Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya (Wanne kutoka kulia) katika picha ya pamoja na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Prof. Petteri Taalas. Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO (wa kwanza kushoto) na Wakurugenzi wa Mazingira kutoka Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk na Dkt. Andrew Komba kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais.
Glasgow; Tarehe 07/11/2021
Tanzania imeendelea kushiriki katika Mkutano wa 26 wa nchi wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa na Tabianchi (COP26) unaoendelea Glasgow, Uingereza, ambapo viongozi mbalimbali wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar akiwemo mheshimiwa Rais na mawaziri wameshiriki. Kwa upande wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliwakilishwa na Mkurugenzi Mkuu na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi pamoja na Wataalamu wa TMA.
Katika hatua za kuhakikisha huduma za hali ya hewa zinaendelea kuboreshwa kwa manufaa ya nchi, Mhe. Dkt. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar alipata fursa ya kuzungumza na washiriki wakati wa tukio la uzinduzi wa programu ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani ya “Systematic Observation Financing Facility (SOFF)” ambapo alielezea umuhimu wa program hiyo kwa nchi zinazoendelea pamoja na Tanzania ambazo uchumi wake kwa asilimia kubwa hutegemea zaidi kilimo.
Aidha katika hatua nyingine, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Selemani Jafo pamoja na Mhe. Dkt. Saada Mkuya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais – Serikali ya Mapinduzi Zanzibar walifanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Prof. Petteri Taalas ambapo walishukuru ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Shirika hilo kupitia utekelezaji wa programu mbalimbali ikiwemo changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Kwa upande wake Prof. Taalas aliwashukuru Waheshimiwa Mawaziri kwa kuwezesha ushiriki wa TMA katika utekelezaji wa programu hizo za WMO ikiwa ni pamoja na kazi anayofanya Dkt. Agnes Kijazi katika nafasi yake kama Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO. Ujumbe wa Tanzania ulitambulishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa WMO Dkt. Agnes Kijazi.
Kwa upande wa TMA, Dkt. Kijazi alikuwa miongoni mwa washiriki katika jopo (High level Panelist) la kujadili umuhimu wa sayansi na taarifa za hali ya hewa kwa ajili ya kupanga mipango na kutoa maamuzi katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi ambazo hutegemea sana hali ya hewa, “High-level launch of the Climate Science Information for Climate Action Initiative”, vile vile, TMA ilishiriki mazungumzo yenye lengo la kuboresha ushirikiano kati yake na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Denmark (DMI). Kati ya maeneo ya uboreshaji wa ushirikiano huo ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa; uendelezaji wa wataalamu wa hali ya hewa; utafiti na utoaji wa tahadhari kwa ajili ya uratibu na kupunguza athari za maafa yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa.
TMA pia ilifanya mazungumzo na Taasisi ya Hali ya Hewa ya Burundi kuhusiana na mwendelezo wa ushirikiano uliyopo kati ya taasis hizo mbili ikiwa Pamoja na eneo la mafunzo ambapo Burundi wanatarajiwa kuleta wataalamu wao kusoma katika Chuo cha Hali ya Hewa cha Taifa (NMTC) kilichopo Mkoani Kigoma.
Mkutano huo wa COP26 unajadili namna ya kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi na athari za mabadiliko hayo katika sekta mbali mbali za kijamii na kiuchumi. Katika mikutano ya COP, taasisi za hali ya hewa zimepewa jukumu la kufuatilia masuala yanayohusu tafiti za kisayansi na masuala ya uangazi ‘Research and Systematic Observation’, pamoja na masuala ya teknolojia ya hali ya hewa.
No comments:
Post a Comment