|
“Mchango wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our
Climate and Weather)
|
Dar
es Salaam, Tarehe 23/03/2021
Leo,
tarehe 23 Machi, 2021 ni Siku ya Hali ya Hewa Duniani ikiwa ni kumbukizi ya
kusainiwa kwa Mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO)
mnamo tarehe 23 Machi, 1950. Siku hii imefikiwa wakati Tanzania ikiwa katika
maombolezo ya Kitaifa kufuatia kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli
aliyefariki tarehe 17 Machi, 2021. Hivyo kwa upande wa Tanzania maadhimisho
haya hayatafanyika Kitaifa kama ilivyo kawaida bali siku hii inatumika kukumbuka
mchango wa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha sekta
na huduma za hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Bodi,
menejimenti na watumishi wa TMA tunatoa salamu za pole kwa Watanzania wote kwa
kuondekewa na Kiongozi wetu Mahiri, Mchapakazi na Mzalendo wa kweli.
Miongoni
mwa michango muhimu katika sekta ya hali ya hewa katika kipindi cha Uongozi wa
Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ni;
1.
Kutungwa kwa Sheria ya
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Namba 2 ya mwaka 2019 iliyoibadili TMA kutoka
Wakala wa Hali ya Hewa Tanzania na kuwa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania. Mabadiliko
hayo yameipa TMA mamlaka ya kisheria ya kuendelea kutekeleza jukumu la kutoa
huduma za hali ya hewa na kuongezewa jukumu la kudhibiti na kuratibu shughuli za
hali ya hewa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha, sheria hiyo inaipa
TMA mamlaka ya kisheria ya kukusanya mapato yanayotokana na matumizi ya huduma
za hali ya hewa kwa shughuli za kibiashara. Hivyo, kuiwezesha sekta ya hali ya
hewa kuwa bora zaidi na kuongeza mchango wake katika kuinua uchumi wa Nchi katika kipindi hiki
ambacho dunia inakabiliwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
2.
Mchango mwingine muhimu uliofanywa
na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika sekta ya Hali ya
Hewa ni uboreshaji wa miundombinu ya ufuatiliaji na upimaji wa hali ya hewa
ikiwa ni pamoja na mtandao wa RADA saba za hali ya hewa ili kuona hali ya hewa
ya eneo lote la nchi yetu. RADA tatu zilizofungwa Dar es Salaam, Mtwara na
Mwanza tayari zinafanya kazi. RADA nyingine nne ambazo ziko katika mpango huu na tayari ziko katika hatua za matengenezo na ununuzi
zitafungwa katika mikoa ya Kigoma, Dodoma, Kilimanjaro na Songwe. RADA tano kati ya saba zitahusika katika
uangazi wa eneo la bahari na maziwa makuu yanayozunguka nchi yetu. Maeneo hayo
ni pamoja na pwani ya Bahari ya Hindi (Dar es Salaam na Mtwara), Ziwa Viktoria
(Mwanza), Ziwa Tanganyika (Kigoma) na Ziwa Nyasa (Songwe).
3.
Hayati Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli ameboresha miundombinu ya vifaa vya hali ya hewa
kuwa vya kisasa zaidi. Vifaa vinavyotumia
zebaki vimeondolewa na kufungwa vifaa vya kisasa visivyotumia zebaki ikiwa ni utekelezaji
wa mkataba wa Minamata unaoelekeza kusitisha matumizi ya zebaki duniani.
4.
Hayati Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli pia aliweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa
programu za Kidunia na Kikanda za masuala ya hali ya hewa. Programu hizo ni
pamoja na programu ya WMO ya Kidunia ya utoaji wa huduma za hali ya hewa “Global Framework for Climate Services
Adaptation Programme in Africa (GFCS APA)”; na programu ya “Weather and Climate Information Services
for Africa (WISER)”, pamoja na uandaaji wa Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za
Hali ya Hewa “National Framework for
Climate Services(NFCS)”. Utekelezaji wa programu hizi umechangia kuboresha
huduma za hali ya hewa ikiwa ni pamoja na huduma kwa watumiaji wa bahari na
maziwa makuu. Kwa mfano, program ya “WISER” ilisaidia kuundwa kwa mfumo wa
utoaji huduma za hali mbaya ya hewa “Multi-Hazard
Early Warning System (MHEWS)”, ambao umejumuisha wadau wote muhimu,
ikiwa ni pamoja na Mfumo wa Kitaifa wa Utoaji wa Taarifa “National
Early Warning System (NEWS)” ukihusisha Ofisi ya Taifa ya Uratibu wa
Maafa “National Disaster Management Office (DMO)”. Mfumo huo ulifanyiwa
majaribio katika tukio la kimbunga Kenneth
kilichotokea mwezi Aprili, 2019 ambapo ulionekana kuwa ni mfumo wenye
ufanisi mkubwa katika uratibu wa matukio ya vimbunga.
