Thursday, November 29, 2018

TMS YAWAPONGEZA DKT.BURUHANI NYENZI KWA KUCHAGULIWA KUWA MAKAMU MWENYEKITI WA JUKWAA LA KIMATAIFA LA WATAALAMU WA HALI YA HEWA (IFMS) NA DKT. AGNES KIJAZI KWA KUTEULIWA NA KATIBU MKUU WA UMOJA WA MATAIFA (UN) KUWA MJUMBE WA JOPO LA WATAALAM KUMI (10-MEMBER GROUP).




Chama cha Wataalamu wa Hali ya Hewa Tanzania (Tanzania Meteorological Society-TMS) kimewapongeza Dkt. Buruhani Nyenzi ambaye pia ni rais wa chama hicho kwa kuchaguliwa kuwa makamu rais wa Jukwaa la Kimataifa la Wataalamu wa hali ya hewa ( International Forum of Meteorological Societies- IFMS) na Dk. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu wa TMA kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuwa mjumbe wa Jopo la wataalam kumi (10-member Group) lenye jukumu la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu namna ambavyo sayansi, teknolojia na ubunifu (STI) zinavyoweza kutumika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu ya umoja huo (Sustainable Development Goals(SDGs).

Pongezi hizo zilitolewa katika mkutano wa TMS uliofanyika jijini Dar es Salaam kwa kujumuisha wanachama wa TMS kutoka maeneo mbali mbali nchini. Makamu wa rais wa TMS Dkt. Clavery Tungaraza kutoka chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) na Katibu wa TMS Dkt.Ladislaus Chang'a kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kwa pamoja walisema mafanikio hayo ni mafanikio ya TMS kwani Dkt. Nyenzi na Dkt.Kijazi ni wanachama wa TMS.

Tunampongeza sana rais wa Umoja wetu Dkt. Nyenzi kwa kuchaguliwa kuwa makamu wa rais wa IFMS na Dkt. Kijazi ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa kuteuliwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo la wataalam kumi (10) kuunda kamati ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja huo, tunatambua nafasi hizi ni fahari kwa wana TMS wote kwani ni fursa kwa TMS  kuitangaza nchi yetu kimataifa ‘alisema Dkt. Tungaraza’

Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwashukuru sana wanachama wote kwa pongezi na kusisitiza ushirikiano ili aweze kuipeperusha vyema bendera ya nchi kimataifa. Jukwaa lile ni la kimataifa hivyo mtanzania kuwa miongoni mwa viongozi wa juu wa jukwaa (forum) hilo ni jambo la kujivunia sisi kama wana TMS na nchi yetu kwa ujumla. Akipokea pongezi hizo Dkt. Kijazi aliwashukuru wanachama na kufafanua kwamba wao kama wana sayansi mawazo yao ni muhimu katika kumuwezesha kutekeleza jukumu hilo kubwa la kimataifa. Uteuzi huu ni fahari kwa TMS na nchi yetu kwa ujumla hasa ikizingatiwa kwamba katika kundi la watu kumi tu kwa dunia nzima Tanzania nayo inatajwa ‘alisema Dkt. Kijazi.’

Wakati huo huo wanachuo waliomaliza na kufanya vizuri kwa masomo ya elimu ya shahada ya sayansi ya hali ya hewa (Bsc. Meteorology) kwa mwaka 2017 Bi. Aisha Nassor (mwanafunzi bora wa jumla), Bi. Leila Muhoma na Bw. Kekazuri Elly walipongezwa kwa jitihada zao na kupatiwa zawadi ya cheti na fedha taslim. Akikabidhi zawadi hizo Dkt. Kijazi alisema anafurahishwa kuona wanawake wanaongoza katika mafunzo hayo ya BSc Meteorology yanayotolewa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kwa upande wake Dkt. Nyenzi aliwajulisha wanachama kwamba TMS itaendelea kuwapongeza wanafunzi wanaofanya vizuri kwa lengo la kuchangia katika kuendeleza taaluma ya hali ya hewa hapa nchini.

Imeandaliwa na;
Ofisi ya Uhusiano
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA)

Monday, November 26, 2018

TMA YAZINDUA PROGRAMU MPYA YA KISASA YA KUSAMBAZA UTABIRI WA KILA SIKU WA HALI YAHEWA KWENYE TELEVISHENI (LUNINGA)



26/11/2018; DAR ES SALAAM

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imezindua rasmi programu mpya ya usambazaji wa utabiri wa kila siku wa hali ya hewa kwa njia ya televisheni kwa kutumia teknolojia ya kidigitali ya kisasa “Full HD” katika mkutano na vyombo vya habari, Makao Makuu ya TMA, Ubungo Plaza Dar es Salaam. 

Akizindua rasmi programu hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA Dkt. Agnes Kijazi alivishukuru vyombo vya habari hapa nchini kwa kushirikiana na Mamlaka katika kufikisha taarifa za hali ya hewa kwa jamii pia alisisitiza lengo la Mamlaka kuboresha ubora wa huduma zake kwa jamii kwa kufuata maoni yao.

‘Napenda kuvishukuru vyombo vya habari kwa ushirikiano mnaotupatia katika kusambaza taarifa za hali ya hewa kwa jamii na maoni yenu kuhusu uboreshaji wa huduma zetu, Mamlaka imekuwa sikivu na kufanyia kazi maoni ambayo mmekuwa mkiyatoa’.

