Tuesday, September 8, 2020

VULI 2020: MAENEO MENGI YA NCHI YANATARAJIWA KUPATA MVUA ZA CHINI YA WASTANI HADI WASTANI.

 



Dar es Salaam, 08/09/2020;

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa utabiri wa msimu wa mvua za VULI 2020 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari, Mkurugenzi Mkuu na Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi alisema maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ni Mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba, Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma (wilaya za Kibondo, Kakonko na Kasulu).

Dkt Kijazi alisema, mvua za Vuli kwa mwaka huu zinatarajiwa kuwa za chini ya wastani hadi wastani na zitakazoambatana na vipindi virefu vya ukavu katika maeneo mengi ya nchi, aidha mvua za Vuli zinatarajiwa kuanza kwa kuchelewa kati ya wiki ya pili na ya tatu ya mwezi Novemba, 2020 katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, na ukanda wa pwani ya Kaskazini pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Morogoro.

Akizungumza kuhusu athari zinazotarajiwa kujitokeza, Dkt. Kijazi alisema upungufu wa unyevunyevu katika udongo unatarajiwa kujitokeza katika maeneo mengi, magonjwa ya mlipuko kutokana upungufu wa maji safi na salama, upungufu wa malisho na maji unaweza kujitokeza hivyo uwezekano wa kutokea migogoro kati ya wakulima na wafugaji unatarajiwa.

“Matukio ya moto katika mapori na misitu yanategemewa kutokea, mamlaka husika zinashauriwa kupanga mikakati mahsusi ya kukabiliana na hali hiyo, nitoe angalizo,ingawaje maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za chini ya wastani hadiwastani, izingatiwe kuwa matukio ya vipindi vifupi vya mvua kubwa yanaweza yakajitokeza katika maeneo machache”. Aliongezea Dkt. Kijazi

Utabiri wa msimu wa mvua za vuli 2020 unapatikana katika ofisi zote za TMA nchini pamoja na mitandao ya mawasiliano kama vile TMA online TV, tovuti, blog, facebook na Instagram.

Kwa taarifa zaidi tembelea; http://www.meteo.go.tz/uploads/weathers/forecast/en/1599567307-Seasonal%20Rainfall%20Outlook%20OND%202020%20(English%20Version)-FINAL.pdf

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...