Wednesday, April 27, 2022

TMA YAJIPANGA KUIMARISHA USHIRIKIANO NA WADAU MBALIMBALI WA HALI YA HEWA ZANZIBAR

Mkurugenzi wa TMA - Zanzibar, Ndg. Mohammed Ngwali, akizungumza na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari kwenye maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.










Matukio mbalimbali kwa picha wakati wataalam wa TMA wakitoa elimu ya hali ya hewa kwa wadau kutoka sekta mbalimbali waliotembelea banda la TMA, kupitia maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.  


Mkurugenzi wa TMA - Zanzibar, Ndg. Mohammed Ngwali, akiwa kwenye picha ya pamoja na wataalam wa hali ya hewa kupitia maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22 Aprili - 26 Mei 2022.

 

Zanzibar, Tarehe 26/04/2022

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ni Taasisi ya Muungano ambayo inafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria Tanzania Bara na Zanzibar ambapo huduma tunazotoa zina umuhimu mkubwa kwa jamii kwa sababu zimelenga katika kuokoa maisha ya watu na mali zao pamoja na kukuza uchumi wa nchi. Mamlaka imejipanga kudumisha ushirikiano na wadau mbali mbali wa hali ya hewa hapa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuimarisha usalama kwa jamii na kuinua uchumi kupitia huduma za hali ya hewa kwa sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi”. Aliyasema hayo Mkurugenzi wa TMA – Zanzibar, Ndugu Mohamed Ngwali wakati wa maonesho ya miaka 58 ya Muungano wa Tanzania yanayofanyika katika viwanja vya Maisala, Mjini Unguja, kuanzia tarehe 22/04 – 06/05/2022

Aidha, Ndugu Ngwali alisisitiza kuwa zipo njia mbali mbali ambazo wadau na wananchi wanaweza kutumia kupata taarifa za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na tovuti ya TMA, luninga, redio, magazeti, mitandao ya kijamii na pia wanaweza kufika katika Ofisi za Mamlaka ya Hali ya Hewa zilizopo Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Amani Abeid Karume, Zanzibar na Uwanja wa ndege wa Pemba.

Sambamba na hilo wataalam wa hali ya hewa wa TMA wameendelea kutoa elimu kwa wananchi na wadau wa sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, uvuvi, usafiri wa anga na maji ili kuongeza uelewa wa matumizi ya taarifa za hali ya hewa kwa usahihi na kuongeza uzalishaji kupitia sekta zao. Vilevile elimu hii husaidia katika kuepusha majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa sambamba na kutambua njia zitumikazo na Mamlaka katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa wadau na wananchi kwa ujumla.

Katika manesho haya, wageni mbalimbali wameweza kutembelea banda la TMA na wameonesha kufurahishwa na huduma zinazotolewa na Mamlaka. Aidha, TMA inaendelea kutekeleza jukumu hili kwa umakini wa hali ya juu na kuongeza ushirikiano zaidi na jamii ili kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata na anatambua umuhimu wa huduma hizi muhimu za hali ya hewa na kuzitumia kwa usahihi na kwa wakati ili kuepuka majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa yanayoweza kujitokeza.

Friday, April 22, 2022

MHE. PROF. MBARAWA ATOA WITO KWA WADAU WANAOTUMIA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KIBIASHARA KUTIMIZA TAKWA LA KISHERIA LA KUCHANGIA HUDUMA HIZO.



 




Dodoma, Tarehe 21/04/2022:

Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhe. Profesa Makame Mnyaa Mbarawa (Mb) ametoa wito kwa wadau wanaotumia huduma za hali ya hewa kibiashara kuhakikisha wanatimiza takwa la kisheria la kuchangia huduma hizo. Alizungumza hayo alipokuwa akifungua rasmi mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), uliofanyika katika ukumbi wa Kilimani Land Mark – Dodoma, Tarehe 21/04/2022

“Kuchangia huduma za hali ya hewa ni suala la kisheria hivyo kila mdau hana budi kulitekeleza. Wakati serikali inatekeleza jukumu hilo, natoa wito pia kwa wadau wanaotumia huduma hizo kibiashara kuhakikisha wanatimiza takwa hilo la kisheria la kuchangia huduma za hali ya hewa ili ziweze kuboreshwa zaidi”.  Alisisitiza Prof. Mbarawa.