5.
Aidha, Hayati Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli ameweka kipaombele katika kujenga uwezo wa rasilimali
watu katika sekta ya hali ya hewa kwa kuongeza wataalam bingwa wa hali ya hewa (Meteorologists)
ambapo mwaka 2015 alipoingia madarakani TMA ilikuwa na wataalam bingwa sitini
na saba (67) na mwaka huu 2021 wapo wataalam bingwa 131. Aidha, wataalam hao wamepatiwa
mafunzo mbali mbali ya kuwaongezea weledi na hivyo kuongeza umahiri wao katika
kutoa utabiri wa hali ya hewa.
6.
Uboreshaji huo alioufanya Hayati
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wa miundo mbinu ya hali ya hewa pamoja
na ongezeko la wataalam bingwa umeiwezesha TMA kupata cheti cha kimataifa cha
ubora katika utoaji wa huduma za hali ya
hewa kwa usalama wa usafiri wa anga yaani ISO 9001:2015 certification. Aidha,
uboreshaji huo umewezesha kuongezeka kwa viwango vya usahihi wa utabiri wa hali
ya hewa kutoka asilimia 78 mwaka 2015 hadi kufikia kati ya asilimia 82 na 96
mwaka 2020.
7.
Hayati Mheshimiwa Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli ameweka mazingira
wezeshi yaliyoiwezesha TMA kutekeleza
jukumu lake la kuiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika masuala ya
hali ya hewa kikanda na kimataifa kwa ufanisi na mafanikio makubwa. Aidha, Hayati
Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliidhinisha
jina la Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi kugombea nafasi ya makamu wa
tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani (WMO) ambapo alichaguliwa katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka
minne kuanzia 2019 hadi 2023. Dkt.
Agnes Kijazi ni mwanamke wa kwanza kutoka Bara la Afrika na nchi
zinazoendelea kuchaguliwa kwenye nafasi hiyo kubwa ya uongozi wa juu kabisa katika
Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
8. Aidha, kipindi cha utawala wa Hayati
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli taarifa za kisayansi za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini
zimeboreshwa ambapo TMA inatoa jarida la mwenendo wa hali ya hewa nchini
(Statement on the Status of Tanzania Climate). Jarida hili limesheheni taarifa
muhimu ambazo zinasaidia katika mipango ya muda mrefu sambamba na utekelezaji
wa dira ya nchi ya uchumi wa viwanda.
9. Uboreshaji
wa huduma za hali ya hewa zitolewazo na TMA alioufanya Hayati Mheshimiwa Dkt.
Magufuli umeimarisha uwezo wa Serikali katika kupunguza madhara ya majanga
yanayosababishwa na matukio ya hali mbaya ya hewa. Aidha,
uboresha wa huduma za hali ya hewa umeimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na
athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Kutokana na mafanikio haya na mengine
mengi katika sekta ya hali ya hewa, matumizi ya taarifa za hali ya hewa
zitolewazo na TMA yameongezeka katika kupanga shughuli za kiuchumi na kijamii
hapa nchini.
10. Sambamba na mafanikio
yaliyofikiwa, maboresho zaidi yanahitajika hususan kuongeza na kuboresha
miundombinu ya vifaa vya upimaji na uchambuzi wa data za hali ya hewa; ufungashaji
na elimu juu ya matumizi sahihi ya taarifa.
Katika kutekeleza hilo, TMA itaendelea kushirikiana na wadau wote katika
kuhakikisha matumizi sahihi ya huduma za hali ya hewa. Aidha, jitihada za
Serikali pekee haziwezi kutatua changamoto zote za masuala ya hali ya hewa
zinazoikabili jamii. Hivyo, jitihada zinahitajika pia kutoka kwa watumiaji na
washirika wa huduma za hali ya hewa katika kuziboresha na kuhakikisha
zinatumika ipasavyo.
