Friday, June 26, 2020

TMA KUWA MSTARI WA MBELE KUSAIDIA HUDUMA ZA HALI YA HEWA KATIKA NCHI ZA AFRIKA


Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Daouda Konate (kushoto aliyevaa miwani) aliyekuwa Mwenyekiti wa Kikao akimsikiliza Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas (kushoto aliyekaa katikati ya wataalamu) akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika (RA I) katika Mkutano wa viongozi wa WMO Kanda ya Afrika (WMO Regional Association I Management Group) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 hadi 12 Juni 2020.

Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi akichangia katika taarifa ya utekelezaji wa shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika (RA I) iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa WMO, Prof. Petteri Taalas katika  Mkutano wa viongozi wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya Afrika (WMO Regional Association I Management Group) uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 10 hadi 12 Juni 2020.

Dar es Salaam; 
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema iko tayari kushirikiana na Taasisi za Hali ya Hewa za Nchi  Wanachama wa Shirika la Hali ya Hewa  Duniani (WMO) Kanda ya Afrika (WMO Regional Association  I (RA I), kusaidia kuboresha huduma za hali ya hewa katika maeneo ambayo imekwisha kupiga hatua zaidi. Hayo yalisemwa katika Mkutano wa Viongozi wa WMO Kanda ya Afrika (RA I Management Group), uliofanyika kwa njia ya mtandao (videoconference) kuanzia tarehe 10 hadi  12 Juni, 2020.

Akizungumza wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa WMO Prof. Petteri Taalas, Mkurugenzi Mkuu wa TMA ambaye pia ni Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa  Duniani (WMO), Dkt. Agnes Kijazi alieleza kwamba Tanzania imepiga hatua katika uandaaji wa majarida ya taarifa za klaimatolojia (hali ya hewa ya muda mrefu) kwa nchi ya Tanzania, hivyo iko tayari kusaidia nchi nyingine Wanachama wa WMO Kanda ya Afrika.
“Kuhusiana na uandaaji wa taarifa za klaimatolojia (hali ya hewa ya muda mrefu), nafurahi kusema kwamba Tanzania tumekwishaanza kutoa machapisho hayo tangu mwaka 2011 na tuko tayari kusaidia katika ngazi ya Kanda”. Alisema Dkt. Kijazi.

Aidha, aliendelea kusisitiza utayari wa Tanzania katika kusaidia nchi zingine wakati akielezea faidi za kuwa na Mfumo wa Kitaifa wa Huduma za Hali ya Hewa (National Framework for Climate Services) ambapo alisema kwa upande wa Tanzania, mfumo huo umesaidia kuboresha sana huduma za hali ya hewa. Moja ya uboreshaji huo ni  kutungwa kwa sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Na. 2 ya mwaka 2019 ambayo ina malengo ya kuiwezesha TMA kusimamia vyema huduma zote za hali ya hewa zinazotolewa nchini Tanzania na hivyo kutekeleza vyema program zote za WMO kwa ustawi wa wananchi wa Tanzania na dunia kwa ujumla hasa ikizingatiwa kwamba hali ya hewa haina mipaka. Aliongeza Dr. Kijazi.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa WMO alimpongeza Dr. Kijazi kwa umahiri anaoonyesha katika kushiriki kwenye program za WMO katika nafasi yake kama Mwakilishi wa kudumu wa Tanzania katika Shrika la Hali ya Hewa Duniani na kama Makamu wa tatu wa rais wa shirika hilo. Aidha, aliipongeza Tanzania kuwa imefanya kazi kubwa katika kutekeleza program za WMO ikiwemo program ya Global Framework for Climate services na akasema WMO inafurahishwa na utayari wa Tanzania kusaidia nchi zingine barani  Afrika.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi wa WMO Ofisi ya Kanda ya Afrika, Dkt. Amos Makarau alitoa taarifa ya wataalamu walioteuliwa kuongoza majopo na vikosi kazi mbalimbali vya WMO, ambapo taarifa hiyo ilibainisha uteuzi wa Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Dkt. Pascal Waniha kuwa Makamu Mwenyekiti (Vice Chair) wa   Kikosi Kazi cha Mtandao wa Dunia wa Upimaji wa Hali ya Hewa (Study Group on Global Basic Observing Network (GBON), akiwa miongoni mwa wataalamu watatu (3) walioteuliwa kutoka Afrika kuongoza majopo na vikosi kazi vya WMO.  Hii ni sifa na heshima kwa Tanzania na TMA.

Awali akifungua mkutano huo, Mwenyekiti ambaye ni Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) Kanda ya Afrika, Dkt. Daouda Konate kutoka Ivory Coast alisema lengo la mkutano ni kujadili utekelezaji wa shughuli za huduma za hali ya hewa katika Kanda ya Afrika. Mkutano ulijadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na shughuli za WMO katika Kanda ya Afrika; utekelezaji wa maazimio ya Mkutano Mkuu wa WMO (WMO Congress) wa mwezi Juni, 2019; Uteuzi wa wataalamu katika majopo na vikosikazi vya WMO; Vipaumbele vya Kanda; Mpango Mkakati wa Kanda; na athari za janga la ugonjwa wa “COVID-19” katika huduma za hali ya hewa. 

Aidha, baada ya majidiliano ya kina, mkutano ulikuja na  mapendekezo ambayo  ni pamoja na: kutoa nafasi kwa watunga sera kushiriki katika mikutano ya Kanda ya Masuala ya hali ya hewa; na kuziomba Nchi Wanachama kuridhia katiba ya Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya hali ya hewa “African Ministerial Conference on Meteorology (AMCOMET).

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...