Katika hatua nyingine mheshimiwa Prof. Mbarawa aliwapongeza wadau wote walio onesha ushirikiano kwa kujitokeza kusajili vituo vyao na kuchangia gharama za utoaji huduma mahususi zinazotolewa katika sekta zao na hivyo kukidhi matakwa ya Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 pamoja na kanuni zake. Aliwaelekeza TMA kuongeza juhudi na kuhakikisha sekta zote ambazo hawajaanza kuchangia huduma za hali ya hewa wanachangia kama sheria inavyoelekeza. Prof. Mbarawa aliwapongeza TMA kwa kuiwakilisha vyema nchi katika shughuli za hali ya hewa kimataifa na kuendelea kushikilia cheti cha ubora cha ISO 9001-2015.

Katika kutatua changamoto zinazoikabili TMA, Prof. Mbarawa aliahidi Wizara kuendelea kuiwezesha Mamlaka kupitia fedha za Miradi ya Maendeleo ili kuhakikisha miundo mbinu ya hali ya hewa inaboreshwa. Aliongeza kusema  maslahi ya watumishi pia yataboreshwa hivyo aliwataka wataalam wa hali ya hewa kuendelea kufanya kazi kwa bidii wakati serikali inashughulikia uboreshaji wa maslahi. 

Kwa upande mwingine Mwenyekiti wa Bodi ya TMA, Dkt. Buruhani Nyenzi aliishukuru Serikali kwa kuendelea kuwajengea uwezo watumishi wa TMA na kuwapatia mazingira bora ya kazi yanayowawezesha kutekeleza vyema jukumu lao la kuiwakilisha nchi katika masuala ya hali ya hewa kikanda na kimataifa. Hali iliyopelekea kuendelea kuitambulisha Tanzania katika nyanja za hali ya hewa kimataifa na kumuwezesha Makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) pamoja na wataalam wa hali ya hewa walioko katika vikosi kazi vya Shirika hilo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alielezea dhumuni kuu la Baraza hilo la Wafanyakazi kuwa ni kupitia bajeti ya Mamlaka ya mwaka 2022/2023 na kufanya tathmini ya utendaji wa Mamlaka itakayosaidia kuongeza ubora na ufanisi katika utoaji wa huduma kwa umma kwa lengo la kupunguza athari za mabadiliko ya hali ya hewa na tabia nchi zinazoikabili Dunia. Aidha, aliishukuru serikali kwa kuboresha miundo mbinu ya hali ya hewa nchini na kuwajengea uwezo wataalam hali iliyoiwezesha TMA kukosa dosari yoyote wakati wa ukaguzi wa kimataifa uliofanyika Desemba, 2021 na hivyo kuendelea kumiliki cheti cha ubora cha ISO.


Wednesday, April 13, 2022

TMA YATOA MREJEO WA UTABIRI WA MVUA ZA MSIMU WA MASIKA ULIOTOLEWA RASMI FEBRUARI 2022


 

Dar es Salaam, Tarehe 13/04/2022:

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa MASIKA 2022, uliotolewa  rasmi Februari 2022 kwa maeneo yanayopata mvua za msimu mara mbili kwa mwaka, ikijumuisha maeneo ya Ukanda wa Ziwa Victoria, Nyanda za juu Kaskazini Mashariki pamoja na Pwani ya Kaskazini. Katika mrejeo huo TMA imetoa uchambuzi wa mwenendo mzima wa mifumo ya hali ya hewa na mwelekeo uliohuishwa wa msimu wa nvua katika kipindi cha Machi hadi Mei 2022 pamoja na ushauri kwa wadau kutoka sekta mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Dkt. Agnes Kijazi ameelezea sababu zilizosababisha kuwepo kwa vipindi virefu vya ukavu hususan kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki kuwa ni pamoja na kujitokeza kwa vimbunga katika Bahari ya Hindi pamoja na mabadiliko ya muda mfupi ya  joto la bahari.

