Dar es Salaam, Tarehe; 03/09/2020.
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeweka msisitizo wa matumizi ya taarifa mahususi za hali ya hewa kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda. Hayo yalizungumzwa wakati wa ufunguzi wa mkutano wa wadau wa utabiri wa mvua za vuli 2020, uliofanyika katika Ukumbi wa Taasisi ya Mafunzo ya Uanasheria kwa Vitendo Tanzania (The Law School of Tanzania), Dar es Salaam.
“Taarifa za hali ya hewa zinalenga kusaidia katika kufikia malengo ya Mpango wa Taifa katika kujenga uchumi wa viwanda. Kwa mfano, katika eneo la uzalishaji mazao ya chakula na biashara, Nishati na maji; huduma za hali ya hewa zikitumika ipasavyo tutajihakikishia upatikanaji wa malighafi na nishati kwa viwanda vyetu”. Alizungumza Dkt. Nyenzi, Mgeni Rasmi katika mkutano huo na Mwenyekiti wa Bodi ya TMA.
“Ni matumaini yangu kuwa mkutano wa leo utakuwa ni hatua muhimu kuelekea mashirikiano ya kisekta kati ya Mamlaka ya Hali ya Hewa na watumiaji wa huduma za hali ya hewa na hivyo kuongeza matumizi ya huduma hizo kwa maendeleo endelevu. Kila mmoja wetu ana mchango na jukumu la kufuatilia kwa karibu, kuelewa na kukabiliana na hali ya hewa ilivyo leo na itakavyokuwa siku zijazo. Tuendelee kuelimishana kupitia njia zote stahiki kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na namna ya kukabiliana nayo na wakati huohuo tukiendelea kutekeleza sera ambazo zitatusaidia sasa na siku zijazo”. Aliongeza Dkt. Nyenzi.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambaye pia ni Makamu wa tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alisisitiza kuwa kuna uhusiano mkubwa wa hali ya hewa na uzalishaji wa malighafi kwa ajili ya viwanda pamoja na ujenzi wa viwandavyenyewe. Hivyo alieleza umuhimu wa kutumia taarifa za hali ya hewa katika uchumi wa viwanda. Alieleza kwamba Mamlaka imeanzisha huduma za utoaji taarifa mahususi kwa matumizi katika sekta mbalimbali. Maandalizi ya taarifa hizo yanahusisha ushirikiano na wadau husika, ambapo wadau katika sekta ya utalii na madini wameanza kunufaika.
“Mamlaka imedhamiria kuendelea kuandaa taarifa za aina hiyo kwa kushirikiana na wadau wa sekta nyingine. Natoa wito kwa wadau mliopo hapa tuendelee kushirikiana katika kuandaa taarifa katika sekta zenu. Wakati huo huo tukizingatia utekelezaji wa sheria Na. 2 ya 2019 iliyoanzisha Mamlaka ya Hali ya Hewa ambayo imeweka bayana mahitaji ya wadau wa sekta mbalimbali ”. Alisema Dkt. Kijazi
Naye mdau kutoka Wizara ya Kilimo Bi. Halima Kwikwega aliungana na wadau wengine kuipongeza TMA kwa kazi nzuri ya kutoa utabiri ambao kwa kiasi kikubwa umekuwa na uhalisia wa hali ya juu, vilelvile alieleza kufurahishwa na maandalizi yanayofanywa na TMA katika kuandaa mikutano kama hii na kuahidi kuendelea kutumia utabiri unaotolewa kwa manufaa ya sekta ya kilimo na nchi kwa ujumla. Alisema ni muhimu kuzingatia kuwa kilimo ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu, akitolea mfano utabiri wa msimu uliopita uliwasaidia wakulima kupata mavuno yakutosha na hivyo kuongeza tija katika uchumi wa Taifa letu.
Wadau wengine kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Wizara ya Kilimo – Zanzibar, TANESCO, Vyombo vya Habari, TPDC, Red Cross, Mifugo na Uvuvi, Shirika la Chakula Duniani (FAO) n.k waliipongeza TMA kwa utabiri wa uhakika ambao umeongeza tija katika sekta zao.
Lengo la mkutano huo wa kikazi ni kuongeza mchango wa wataalam juu ya matumizi ya taarifa za hali ya hewa na athari zinazotarajiwa katika sekta mbalimbali, kukusanya maoni na ushauri kutoka katika makundi ya wadau yanayotumia taarifa za hali ya hewa pamoja na kuongeza uelewa wa wadau na jamii kwa ujumla juu ya tafsiri bora na sahihi za utabiri wa mvua za vuli kwa sekta mbalimbali. Utabiri wa mvua za vuli utatolewa rasmi tarehe 8/9/2020.
No comments:
Post a Comment