Dar es Salaam: Tarehe 20 Agosti 2020
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya Sekta ya Hali ya Hewa ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) – “SADC Sub-Sectoral Committee on Meteorology (SADC SCOM)”, Dkt. Agnes Kijazi, amesisitiza nchi wanachama kuweka nguvu zaidi katika mpango wa kuhakikisha zinapata cheti cha ubora wa kimataifa kwenye utoaji wa huduma za hali ya hewa katika sekta ya usafiri wa anga (QMS, ISO 9001:2015 ).
Dkt. Kijazi alizungumza hayo katika mkutano wa Kamati hiyo uliofanyika tarehe 20 na 21 Agosti 2020 kwa njia ya mtandao alipokuwa akitoa taarifa fupi ya utekelezaji wa shughuli za sekta ya hali ya hewa katika kipindi cha Uenyekiti wake katika sekta hiyo kuanzia Agosti 2019 hadi Agosti 2020.
”Mpaka hivi sasa ni nchi saba (7) tu kati ya kumi na sita (16) za SADC ambazo zimepata cheti cha ubora wa kimataifa katika utoaji wa huduma za hali ya hewa kwenye sekta ya usafiri wa anga. Nchi hizo ni pamoja na Tanzania, Afrika ya Kusini, Angola, Botswana, Mauritius, Msumbiji na Zimbabwe. Kwa kuwa hili ni moja ya malengo tuliyojiwekea na yanayoendana na matakwa ya utoaji wa huduma za hali ya hewa Kimataifa, ni vyema tuweke msisitizo zaidi kuhakikisha kuwa nchi zote za SADC zinafikia lengo hili”. Alisema Dkt. Kijazi
Aidha, Dkt. Kijazi alielezea mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi cha mwaka mmoja wakati Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa SADC licha ya changamoto za ugonjwa wa COVID-19, ikiwa ni pamoja na:
- Utekelezaji wa miradi mbalimbali itakayochangia kuboresha huduma za hali ya hewa hususani uboreshaji wa miundombinu. Miradi hii ni pamoja na mradi wa kikanda wa ”Southern African Regional Climate Information Service for Disaster Resilience Development (SARCIS-DR)” ambao umefanikisha upatikanaji wa vituo vinavyojiendesha vyenyewe ”Automatic Weather Stations-(AWS)" na Kompyuta mahsusi za uchakataji wa taarifa za hali ya hewa ”High Perfoming Computers (HPC)” ambazo zitasaidia katika juhudi za nchi wanachama kukabiliana na majanga ya hali mbaya ya hewa.
- Wataalamu wa hali ya hewa walipata mafunzo mbalimbali kupitia warsha zilizoandaliwa na Sekretariati ya SADC. Mfano ni warsha ya mafunzo ya kujenga uwezo wa wataalamu wa hali ya hewa ili waweze kutoa utabiri bora zaidi wa msimu yaliyoendeshwa sambamba na kongamano la 23 la nchi za SADC la utoaji wa utabiri wa hali ya hewa wa msimu linalojulikana kama “Southern Africa Climate Outlook Forum (SARCOF)”. Mafunzo haya yalifanyika kuanzia tarehe 19 hadi 27 Agosti 2020, Luanda, Angola. Utabiri huo wa hali ya hewa wa msimu-kikanda husaidia kila nchi mwanachama kuandaa utabiri wa hali ya hewa wa msimu katika eneo la nchi zao.
- Kuendelea kufanyika kwa mikutano muhimu iliyochangia katika maamuzi ya uendelezaji wa sekta ya hali ya hewa kwa nchi wanachama wa SADC kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Mikutano hiyo ni pamoja na Mkutano wa Mawaziri wa Sekta za Uchukuzi, TEHAMA, na Hali ya Hewa, Mkutano wa Mawaziri wanaoratibu Maafa na Mikutano ya Wakuu wa Taasisi za hali ya hewa za SADC.
Mkutano huo wa SCOM ulihudhuriwa na Wakuu wa Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi Wanachama wa SADC, Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Umoja wa Taasisi za Hali ya Hewa za Kusini mwa Afrika (Meteorological Association of Southern Africa (MASA).