Wachezaji
wa Uchukuzi SC wakiwa wamevipanga vikombe 11 walivyotwaa kwenye michezo
mbalimbali ya Mei Mosi, iliyomalizika juzi mkoani Dodoma
TIMU ya Uchukuzi SC iliyopo chini ya
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imeibuka kinara kwenye mashindano ya
Mei Mosi baada ya kutwaa vikombe 11 vya michezo mbalimbali. Timu hiyo inajumuisha wanamichezo kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania.
Timu hiyo imetwaa ubingwa katika michezo
ya netiboli, baiskeli na bao (wanaume), kamba
(wanawake na wanaume); huku vikombe vya ushindi wa pili ni vya michezo ya bao
(wanawake) na draft (wanaume); wakati vya ushindi wa tatu ni katika soka, karata
(wanaume), riadha (wanawake na wanaume).
Hata hivyo, kutokana na uwingi wa vikombe
timu hiyo ilitangazwa mshindi wa jumla kwenye sherehe za Mei
Mosi na kukabidhiwa kombe na Mh. Rais John Magufuli.
Timu nyingine na idadi ya vikombe
zilizopata ni TAMISEMI saba kikiwemo cha ubingwa wa soka baada ya kuwafunga GGM
katika fainali kwa magoli 2-0, huku TPDC wakiwa na vikombe vitano sawa na
Tanesco.Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),
wamejikusanyia vikombe vinne, Ujenzi vikombe viwili, na Mawasiliano,
Ukaguzi na Halmashauri ya Nyasa kila
mmoja wana kikombe kimoja kila mmoja.
Awali katika michezo iliyochezwa jana
timu ya Uchukuzi SC iliwafunga Tamisemi kwa magoli 18-15 katika mchezo wa
netiboli, ambapo wafungaji wake Tatu Kitula na Matalena Mhagama waliwapeleka
puta wapinzani wao na hadi mapumziko walikuwa mbele kwa magoli 11-7.
Washindi wote walikabidhiwa kombe na
mgeni rasmi Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Reli Tanzania (TRAWU), Mussa
Kalala, ambaye katika hotuba yake
aliwashutumu viongozi walioshindwa kupeleka timu zao kwenye mashindano hayo na
kusema michezo mahala pa kazi husaidia kuijenga miili ya wafanyakazi kuendelea
kuwa mikakamavu na kuwa na afya bora, ambapo hutoa huduma bora iliyotukuka na
kuzalisha tija zaidi.