa ajili ya mifugo. Vilevile, kina cha maji katika mito na mabwawa kinatarajiwa kupungua na kuathiri upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali kama vile umwagiliaji na uzalishaji wa nishati. Mamlaka zinashauriwa kuhakikisha vyanzo vya maji vinatunzwa pamoja na kuweka miundombinu ya uvunaji maji sambamba na kuandaa na kutekeleza mipango mkakati ya kuhimiza kilimo himilivu”. Alifafanua Dkt. Kabelwa.
Alisema, “Katika nusu ya kwanza ya msimu (Novemba, 2022 – Januari, 2023) vipindi virefu vya ukavu vinatarajiwa kujitokeza hata hivyo, ongezeko la mvua linatarajiwa katika nusu ya pili ya msimu (Februari- Aprili, 2023). Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa mwezi Mei, 2023 katika maeneo mengi.Maeneo ya mikoa ya Singida na Dodoma mvua za Msimu zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa katika wiki ya pili ya mwezi Januari, 2023“.Alizungumza Dkt. Kabelwa
Mvua za chini ya wastani hadi wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi, Singida, Dodoma, Ruvuma, Lindi na Mtwara. Aidha, mvua za wastani hadi chini ya wastani zinatarajiwa katika baadhi ya maeneo ya mikoa ya Njombe, Rukwa, Songwe, Mbeya, Iringa na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Akizingumzia kuhusu Msimu wa Vuli kwa miezi ya Oktoba hadi Disemba 2022 katika maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka, alisema Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani (ikijumuisha kisiwa cha Mafia) pamoja na Zanzibar (visiwa vya Unguja na Pemba), msimu unatarajiwa kuendelea kama utabiri ulivyotolewa tarehe 2 Septemba, 2022, ambapo maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani. Aidha, mvua za nje ya msimu zinatarajiwa katika mwezi Januari, 2023.
Kwa maelezo kamili kuhusu utabiri huu tembelea http://www.meteo.go.tz/
No comments:
Post a Comment