Dar es Salaam, Tarehe
28/12/2022.
Tunapoelekea katika sherehe za kumaliza mwaka 2022 na
kuukaribisha mwaka 2023, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitembelea kituo
cha afya cha Tandale, Tarehe 28/12/2022 na kutoa msaada wa vifaa tiba ambavyo
viliwasilishwa rasmi na Kaimu Meneja wa
Masoko wa TMA Bi Monica Mutoni kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt.
Ladislaus Chang’a.
Akizungungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Bi. Monica
Mutoni alisema msaada wa vifaa tiba hivyo ni matokeo ya Kongamano la 15 la EUMETSAT lililofanyika mwezi Septemba 2022 kwa
lengo la kutoa huduma ya kwanza kwa wadau wa Kongamano hilo kutoka nchi zote za
Afrika na baadhi ya nchi za nje ya Afrika.
“vifaa hivyo vilikabidhiwa TMA na wataalamu wa afya kutoka
hospitali ya Taifa ya Muhimbili, vipo takribani 25, hivyo basi kwa upendo wetu
kwenu na kwa kuwa moja ya majukumu ya TMA ni kurudisha kwa jamii, Kaimu
Mkurugenzi Mkuu ametuagiza kutoa msaada wa hivi ili kuweza kusaidia jamii na
wahitaji wote wanaotumia kituo hiki”. Alisisitiza Bi. Monica Mutoni
Aidha, vifaa hivyo vilipokelewa na Kaimu Mganga Mfawidhi wa
kituo cha afya cha Tandale, Dkt. Merina Kulwa, ambaye aliishukuru TMA na kusema
kuwa msaada huo utasaidia katika kuboresha utoaji huduma kituoni hapo.