Katika
Siku hii ya Hali ya Hewa Duniani kwa mwaka 2021, TMA inauenzi mchango mkubwa wa
Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alioutoa katika sekta ya hali ya hewa hapa
nchini, na pia kikanda na kimataifa. Aidha, TMA itaendelea kuchapa kazi kwa bidii
na kuwahudumia Watanzania wote ili kumuenzi shujaa wa uboreshaji wa sekta ya
hali ya hewa Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuhakikisha
uboreshaji alioufanya unakuwa endelevu. Pia, tunatoa wito kwa wadau wote wa
huduma za hali ya hewa, ikiwa ni pamoja na watumiaji wa bahari, wavuvi, wakazi
wa maeneo ya fukwe na Mamlaka zinazohusika kuendelea kuzifuatilia na kuzitumia
ipasavyo taarifa zitolewazo na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) katika mipango
ya shughuli za kiuchumi na kijamii, na kuchukua hatua stahiki ambazo zitasaidia
kupunguza madhara ya majanga na hatimaye kuongeza kasi ya ujenzi na maendeleo
ya Taifa letu. TMA inakaribisha mashirikiano katika utekelezaji wa Mfumo wa
Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate Services) na
programu zingine za kuboresha huduma za hali ya hewa nchini ambazo Hayati Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli ametuachia, wadau wote tuzitekeleze kwa ufanisi
ikiwa ni sehemu ya kumuenzi shujaa huyu wa uboreshaji wa sekta ya hali ya hewa
hapa nchini.
Maadhimisho
ya Siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD) kwa mwaka 2021 yanaongozwa na kaulimbiu
ya “Mchango
wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather). Kaulimbiu hii inalenga kufafanua umuhimu
na uhusiano kati ya bahari, hali ya hewa, na athari zake kwa shughuli za
kichumi na kijamii za kila siku.
Mchango
wa bahari katika hali ya hewa umetokana na uhusiano mkubwa uliopo kati ya
bahari na anga ambapo umesababisha kuona ulazima wa kuelewa kwa kina tabia na
mwenendo wa bahari ili kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa usahihi. Moja ya
uhusiano muhimu kati ya bahari na anga, ni uwezo wa bahari kusharabu nishati ya
jua inayofanikiwa kufika katika uso wa Dunia kwa kiasi kikubwa sana ambapo
sehemu ya nishati hii huvukiza maji ya bahari na kutengeneza mawingu mengi na
mazito, vimbunga na kusababisha mvua baharini na nchi kavu.
Utekelezaji
wa programu mbalimbali za huduma za uangazi katika bahari umerahisisha
upatikanaji wa data za hali ya bahari. Hivyo, uboreshaji wa miundombinu ya
upimaji na ufuatiliaji wa hali ya anga na bahari, pamoja na uelewa wa kutosha
wa mahusiano yaliyopo, unasaidia wanasayansi kutambua na kutabiri kwa urahisi zaidi
viashiria muhimu vya bahari kwa hali ya hewa kama vile “El Niño” na “La Niña”
hali ambazo huathiri hali ya hewa ya maeneo mengi na makubwa duniani ikiwa ni
pamoja na Tanzania.
Tanzania
ni miongoni mwa Nchi 193 Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ambao
leo duniani kote wanaikumbuka siku hii muhimu ya kuanzishwa kwa Shirika la Hali
ya Hewa Dunia mwaka 1950. Aidha, Katibu Mkuu wa Shirika la Hali ya Hewa
Duniani Prof. Petteri Taalas ametuma Salaam za Pole kwa Serikali, wana TMA na
wananchi wote wa Tanzania kufuatia kifo cha Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli ambapo alisema Jumuia ya kimataifa imempoteza kiongozi mahiri aliyesimamia
Amani na Maendeleo ya nchi yake. Wana TMA tuna ikumbuka siku hii tukiwa
tumejawa na majonzi na simanzi kwa kuondokewa na shujaa wa uboreshaji wa huduma
za hali ya hewa hapa nchini.
Maono
ya Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa Sekta ya Hali ya Hewa
Nchini yataendelea kuishi na Mchango wake Tutauenzi Daima.
PUMZIKA
KWA AMANI SHUJAAWA UBORESHAJI WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA.
“Mchango
wa bahari katika hali ya hewa”-(The Ocean, Our Climate and Weather)”