Mamlaka imekuwa ikiboresha huduma zake kwa jamii ili kukidhi matakwa ya watumiaji  na miongoni mwa matakwa hayo ni pamoja na kuwa na muonekano wa ‘graphics’ zenye mvuto katika utabiri wa kila siku unaotolewa na televisheni mbalimbali za habari hapa nchini. 

‘TMA inatambua kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika zilizopiga hatua kubwa katika kuboresha utangazaji wa njia ya televisheni ambapo kwa sasa imeshaingia katika urushaji kwa njia ya kidigitali. Aidha TMA ikiwa ni mmoja wa wadau wanaotumia vyombo vya habari hususan televisheni  katika kufikisha taarifa zake kwa jamii imeona pia ni muhimu kuboresha miundombinu yake ili kuendana na mabadiliko hayo’ alisema Dkt. Kijazi.

Dkt. Kijazi aliishukuru Taasisi ya Hali ya Hewa ya Uingereza ambayo kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) waliisaidia TMA kupata ‘software’ hiyo ya kisasa (High Definition) na pia kutoa mafunzo kwa wataalam wa TMA.
Kutokana na huduma hizo za usambazaji zilizoboreshwa Dkt. Kijazi aliviomba vyombo vyote vya habari vinavyotoa taarifa kwa jamii kupitia Televisheni kushirikiana na TMA ili kusambaza utabiri wa kila siku wa hali ya hewa. Alisema utabiri wa kila siku ni muhimu kwa usalama wa watu na mali zao pia kwa maendeleo ya Taifa letu, hivyo wote tushirikiane kulijenga Taifa letu.


Thursday, November 22, 2018

VIONGOZI TUGHE WATAKIWA KUWA VIELELEZO VYA UADILIFU KWENYE MAENEO YA KAZI


Halmashauri ya TUGHE ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) na menejiment ya TMA wamejumuika katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TMA makao makuu,Ubungo Plaza tarehe 22 Novemba 2018.

Katika kikao hicho, mkurugenzi mkuu wa TMA Dkt.Agnes Kijazi aliwataka viongozi wa TUGHE kuwa vielelezo vya uadilifu kwenye maeneo yao ya kazi.

Aliongezea kuwa ni vyema viongozi  wa TUGHE na menejiment ya TMA kuweka vipaumbele vya ufanisi wa kazi ili kufanikisha maendeleo ya nchi kupitia huduma za hali ya hewa zinazotolewa na TMA

Wakati huo huo alisisitiza haki iende sambamba na wajibu kwa kuzingatia utendaji kazi wa pamoja (team work)

Kwa upande wa TUGHE katibu wake,bw.Benjamin Bikulamchi alishukuru Menejiment ya TMA kwa ushirikiano uliopo baina yao pamoja na kutoa pongezi kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuboresha maslahi ya wafanyakazi

Kikao hicho cha siku moja kilijadili masuala mbalimbali kwa manufaa ya Mamlaka kwa ujumla
Halmashauri ya TUGHE katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Agnes Kijazi na baadhi ya viongozi wa TMA
Halmashauri ya TUGHE katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa halmashauri hiyo wanaotarajiwa kustaafu
Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kikao hicho


Wednesday, November 21, 2018

TMS YAJIZATITI KUTEKELEZA MFUMO WA TAIFA WA HUDUMA ZA HALI YA HEWA

Tarehe 21/11/2018, Dar es Salaam, mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania alifungua mkutano wa chama cha wataalamu wa hali ya hewa Tanzania (Tanzanian Meteorological Society (TMS) kilichofanyika katika ukumbi wa Ubungo Plaza na kuhudhuriwa na wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini. 

Wakati akifungua mkutano huo, Dkt. Kijazi  aliwapongeza TMS kwa nia waliyoionesha ya kuhakikisha wanaweka msisitizo wa utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa uliozinduliwa tarehe 21 Agosti 2018. ‘napenda kuwapongeza na nimefarijika kusikia kuwa mipango mikakati ya utekelezaji wa majukumu ya TMS imelenga na inaenda sambamba na utekelezaji wa malengo/madhumuni ya Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa, hii ni hatua nzuri kwa fani ya hali ya hewa na TMS pia.’, alisema dkt. Kijazi

Katika hatua nyingine, Dkt. Buruhani Nyenzi, ambaye ni rais wa TMS alielezea kuwa mojawapo ya kipaumbele cha TMS ni kuhamasisha utekelezaji wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa, ambao una umuhimu wake katika shughuli mbalimbali zinazohusisha hali ya hewa na  maendeleo ya nchi kwa ujumla. 

Lengo kuu la mkutano ilikuwa kujadili mpango mkakati wa TMS na namna ya kuendeleza jitihada za utekelezaji (matumizi) wa Mfumo wa Taifa wa Huduma za Hali za Hewa kwa manufaa ya wanachama na sekta ya hali ya hewa kwa ujumla..

Mkutano huo umedhaminiwa na Programu ya Kidunia ya Huduma za Hali ya Hewa, awamu ya pili (Global Framework for Climate Services Adaption Programme in Africa (GFCS APA)- Phase II)  kupitia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) chini shirika la misaada la Norway (Norwegian Agency for Development Cooperation (NORAD)). 
  
Imetolewa:
Monica Mutoni,
Ofisi ya Uhusiano,
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
 


Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...