Thursday, June 28, 2018

WATAALAMU TUMIENI TAARIFA ZA TMA-MAJALIWA

Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akibonyeza kitufe kuashiria uzindua vituo 51 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dododma tarehe 27 Juni 2018.Pichani kushoto kwake ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Mhe. Jinista Mhagama.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa  na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP Bi. Natalia Bouclywakizindua vituo 51 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dododma tarehe 27 Juni 2018.Pichani kushoto kwa waziri mkuu ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Mhe. Jinista Mhagama.
Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa akitazama kifaa cha kupima kiasi cha mvua baada ya uzindua vituo 51 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dododma tarehe 27 Juni 2018.Wengine pichani kutoka kushoto ni Waziri wa nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na wenye ulemavu Mhe. Jinista Mhagama, waziri wa Maji Mhe. Mhandisi. Isaack Kamwele, Mwakilishi Mkaazi wa UNDP Bi. Natalia Boucly, Kaimu Mkurugenzi Mkuu TMA Dkt. Ladislaus Chang'a na kulia ni Mbunge wa Viti Maalum kutoka mkoa wa Dodoma Bi.Felister Bura.
Baadhi ya wananchi walishiriki katika uzindua vituo 51 vya hali ya hewa vinavyojiendesha vyenyewe katika viwanja vya Halmashauri ya Wilaya ya Bahi, Dododma tarehe 27 Juni 2018.(Picha zote kwa hisani ya Ofisi ya Waziri Mkuu)


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wataalamu wa sekta za kilimo, mifugo na maji watumie taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ili waongeze ufanisi katika utendaji kazi wao.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizindua vituo 51 vya kufuatilia taarifa za hali ya hewa, vituo 15 vya haidrolojia, kanzidata ya taarifa za hali ya hewa na kituo cha operesheni na mawasiliano ya dharura wilayani Bahi, Dodoma.

Amesema kuwa kuongezeka kwa vituo vipya vya kisasa vya ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya hewa kumeboresha uhakika wa utabiri kutoka asilimia 81 hadi 87 kama inavyoshuhudiwa kwenye taarifa zinazotolewa katika siku za hivi karibuni. “Hivi sasa tukiambiwa kwamba mvua itanyesha katika maeneo fulani tunakuwa na uhakika kwa asilimia 87 ya utabiri huo,”. 

“Vituo hivi ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa nchi wa utoaji wa huduma za hali ya hewa na haidrolojia kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuongeza ufanisi katika utoaji wa tahadhari za awali za majanga yanayosababishwa na hali mbaya ya hewa na mabadiliko ya tabianchi,”. 

Amesema kupitia mradi huo uliofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Serikali imeweza kufungua vituo 51 vya kisasa vya hali ya hewa katika maeneo mbalimbali nchini na vituo 15 vya kupima ujazo wa maji kwenye mito iliyopo kwenye mabonde ya Pangani, Ruvuma na Pwani ya Kusini ambavyo vinajiendesha vyenyewe. 

“Pia, mradi huu umeiwezesha Serikali kuanzisha kanzidata ya takwimu na taarifa za mafuriko         na ukame na taarifa za hali ya hewa na kuondoa ucheleweshwaji wa kupata takwimu au taarifa kutoka Wizara moja kwenda Wizara nyingine,” amesema. 

Hata hivyo, Waziri Mkuu ameziagiza Wizara ya Maji na Umwagiliaji na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano zitenge fedha kwenye bajeti zao ili ziweze kufuatilia na kusimamia mradi huo baada ya wafadhili kumaliza muda wao.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, itaendelea kushirikiana na washirika wa maendeleo katika kuhakikisha kuwa vituo na mifumo iliyowekwa inafanya kazi ipasavyo kwa usimamizi bora ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama, Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isack Kamwelwe na Waziri wa Kilimo, Dkt. Charles Tizeba.

Wengine ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola, Wabunge na Mwakilishi Mkaazi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Bibi Natalie Boucly.

No comments:

Post a Comment

Featured Post

DKT. KIJAZI: KIWANGO CHA USAHIHI WA UTABIRI WA MSIMU WA VULI 2019 KIWE CHA JUU ZAIDI.

Mkurugenzi mkuu wa TMA na Makamu wa Tatu wa Rais wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani Dkt. Agnes Kijazi (katikati mwenye suti nyeusi) waka...