Dar es Salaam; Tarehe 13
Septemba, 2022;
Serikali imewahakikishia wadau
wa hali ya hewa nchini kuwa itaendelea kuboresha miundombinu na watalaam wake
ili kuhakikisha usahihi wa taarifa za hali ya hewa unaongezeka na kusaidia
kwenye maendeleo na ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa kufungua
rasmi Kongamano la 15 la Wadau wa
Satelaiti za Hali ya Hewa wa Shirika la EUMETSAT Barani Afrika, katika Ukumbi wa Mikutano wa
Julius Nyerere, Dar es Salaam,Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. Atupele Fred
Mwakibete (MB) ambaye alimuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Mhe. Kassim Majaliwa, amesema kuwa masuala ya hali ya hewa ni
mtambuka na yanagusa sekta zote hivyo kongamano hilo litakuwa muarobaini wa
changamoto zinazokabili sekta hizo.
“Kwa namna ya pekee
niwashukuru EUMETSAT kwa kuamua kufanyia Mkutano huu wa kimataifa nchini
Tanzania, ni imani yangu kuwa siku hizi nne (4) mtachakata changamoto zote na
kuja na suluhu ili sekta zote zipate ahueni katika utekelezaji wa mipango yake
kwani taarifa za hali ya hewa ni muhimu sana” amesema Naibu Waziri Mwakibete.
Naibu Waziri Mwakibete
aliendelea kwa kusema kupitia teknolojia ya satelaiti, huduma za hali ya hewa
zinaendelea kuboreshwa na hivyo kuchangia katika kukabiliana na changamoto za
mabadiliko ya hali ya hewa yanayoikumba Afrika na Dunia kwa ujumla. Aidha, ameitaka
Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini (TMA) kuendelea kutumia njia mbalimbali
kuifikishia jamii taarifa za hali ya hewa kwa wakati.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TMA na
Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt Agnes
Kijazi amesema Kongamano hilo litajadili kwa pamoja changamoto mbalimbali na
kuja na mikakati mahususi ya kuhakikisha taarifa za hali zinapatikana kwa
urahisi na kwa haraka sambamba na kukidhi matakwa ya watumiaji wa taarifa hizo.
Vile vile, alieleza kuwa Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano hili ni heshima
kubwa kwa nchi na kuonesha mafanikio makubwa katika sekta ya hali ya hewa
nchini pamoja na ushirikiano ulipo baina ya nchi za Afrika na nje ya Afrika.
“Kupitia makongamano haya nchi
za Afrika zimeendelea kunufaika na uboreshaji wa utabiri wa hali ya hewa na
hivyo kuchangia katika kupanga mipango ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii”.
Alisema Dkt. Kijazi
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la EUMETSAT, Dkt. Phil Evans amesema mipango ya shirika hilo ni
kurusha satelaiti ya kisasa zaidi (Meteosat third Generation – MTG) mwishoni
mwa mwaka huu ili kuboresha uangazi na utoaji wa taarifa za hali ya hewa
hususani katika ukanda wa Afrika.
Kongamano la 15 la Wadau wa
Satelaiti za Hali ya Hewa wa Shirika la EUMETSAT barani Afrika linalofanyika
jijini Dar es Salaam kuanzia tarehe 12 hadi 16 Septemba 2022, limewakutanisha
Wadau wa Masuala ya Hali ya hewa kutoka nchi 59 Barani Afrika na nje ya Afrika wakiwemo
Wakurugenzi wa Mamlaka za Hali ya Hewa katika Nchi za Afrika, Kamisheni ya Umoja
wa Afrika, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Umoja wa Ulaya
(EU).
EUMETSAT ni miongoni mwa
Taasisi za kimataifa zinazoshirikiana na WMO katika shughuli za uangazi wa hali
ya hewa kwa kutumia teknolojia ya satelaiti za hali ya hewa kwa nchi wanachama
wa WMO.
No comments:
Post a Comment