“Kumekuwa na vipindi virefu vya ukavu vilivyojitokeza katika kipindi cha mwezi Machi, 2022 hususan kwa maneo ya pwani ya Kaskazini na Nyanda za juu Kaskazini Mashariki ambapo maeneo hayo yalipata vipindi virefu vya ukavu, hali iliyosababishwa na matukio ya vimbunga katika Bahari ya Hindi eneo la Rasi ya Msumbiji, pamoja na kujitokeza kwa mabadliko ya muda mfupi ya joto la bahari kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.”, Alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi alisisitiza kuwa pamoja na maeneo mengi yanayopata mvua za msimu mara mbili kwa mwaka kutarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadi wastani katika msimu huu wa mvua za MASIKA 2022, watumiaji wa utabiri wanatakiwa kuzingatia kuwa matukio ya vipindi vya mvua kubwa yanaweza kujitokeza katika maeneo hayo sambamba na kuwataka kupata ushauri wa kitaalam kutoka kwa maafisa wa sekta zao.

Aidha katika hotuba yake mapema asubuhi alipokuwa akifungua warsha ya wadau iliyotangulia kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari, Dkt. Kijazi  aliwataka wadau kutumia mrejeo mpya wa utabiri wa msimu wa mvua za Masika katika mipango yao ya maendeleo hapa nchini.

 Kwa taarifa zaidi tembelea: https://www.meteo.go.tz/weather_forecasts/seasonal-weather-forecast

TANZANIA YAATHIRIKA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI


 



Dar es Salaam Tarehe 12/04/2022.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekutana na waandishi wa habari kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi katika mifumo ya hali ya hewa ikiwa ni maandalizi ya kurejea utabiri wa MASIKA uliotolewa Februari 2022. Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi, amesema mifumo ya hali ya hali ya hewa imebadilika kutokana na mabadiliko ya tabia nchi yaliyopelekea kubadilika kwa mwenendo mzima wa mvua za msimu wa MASIKA 2022. Aliyazungumza hayo alipokuwa akifungua warsha ya wanahabari iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Makao Makuu ya TMA, Ghorofa ya tatu, Ubungo Plaza, tarehe 12/04/2022.  

“Tanzania tumeanza kuziona athari za mabadiliko ya tabia nchi, katika mifumo ya hali ya hewa hasa kubadilika kwa joto la bahari ambalo kwa kawaida halibadiliki kwa haraka kutokana na tabia ya maji kutunza joto lake kwa muda mrefu.” Alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi alisema kuongezeka kwa joto duniani (global warming) kunasababisha kuyeyuka kwa barafu zilizoko katika ncha za dunia na hivyo kuongeza vina vya bahari katika maeneo mbalimbali duniani ikiwa Pamoja na kubadilika kwa hali ya joto la bahari na hivyo kuathiri mifumo ya hali ya hewa.

Aidha Dkt. Zewdu Segele ambaye ni mtaalam wa masuala ya hali hewa kutoka kituo cha utabiri na matumizi ya hali hewa (ICPAC) alisema, ICPAC imetoa mrejeo wa utabiri wake wa Machi – Mei ambao iliutoa mwezi Februari. Dkt. Zewdu alisema mifumo ya awali ilionyesha uwepo wa mvua za juu ya wastani katika nchi za pembe ya Afrika ikiwemo Tanzania, lakini baada ya mifumo kubadilika nchi hizo sasa zitapata mvua za chini ya wastani.

Dkt. Zewdu aliongeza kusema utabiri unaotolewa na ICPAC ni wa maeneo makubwa hivyo nchi wanachama wana jukumu la kuandaa utabiri wa maeneo madogo madogo katika nchi zao.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inatarajia kutoa rasmi mrejeo wa utabiri wa mvua za msimu wa Masika (MAM) 2022 Tarehe 13/04/2022.


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...