Dar es Salaam;
Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika
la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi amesisitiza kwamba suala la kuwajengea uwezo wataalamu wa
hali ya hewa wanaotoa huduma kwa watumiaji wa bahari ni la umuhimu wa kipekee
ili kuweza kukidhi mahitaji ya wadau hao wa bahari.
Amezungumza
hayo wakati akishiriki katika mkutano wa Bodi ya Mashirikiano kati ya WMO na
Kamisheni ya Kimataifa ya Masuala ya Huduma za Hali ya Hewa kwa watumiaji wa Bahari
(WMO-Intergovernmental Oceanographic Commission Collaborative Board (WMO-IOC
JCB)) uliofanyika tarehe 16 Juni, 2020 kwa njia ya mtandao (videoconference).
“Taasisi
nyingi za Hali ya Hewa zina vituo vya kufuatilia hali ya bahari na kutoa huduma
kwa wadau, lakini wataalamu bado hawajapewa ujuzi wa kutosha kuhusiana na
mahitaji ya wadau. Hivyo tunahitaji kushughulikia masuala muhimu ya kisera na
kimkakati yatakayowezesha kujenga uwezo kwa wataalamu katika ngazi ya nchi, kwani
wataalamu hao bado hawajapewa elimu na ujuzi wa kutosha kukidhi mahitaji ya
wadau wa bahari wanaowahudumia”. Alisema Dkt. Kijazi.
Aidha,
Dkt. Kijazi alitaja kipaumbele kingine kuwa ni kuimarishwa kwa miundombinu ya
upimaji na ufuatiliaji katika maeneo ya bahari ili kuwezesha upatikanaji wa
takwimu ambazo ni muhimu katika utoaji wa huduma katika sekta hii, pamoja na
ushirikiano kati ya taasisi husika kuanzia ngazi ya nchi.
Bodi
ya mashirikiano katika ya WMO na IOC (WMO-IOC Joint Collaborative Board)
huratibu maeneo ya mashirikiano kati ya WMO na IOC, na kwa sasa pamoja na
masuala mengine itashughulikia pia suala la kujenga uwezo katika maeneo ya
mashirikiano. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja rasimu
ya mkakati wa miaka kumi (10) wa kujenga uwezo, ambao utahusisha utaratibu wa
kufanya kazi pamoja; utaratibu wa kushirikiana na washirika wengine; na uendelevu
katika shughuli za kujenga uwezo.
Bodi
hiyo ilikutana kwa lengo la kujadili vipaumbele vya maeneo ya ushirikiano
yanayohitaji kujengewa uwezo, ambayo yatashughulikiwa na majopo ya kujenga
uwezo ya WMO na IOC. Dkt. Kijazi ni Mwenyekiti
wa Jopo la WMO la kujenga uwezo (WMO Capacity Development Panel).
No comments:
Post a Comment